Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Mattar Ali Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shaurimoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Niendeleze hapa alipoacha kaka yangu Mheshimiwa Mgimwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tutakuwa na mikakati thabiti ndani ya Wizara hii na kama tutaishauri Serikali vizuri, itasikia tunavyosema Waheshimiwa Wabunge. Jambo la kwanza kwenye tasnia ya maziwa, lazima Wizara zetu yaweze kutumika maziwa ambayo tunazalisha nchini kwetu. Tunaweza tukai-promote sekta hii ikawa inafanya kazi vizuri kuliko kitu chochote, lakini sisi wenyewe ndani yetu tunaanza kutumia maziwa ya kuagiza nje. Hivi sekta hii itakua lini? Naomba sana Serikali tubadilishe utumiaji wa maziwa, twende katika utumiaji wa maziwa tunayozalisha ndani sisi wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ukiangalia bajeti ambayo ilikuwa imepangwa kutolewa katika Wizara hii, jambo la kusikitisha sana, bajeti hii haijaenda, haina hata kitu kimoja. Hawa Mawaziri wanachapa kazi vizuri, naamini wana jitihada sana ya kufanya kazi. Nawashukuru sana hawa Mawaziri, lakini kutokana na bajeti ambayo iko hapa, waliyopewa hawa, basi haiwezi kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ni uvuvi wa Bahari Kuu ambao nauzungumzia kwa kina. Nchi yetu tukitaka tuendelee, tufike mahali halisi tunapopataka pasipo kuangalia madini, basi tuangalie kwenye uvuvi wa Bahari Kuu. Tukisimamia uvuvi wa Bahari Kuu tunaweza kufika mahali pazuri kuliko kuangalia madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, baada ya macho kuangalia katika madini, basi tuangalie hapa kwenye uvuvi wa Bahari Kuu. Tukifanya kazi, tukipaimarisha vizuri katika uvuvi wa Bahari Kuu, haya matatizo ya uvuvi haramu na matatizo sijui ya maziwa, yote yataondoka. Nami kaka yangu Mheshimiwa Ulega namshauri kila siku, hebu twendeni kwenye uvuvi wa Bahari Kuu, tuangalieni, kuna nini? Sijui tumelogwa na nani?

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, tumesema katika Kamati tukilalamika kuhusu ununuaji wa meli na ujengaji wa gati. Ndani ya hotuba zetu hizi hatujaona mahali palipo na mkakati rasmi kwamba sasa tunaenda kuwekeza kwenye Bahari Kuu. Uchumi wa Bahari Kuu, wenzetu waliokuja kuwekeza ndani ya nchi yetu hii wanapata mafanikio makubwa, sisi tunabakia katika tozo ya leseni tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Wizara hii na Serikali iweze kusimamia uvuvi wa Bahari Kuu, kuhakikisha tunakwenda mahali pazuri. Naamini tukisimamia kidhati kwenye Bahari Kuu, basi tutakwenda tunapopataka.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, nigusie suala la ufugaji, bado hatujatoa elimu na bado hatujaamua kusimamia katika suala la ufugaji. Tukiangalia hata mifugo yetu, bado hatuna ng’ombe wanaoridhisha. Angalau ng’ombe unayemkamua maziwa umpe malisho bora. Kikitokea kiangazi kidogo tunashuhudia ng’ombe wanaokufa ni wengi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka tumekwenda ziara kuangalia ng’ombe, wanapukutika njiani kama majani. Tujipange katika suala la ufugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Ahsante. Tuwawezeshe wafugaji wetu, tuwape mikopo ya ng’ombe wa kisasa, tuwaelimishe ufugaji wa kisasa ili tupate maziwa mengi.