Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kabisa, napenda kuchukua fursa hii kuipongeza sana Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi katika kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha tunapata uvuvi endelevu na pia tunaliongezea Taifa fedha za kigeni kupitia Sekta hizi za Ufugaji na Uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Ufugaji na Uvuvi ni sekta muhimu sana kwa sababu ni sekta ambayo kwanza pia inatupa usalama wa chakula ndani ya nchi; lakini pili, inaongeza ajira; tatu, inaongeza pato la Taifa, lakini pia inatupa lishe bora. Ni vyema sasa Serikali ikaona kuna haja ya kuongeza msukumo zaidi katika sekta hizi ili kuongeza pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, katika Sekta ya ufugaji, wafugaji wanahitaji mipango bora ya malisho na maji, wanatakiwa wapewe elimu juu ya uvunaji wa maji ya mvua ili waweze kujenga mabwawa na malambo kwa ajili ya kulishia mifugo yao. Natumai wafugaji wakipewa elimu hii wataweza kuchukua baadhi ya mifugo na kuwekeza katika sekta hii ya upatikanaji wa maji na malisho; pia kunatakiwa wafugaji na wavuvi waendelee kupewa elimu ya juu ya uhifadhi wa mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, naelekea kwenye bidhaa za ngozi, kuna bidhaa nyingi za ngozi ambazo hazitumiki, na badala yake zinakaa zinapotea. Nawashauri Serikali, kwa vile viwanda ambavyo sasa hivi vinachakata ngozi, ile ngozi ya ziada ambayo haitumiki ni bora kukatengenezwa mazingira rahisi ili ngozi zile zikauzwa badala ya kubaki na kuwa hazifai au kuharibika au kuoza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Sekta ya Maziwa; sekta hii ina changamoto nyingi kwa wawekezaji wa viwanda vya maziwa. Changamoto pia inamkuta hata yule mzalishaji mdogo wa maziwa kwa sababu maziwa mengi yanaharibika njiani kutokana na miundombinu ambayo siyo rafiki kwa mkulima wa maziwa na tukizingatia kwamba bidhaa hi ya maziwa haichukui muda kuharibika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale wazalishaji wadogo wa maziwa wanapokwenda kupeleka maziwa kiwandani hawana vyombo vya kupooza maziwa hayo ili yachukue muda mrefu yawafikie viwandani na watumiaji wengine. Ni vyema sasa tukahamasisha, au Serikali ikatafuta mpango wa vipoozeo vya maziwa kuwapa hawa wakakopa kwa kupitia mabenki, kwa kupitia vikundi mbalimbali, waweze kupata vipoozeo vya maziwa ili maziwa yao yakae muda mrefu na yamfikie mtumiaji bila kuharibika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sheria za uvuvi, sheria hizi wavuvi wengi hawazifahamu, hizo sera hawazifahamu. Kwa hiyo ni vyema sasa wavuvi wetu wakaelekezwa juu ya sheria, sera na kanuni mbalimbali za uvuvi kwa sababu inaelekea kuna baadhi ya sheria zimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza ambazo wavuvi wetu hawazifahamu. Kwa hiyo, naipongeza Wizara kwa kutafsiri hii sheria kwa lugha ya Kiswahili ambayo itakuwa ni lugha nyepesi kwa wavuvi wetu kuweza kuifahamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kinachotakiwa baada ya tafsiri hiyo, zishushwe chini sasa kwa wavuvi wenyewe ili wazifahamu na wapewe mafunzo elekezi ya kufahamu sheria hizo na sera za uvuvi. Tukiwafundisha kanuni na sera za uvuvi kutapunguza huo uvuvi haramu tunaoupiga vita. Sisi sote tunajua kwamba uvuvi haramu ni janga la Taifa, linaharibu mazingira, linaharibu mazao yetu ya samaki na mazao mengine ya baharini. Sasa ni vyema wavuvi wetu wakapewa elimu zaidi ya kufahamu sheria, kanuni, vitu gani vinafaa kwa uvuvi na vitu gani havifai, nyavu ziwe na ukubwa gani, elimu hii iendelee kutolewa mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na hiki Kiwanda cha Sunflag ambacho kinazalisha nyavu inaelekea nyavu zake hazina ubora. Kwa sababu wavuvi wakitumia mara moja au mara mbili nyavu zimeshavurugika, zimeshakatika, hivyo tunamtia hasara mvuvi mdogo maskini ambaye amejichuma pesa zake ndogondogo akaweza kununua nyavu. Sasa tuangalie upatikanaji wa nyavu bora na vivulio bora vya samaki ili tusimuongezee mzigo mvuvi wetu mdogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inapotokea samaki, mvuvi amevua kwa bahati mbaya, kuna masikitiko na malalamiko, samaki ambaye hahitajiki kwa wakati ule, samaki ni samaki ndani ya bahari, unapopitisha nyavu anaweza akaingia na mwingine ambaye hahitajiki. Basi jambo lile lisichukuliwe kwamba yule mvuvi kafanya makusudi akalipishwa faini, akachomewa nyavu, akachomewa vyombo. Kwa hiyo hili suala linatakiwa lichukuliwe kwa umakini wake na kujua katika bahari kuna vitu vingi na vitu hivyo vinaweza vikajichomeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tatizo la mipaka ya leseni za uvuvi, wale wavuvi wanatakiwa waelezwe leseni zile wanazokata zinatumia mipaka gani. Kwa sababu bahari haina mipaka, imeanzia Zanzibar, Kilwa, Dar es Salaam, Kimbiji, inazunguka, na mvuvi anataka kutafuta samaki ili asipoteze muda wa kukaa kutwa kucha nzima baharini bila ya samaki, kwa hiyo hizi leseni zinazotoka hebu zitolewe kwa ufafanuzi ili wavuvi waelewe mipaka yao ya kuvua ni ipi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi, kwa sababu wakienda eneo lingine wanatozwa faini wanaambiwa wakate leseni nyingine. Sasa hizi leseni zimegawiwa kwa viwango gani, au akate leseni ya aina gani ili aweze kuvua sehemu yoyote ya Tanzania? Hili linatakiwa lifanyiwe kazi na wavuvi wetu waelezwe ili kuepusha hizo kasoro ndogondogo zinazojitokeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Wizara kwa kutengeneza huo mfumo wa kuzalisha samaki ambao sasa wavuvi wetu watajua wapi samaki wapo na watavua kwa wingi gani. Kwa hiyo, hili nalipongeza, ni jambo zuri na linatakiwa liwe endelevu kwa wavuvi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza pia Serikali na Wizara kwa kutaka kuifufua na kuiboresha TAFICO. TAFICO ikifufuliwa na ikiboreshwa ikawekewa miundombinu na mitaji, itaweza kufanya kazi za uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zana bora za uvuvi, zana bora za uvuvi kwa wavuvi wetu zinahitajika kwa sababu wataepuka kubahatisha kuvua. Kazi ya uvuvi ni ngumu na inahitaji uvumilivu wa hali ya juu. Wavuvi wanapokwenda baharini ukaona upepo unavuma huna uhakika kama mvuvi atarudi au harudi, atakuwa salama au hawi salama, atapotelea wapi. Tumeshuhudia Tanzania tunapokea wavuvi kutoka Comoro wengi tu ambao wamepotea baharini siku saba, siku nane na Watanzania wanapotea kuelekea nchi nyingine. Kwa hiyo, hii kazi ni ngumu, siyo kazi rahisi, inataka ujasiri. Kwa hiyo, ni vyema wavuvi wetu sasa tukawaendeleza ili wapate zana bora za uvuvi za kujua wapi samaki wapo, kwa ukubwa gani, kwa wingi gani, kwa kina gani cha maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nichangie kuhusu uvuvi wa Bahari Kuu, naomba Serikali imalize hii michakato ya ujenzi wa bandari za uvuvi na ununuzi wa meli ya uvuvi. Kwenye uvuvi wa bahari kuu hakuna haja ya kuwekeza, Mwenyezi Mungu ameshawalea mwenyewe samaki, ameshawakuza sasa hivi kazi yetu sisi wanadamu ni kwenda kuwavua. Kwenye uvuvi wa bahari kuu kuna samaki wengi ambao nchi za duniani wanafaidika na uvuvi huu. Tutaweza kuongeza Pato letu la Taifa na tutaweza kutengeneza miundombinu mingi kupitia uvuvi wa bahari kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nikiendelea kwenye uvuvi huu wa bahari kuu, kuna mgao wa fedha, mgao huu unahusu Serikali mbili. Naomba usicheleweshwe, ugawiwe kwa maeneo yote Bara na Zanzibar, ili Sekta ya Uvuvi iweze kusonga mbele badala ya kubakia tu hazipelekwi. Kwa sababu kuna miundombinu mingi ya kupanua Sekta ya Uvuvi bado hatujafikia na tunahitaji mapato ya kutosha ili tuwekeze kwenye Sekta hii ya Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Wizara, lakini pia nakipongeza Chuo kile cha Uvuvi cha Kigoma. Bila kutumia senti hata moja ya Serikali wameweza kufufua chuo kile kwa fedha zao wenyewe, wamejibinya, wameweza kufufua kile chuo na kuongeza wanafunzi wa kusomea mambo ya uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.