Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Halima Abdallah Bulembo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwa majina naitwa Halima Abdallah Bulembo, ni Mbunge wa Viti Maalum kundi la vijana au Mbunge mdogo kuliko wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba kumpongeza Mheshimiwa Rais, katika kipindi alipokuwa akitafuta kura aliahidi kutowaangusha vijana na ukiangalia Baraza lake Mawaziri wengi ni vijana, ukimuangalia kaka yangu Wakili msomi Mavunde ni kijana, kuna Injinia Masauni ni kijana, kuna Dkt. Kigwangalla na kuna Dkt. Possi, tunamuahidi na sisi vijana hatutomuangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, naomba pia kusema kidogo. Nina masikitiko katika suala zima linaloendelea Bungeni, Wabunge wenzetu wa Upinzani kuwa wanatoka. Ningeshauri kale kautaratibu ka posho tungekuwa tunasaini saa 12 jioni tuone pia kama wangekuwa wakitoka? (Makofi).
Baada ya hayo machache, naomba kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa hotuba yake nzuri, ni hotuba yenye kufufua matumaini, ni hotuba yenye kujali wananchi hasa wanyonge, ni hotuba yenye kujali na kuleta nuru na matarajio mapya kwa wananchi na kiukweli Tanzania mpya inaonekana chini ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mimi ni kijana, nitaanza na tatizo sugu la vijana ambalo ni ajira na kaka yangu Mheshimiwa Mavunde naoma unisikilize. Katika hotuba ya Rais, alizungumzia tatizo la ajira kwa vijana. Wote tunafahamu kwamba ajira ni tatizo sugu si kwa Tanzania tu lakini ni kwa dunia nzima. Tatizo hili linahitaji msukumo zaidi wa Kiserikali, Taasisi mbalimbali lakini vilevile linahitaji sisi wenyewe Wabunge tukipata fursa za ajira tuzipeleke kwa vijana, tusisubirie Serikali tu, tukiendelea kusubiria Serikali ifanye kila kitu tutaishia kubaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika suala zima la ajira naomba kuwaambia Watanzania kwamba vijana wengi wanajiajiri na vijana ambao wanakuwa na uwezo wa kujiajiri ni kuanzia umri wa miaka 18 mpaka 35 ambayo ni asilimia 32 ya Watanzania, kwa hiyo vijana ni kundi kubwa. Safari hii kuna utaratibu vijana wengi wamekuwa wakienda Jeshini, ushauri wangu kwa Serikali, nilikuwa naomba katika kila Kambi ya JKT, kuwe na Chuo au Vyuo vya VETA, vijana wanapotoka hapo wapewe mikopo na nyenzo za kazi. Kwa hivi tunaweza tukasaidia kwa namna moja ama nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo naomba kuzungumzia suala la mikopo, niko na vijana bado. Masharti ya mikopo yamekuwa makubwa! Kijana leo anamaliza Chuo Kikuu anataka kujiajiri, anaambiwa ukitaka mkopo leta kiwanja, leta nyumba! Jamani, ndiyo nimemaliza chuo, nyumba naipata wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningeomba Serikali iongee na taasisi za fedha zilegeze masharti kwa vijana wanaokuwa wamemaliza Chuo, ili waweze kujiajiri. Tunaona nchi inaendeshwa kwa watu wengi ambao wamejiajiri, tuwasaidie vijana wafike kule wanakotaka kufika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ninalotaka kuzungumzia ni suala la ushuru. Mheshimiwa Rais aliahidi na aliongea kwa msisitizo mkubwa kwamba, atapunguza na kuondoa ushuru kwa wafanyabiashara wadogo wadogo. Alisema pia, ataondoa harassment zinazofanyika na mgambo wa Manispaa na Majiji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachofanyika wote tunakijua, wafanyabiashara wadogo bado wananyanyasika, inatia uchungu. Unamkuta mama lishe kajipangia pale anauza chakula, mgambo anakuja anamwambia kama hutaki nikufukuze nipe 1,000/=! Tangu asubuhi hiyo 1,000/= ndiyo anayoitafuta! Kwa hiyo, kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene watu wako hawa uongee nao vizuri, bado wanaendelea kunyanyasa watu wetu na tukumbuke katika nchi yoyote kuna wafanyabiashara wakubwa kama akina Bakhresa, kuna wafanyabiashara wa kati kama akina Shabiby, lakini kuna wafanyabiashara wadogo wadogo! Sasa kwa nini wale wakubwa hawaonewi mnawaonea wadogo, si haki! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alisema kabla ya kuwafukuza wale au kuwaondoa, mwambie mama hapa hustahili kukaa, lakini eneo lako husika ni hili. Unamwambia hapa hufai kukaa, eneo la kukaa halifahamiki, hujampangia! Ni wakati wa Halmashauri za Manispaa na Wilaya ziitikie kwa vitendo hotuba ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila Halmshauri ioneshe ni wapi imetenga maeneo kwa hawa watu. Wafanyabiashara wanaishi kwa mashaka, hawana matumaini, wanatapakaa mitaani! Kwa kufanya hivyo tunazidi kumtia aibu Mheshimiwa Rais kuonekana alichokuwa anakizungumza na kuwaahidi wafanyabiashara wadogo wadogo si sahihi. Kwa hiyo, mimi naomba sana Serikali itie mkazo katika masuala haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho kabisa nataka nimalizie na suala zima la elimu. Naomba kumpongeza Mheshimiwa Rais kwamba ameweza kulitimiza kwa asilimia kubwa, elimu imekuwa bure kuanzia elimu ya msingi mpaka kidato cha nne.
Lakini pia nataka kuzungumzia kuhusu vijana wanaomaliza Chuo Kikuu kwamba kunakuwa na fursa vijana wengi huomba kwenda kusoma nje ya nchi. Lakini fursa hizi kwa uzoefu na kwa utafiti wangu Tanzania ya leo ina Vyuo Vikuu vingi, lakini vijana wengi wanaomaliza Chuo Kikuu huomba zile fursa za kutaka kusoma nje, lakini ambao hupata fursa siku zote wanachukuliwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mzumbe! Kwa maana bado sitaki kuamini kama ile dhana ambayo ilikuwa inasema mtu akisoma Mzumbe na UDSM ndiyo anakuwa hatari kabisa. Siku hizi kuna wanafunzi ambao wana uwezo mkubwa wapo UDOM, wapo Tumaini, wapo katika kila chuo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba vigezo mnavyovitumia kuwachukua hawa vijana kuwapa nafasi za kusoma nje ya nchi, zifike katika kila chuo, zisiende UDSM na Mzumbe peke yake, tuwape vijana wote haki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema machache hayo naomba kushukuru sana, ahsante. (Makofi)