Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba nimshukuru Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia kwenye hii Wizara muhimu kabisa kwetu sisi tunaotoka kandokando ya ziwa, lakini pia maeneo ambayo kwa sasa kilio cha wananchi ni kwa kweli unyang’anyi mkubwa unaoendelea kufanywa na Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kusikitika kidogo, kuna bahati mbaya kwamba tunazungumza hapa kwa nguvu kubwa sana tukiwa tunazungumza maoni ambayo tunaamini waliotutuma ndiyo tunaleta, lakini majibu mepesi yanayokuja ni kwamba tumekamata Wabunge, tumekamata Madiwani ndiyo maana wanalalamika. Kama ziko kumbukumbu za Mbunge aliyewahi kukamatwa anavua samaki au na zana haramu, tungeomba sana leo wakati Waziri anahitimisha aseme ni Mbunge gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu hili linatia woga watu kuchangia kwa kuogopa kutuhumiwa na wengine wanaamini kila anayesema anasema kwa sababu ana maslahi. Kauli hii ilienda mbali zaidi, Mheshimiwa Waziri alikuwa na kikao na viongozi 260 akiandaa Operesheni yake ya Sangara awamu ya tatu. Kauli walizozitoa viongozi aliokuwa nao ni kwamba wanasiasa wanapotosha zoezi hili kwa sababu wana maslahi binafsi na kwa maana nyepesi wanasiasa ni sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ili kuliweka vizuri hili, kwanza ni vizuri sana akaweka kumbukumbu hizi sawa; anawazungumzia wanasiasa wapi wanaopotosha? Kwa sababu tunayoyazungumza sisi tunayazungumza kwa sababu tunayafahamu. Hata hivyo, ni vizuri sana pia viongozi wenzetu huko waliko kwa kuwa tunazungumza kuwawakilisha wananchi, wakafahamu kwamba sisi tunapokuja hapa tunakuja tumetumwa na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze sasa kuchangia; kwanza nianze na suala la operesheni ambayo inaendelea hivi sasa. Tulizungumza hapa na tukaomba mwongozo na tatizo kubwa halikuwa kupinga operesheni ya wavuvi haramu. Naomba niweke kumbukumbu vizuri; naunga mkono operesheni ya kupambana na uvuvi haramu, naunga mkono operesheni ya kupambana na zana haramu, naunga mkono dhamira ya Serikali ya kuongeza kipato kinachotokana na uvuvi na mifugo, yote ninaunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, unapotaka kufanya operesheni lazima uiwekee mipaa, lakini pawe na ile sense of humanity, kwamba ninaokwenda ku-deal nao ni binadamu. Tunao wavuvi kule ziwani, niliuliza swali na halijawahi kujibiwa mpaka leo. Unapotumia nyavu ziwani ya inchi sita iliyoruhusiwa na Serikali ambayo siyo zana haramu, ukaenda nayo ziwani ikiwa single ina uwezo wa kukamata samaki wanaozidi sentimita 50 na wanaopungua sentimita 50.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri na watu wake wote wanakiri kwamba nyavu hiyo kwa kawaida ratio inaweza ikawa mpaka ten percent ya nyavu ambazo ziko under size. Ni kwa nini operesheni ya Mheshimiwa Waziri inaendelea kukamata watu hata wenye samaki wawili? Kwa nini inaendelea kupiga watu faini ya mamilioni ya shilingi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye sheria, sheria zote za mambo ya uvuvi ambazo zipo kwenye Sheria ya Mwaka 2003 na regulations zake, zinazungumzia faini na ziko very clear. Hata hivyo, kwa sababu operesheni ililenga kukusanya pesa, ililenga kwenda kuhakikisha kwamba watu wanatoka barabarani, mtu anapigwa faini mpaka ya milioni 50 kwa kosa la kukutwa na samaki 10, 15 kwenye mtumbwi, na operesheni hii inalenga wavuvi wakubwa peke yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyozungumza wanakwenda kwenye mwalo wanaangalia mvuvi mwenye mitumbwi zaidi ya 30, wakifika wanamkamata, wakimkamata wanam-detain kwenye gari tangu asubuhi mpaka jioni yuko chini ya ulinzi. Wanamwambia faini ni milioni 20 wanatembea naye, akikosa wanamweka ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadaye wanasema wewe bila kuleta milioni 20 tutakufungulia kesi ya uhujumu. Watu wanakwenda kuuza nyumba, wanakwenda kuuza ng’ombe. Kwa nini tunafanya hivi kama tuna nia njema na operesheni? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliposema maneno haya, majibu yaliyotoka mepesi kutoka kwa Mheshimiwa Waziri anasema ni kwamba nikiondoa hiyo exemption ya ten percent zoezi zima la operesheni halina maana. Maana yake ni nini kama wataalam wake wamekiri kuna kasoro na lazima iwepo, kwa nini anasema akiondoa haina maana; maana yake ni kwamba lengo la Mheshimiwa Waziri ni kufilisi watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukichukua nyavu ya dagaa ukaenda nayo ziwani leo, ukizungusha ile nyavu ya dagaa utapata sangara, utapata furu na sangara utakaowapata ni wadogo wadogo na watakufa kabla hujawatoa ziwani. Nataka kujua Mheshimiwa Waziri, anawapeleka wapi hao samaki? Kwa sababu hao samaki atakapovua lazima waje na kokoro na dagaa, unawapeleka wapi? Wavuvi wote wa dagaa sasa hivi wanaogopa kuvua samaki, tulikuwa tunanunua kisado cha dagaa Sh.2,500, sasa kimepanda mpaka Sh.15,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niikumbushe Serikali, pamoja na lengo la kutafuta pesa kwenye samaki, samaki ni chakula kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa. Yaani kwa sisi tunaotoka Kanda ya Ziwa, samaki ni chakula namba moja. Wewe unapofikiria mapato ya nje, fikiria kwanza watu ambao wanafaidika na samaki hao. Kinachoendelea katika zoezi hili ni uonezi mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala la nyavu; hivi tunavyozungumza, nyavu hakuna madukani. Nyavu za dagaa license amepewa mtu mmoja, yuko Arusha, alikuwa anatengeneza neti za mbu, anatengeneza nyavu za dagaa, matokeo yake nyavu ikiingia ziwani miezi miwili imepasuka. Wavuvi wameacha kununua nyavu za Tanzania wananunua nyavu za magendo kutoka Kenya na Uganda, Serikali inakula hasara. Waziri amezuia nyavu zisiingie Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nyavu za sangara; nilizungumza hapa wakati nachangia hotuba ya Waziri Mkuu, wafanyabiashara wamelipia nyavu tangu mwezi wa kwanza ziko bandarini, wanaomba kibali nyavu ziingie Tanzania. Wengine wamelipia na ushuru miezi miwili, Waziri hasemi kwa nini anazuia, hasemi ataruhusu lini, watu wanaenda kupigwa storage. Hebu tuwaambie Watanzania tunataka nini hapa kwenye nyavu, nyavu zile Mheshimiwa Waziri anazozitaka ziko bandarini hataki ziingie kwenye soko. Tunataka watu wavulie nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu ambacho nafahamu na elimu yangu ndogo ya uchumi inaniambia ukitengeneza mazingira ya kupunguza supply kwenye soko ukasababisha demand ambayo haitarajiwi, bei ya nyavu itapanda na matokeo yake watu hawatanunua; ndiyo elimu yangu ya uchumi inavyoniambia. Sasa matokeo yake ni kwamba nyavu imepanda kutoka Sh.16,000 mpaka Sh.45,000 piece moja. Hiyo ambayo imepanda vifaa vyake vimepanda mara nne zaidi kwa sababu wanaoleta wote mali zao zimezuiliwa mpakani.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka Mheshimiwa Waziri aniambie, anazuia kwa maslahi ya nani? Sielewi. Kwa sababu kama anataka ku-control, apeleke mtu akakague kontena, kama anataka kuzuia atangazie watu wasilete nyavu. Watu wamelipa kodi wanamwomba kibali hataki, wanamwambia hiki, hataki, anataka nini, aseme. Kwa sababu ni rahisi sana kuwatangazia Watanzania wasiingize nyavu kutoka nje
tunategemea viwanda vya ndani, watu hawataleta. Sasa hasemi chochote, amekaa kimya, watu wanakula hasara, nyavu ziwani hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachosema hapa, nyavu sasa watu wanaanza kuendea nje ya nchi kwa sababu wanaona kuna urasimu; tunakula hasara. Kwa nini hili linatokea; tunamlinda nani? Kwa sababu lengo ni kulinda viwanda vya ndani, wakati huu viwanda vya ndani havina uwezo lazima uvuvi uendelee. Hiki ninachokizungumza ninavyo vielelezo; Mheshimiwa Waziri nimemwomba zaidi ya mara tatu hataki kusikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu, tulifanya semina akasema amezuia mitungi ya gesi na yenyewe ni uvuvi haramu. Kwenye uvuvi wa bahari, tulipozuia trolling tuliruhusu wavuvi waende zaidi ya mita 50 deep, deep sea ya mita 50 kwa pumzi ya kawaida lazima utumie mitungi ya gesi. Hii inatusaidia sana kwa sababu uvuvi pekee siyo majongoo bahari. Kama lengo ni ku-control majongoo bahari, tungeweka mfumo wa kuweka season fishing kwenye maeneo unasema kuanzia sehemu hii mpaka sehemu hii tutavua kwa miezi mitatu, kuanzia hapa tutavua kwa miezi mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapofanya burning totally wale wanaotumia mitungi hawaendi tu kwenye majongoo bahari, kuna uvuvi ambao ni selective ndani bahari. Hii mitungi watu wanaitumia kuzamia chini, maana yake ni nini sasa, tunajielekeza kwenye kufikiri kwa jambo moja tu kwamba wavuvi wote wa mitungi wanakwenda kwenye majongoo bahari. Pia kuzuia kabisa wala sio economically, sio kitu ambacho nafkiri ni sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza siungi mkono hoja kabisa, lakini namtaka Mheshimiwa Waziri kwa nia njema kabisa atakapokuja hapa aturidhishe na mateso makubwa wanayopata wavuvi wa Kanda ya Ziwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.