Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Ally Mohamed Keissy

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nichangie Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Spika, kusema ukweli tukichunguza, labda kwenye bahari kuu, lakini kwenye maziwa samaki wamepungua sana. Nitatolea mfano Lake Rukwa. Lake Rukwa miaka kumi iliyopita kulikuwa na samaki wengi sana, wanalisha mpaka Zambia na sehemu mbalimbali za nchi hii. Leo Lake Rukwa hakuna samaki hata mmoja. Sisi kule kwetu Lake Tanganyika wanavulia mpaka vyandarua. Tunagawa vyandarua bure, wananchi wetu wanachukua vyandarua wanafanya ndiyo uvuvi.

Mheshimiwa Spika, hizi samaki tulizopewa na Mwenyezi Mungu; je, wazazi wa zamani miaka 50 iliyopita wangetumia uvuvi kama huu uliopo sasa, tungekuta samaki? Haiwezekani. Lazima tuwaelimishe wananchi wetu waache uvuvi haramu, uvuvi wa ovyo ovyo. Lake Victoria miaka kumi tu, leo ni asilimia 50 ya samaki. Miaka kumi ijayo Ziwa Victoria hakuna samaki hata mmoja, hakuna. Hata maziwa yote yatakuwa ni hivyo hivyo.

T A A R I F A . . .

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, huyu hajavua. Mimi nimevua tangu utoto wangu. Mpaka sasa piga simu kwa Afisa uvuvi, Kipili, atakwambia ni vyandarua vingapi vimekamatwa? Kwa ushaihidi vyandarua vinavua, wewe hujui chochote, wala hujaingia majini. Mwanamke gani akaingia majini kuvua? Acha kudanganya Bunge. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, hizi samaki tumepewa sisi na vizazi vijavyo. Haiwezekani mtu ku-support uvuvi haramu, lazima tuwaelimishe wanachi wetu waache uvuvi haramu. Leo nenda Ziwa Tanganyika, wanakuja Wa-congoman, sisi watu wetu huku hawaendi Zaire kuvua, lakini nenda kwenye visiwa vya Mvuna, nenda Mwanakerenge, wamejaa Wa-congoman na nyavu haramu wanavua samaki na dagaa. Yeye anasema ana ziwa, alishaingia ziwani kuvua huyu? Haiwezekani! (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, hizi samaki tumepewa za urithi kulinda vizaizi vijavyo. Leo sisi tunavua, wanavua vizazi miaka 15 iliyopita hakuna samaki. Mfano, Ziwa Rukwa muulize Mheshimiwa Malocha, Mbunge wa Ziwa Rukwa, waulize Wabunge wa Ziwa Rukwa, hakuna samaki Lake Rukwa, samaki zote zimekwisha na ilikuwa samaki malori na malori wanapeleka Zambia kuuza. Leo samaki Lake Rukwa hakuna.

Mheshimiwa Spika, hivyo hivyo na Ziwa Tanganyika, ukianza tu mwezi wanaingia kuvua migebuka ndugu yangu haijafika hata nchi sita au nchi saba, wanaita nyamnyam. Migebuka kwa kawaida inangojewa iwe mikubwa, lakini wanaingia kuvua kuharibu samaki mpaka wanatupa kule Ziwa Tanganyika. Haiwezekani! Hizi tumepewa ni rasilimali yetu na vizazi vijavyo. Haiwezekani watu waingie kuvua jinsi wanavyovua.

Mheshimiwa Spika, nimeona viwanda vilivyokuwa Lake Victoria, leo vimebaki nusu, hakuna viwanda. Lazima tulinde vizazi vya samaki vinavyozaana samaki. Ile Sheria ya kuvua mita 500 kutoka mwambao wa Ziwa Tanganyika haitekelezeki. Jana tu nimepigiwa simu na mtu wa Kabwe, kuna kokoro zaidi ya kumi zinavutwa kule Kabwe, nimepigia Bwana Samaki simu, chunguza hizo kokoro. Kwa majina, ninao. Kokoro inavuta na mayai na kila kitu, imeharibu samaki. Ndugu zangu tusitake kupata kura kwa ajili ya kubembeleza ili tuharibu uchumi wa nchi. Tuelimishe watu wetu.

Mheshimiwa Spika, hatuwezi kubembeleza, Waheshimiwa Wabunge na Madiwani ndio wanaharibu nchi hii kwa kubembeleza kura wanadanganya wananchi. Tuwe wakweli. Hatuwezi kwenda kinyume tuharibu uchumi wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nachangia habari ya mifugo. Tumenunua ndege Bombadier kwa ajili ya kukuza utalii. Tutakuza utalii kwa kutazama ng’ombe katika nchi? Tutakuza utalii kwa ajili ya kuja kutazama ng’ombe au kutazama twiga na tembo na simba na chui? Leo tunataka tupunguze mbuga za wanyama kwa ajili ya wachungaji. Ndugu zangu tufuge kisasa, siyo tuchunge.

Mheshimiwa Spika, hatutaki uchungaji! Ng’ombe ukimkuta kachoka, mchungaji kachoka, haiji. Hakuna ng’ombe zaidi ya kilo 150. Ukimchinja ukitoa utumbo na kila kitu unapata kilo 100 au kilo 70. Utasema nakuza mifugo? Haiwezekani. Lazima tuige nchi zinazoendelea kwa ajili ya ufugaji. Hatuwezi kuwa wachungaji kila siku, mchungaji anachoka na ng’ombe anachoka, haiji. Lazima tutafute sehemu ya kuchungia mifugo yao, wakae sehemu moja, siyo kuhama hama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nazungumza habari ya Nkasi, kuna ng’ombe zaidi ya 130,000. Nkasi ilikuwa ni sehemu ya kilimo, sasa imekuwa na mwisho italeta migogoro kwa ajili ya wachungaji. Wanakuja na mifugo, mifugo inakondeana kila sehemu wanataka majosho na Serikali ndugu zangu, tufuge ng’ombe wa kisasa. Tuna ng’ombe zaidi ya 25,000 lakini hata maziwa hatuna, nyama ya kisasa hatuna, tunaagiza nyama ya kisasa nje ili watu wale nyama. Ukitaka steki, hakuna nyama ya steki, maana yake ng’ombe kakonda ni mifupa mitupu. Haiji! Lazima tupunguze mifugo, tufuge mifugo yenye uwezo ili ng’ombe afike kilo 800 au kilo 900.

Mheshimiwa Spika, ndugu zangu hatuwezi kuwa wachungaji sehemu zote tunakwenda barabarani kuchunga, hakuna hicho kitu. Lazima tufuate sheria na sheria ni msumeno. Haiwezekani wewe kukutetea hapa kwa ajili ya kuja kuomba kura.

Mheshimiwa Spika, hata mimi niliingia Bungeni kwa kuomba kura, lakini nasema ukweli na watu wangu wananisikia. Siwezi kuwatetea wavuvi haramu wanakokoa kila kitu mpaka mayai ya samaki na mjukuu wangu aje kuvua wapi? Siwezi kumtetea mfugaji anaharibu ardhi, mito inakauka, vyanzo vya maji vinakauka, tutakunywa wapi maji? Wakati nchi yetu imebarikiwa na maji nchi nzima, lakini leo vyanzo vya maji vyote vimekwisha. Haiji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatubembelezi kura kwa njia ya namna hiyo ya kudanganya danganya. Tuwaelimishe wananchi wetu, tuweze kwenda sawa na hili tutakwenda sawa. Hata akija kiongozi anaharibu nchi, ndiyo tumchague huyo, haiwezekani! Lazima twende na sheria, tufuate sheria. Sheria tumetunga Bungeni hapa, hakuna sheria Mheshimiwa Mpina alizotoa mfukoni kwake akaenda kwa wavuvi, hakuna. Sheria zimetoka Bungeni hapa, hazikutoka popote. Sheria ni msumeno, hata ningekuwa mimi Waziri nitakuwa hivyo hivyo, wewe ukiwa Waziri utakuwa ni hivyo hivyo au kwa sababu unaomba urudi Bungeni, hili Bunge ndugu zangu, umekuja, utatolewa, atakuja mwingine, ataendelea. Ahsante sana.