Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

Hon. Susanne Peter Maselle

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

MHE. SUSANNE P. MASELLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitekeleza au kukiboresha kilimo unagusa maisha ya mwananchi wa kawaida kabisa. Takwimu zinaonesha kuwa kilimo kinaajiri kati ya 70% hadi 75% ya Watanzania na kinachangia 20% hadi 28% ya pato la Taifa. Kwa nini sekta inayoajiri watu zaidi ya nusu ya ajira na inayochangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa inapuuzwa na kupangiwa bajeti ndogo ukilinganisha na umuhimu wake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ije hapa ituambie kwa nini haitekelezi Azimio la Maputo kuhusu kilimo na usalama wa chakula ambapo ilitakiwa kutenga 10% ya bajeti ya Serikali kila mwaka kwa ajili ya kilimo. Pesa hii ingesaidia sana katika kutatua changamoto nyingi ambazo zinaikumba sekta hii ya kilimo na kukuza uchumi wa wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa pamba wanazidi kukata tamaa kwa sababu pamoja na kazi kubwa wanayofanya wanaishia kupata hasara tu kuanzia maandalizi ya kilimo, kwenye mavuno na hadi kwenye mauzo. Wanakabiliwa na matatizo ya mbegu ambazo hazioti na wameuziwa na mawakala waliopitishwa na Bodi ya Pamba. Hivyo, inawalazimu kununua mbegu mara mbili na kuwafanya wapishane na misimu. Mbali na mbegu mbovu, wanakumbana na dawa ambazo haziui wadudu, wanunuzi wadanganyifu wanaochezea mizani ili kupata faida kubwa, pembejeo kuchelewa kufika na kupishana na msimu wa kilimo na kilimo cha kutegemea msimu huku kukiwa na mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa pamba wa Mwanza na maeneo mengine takribani mikoa 17 inayolima zao hili wanateseka sana na kuona zao hili kama halina faida kwao. Ni wakati sasa wa Serikali kutatua changamoto hizi ili wakulima hawa wafaidike na hili zao lao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iwafutie madeni wakulima wanaodaiwa kwa muda mrefu yanayohusu pembejeo na huduma za ugani hasa mbolea, viuatilifu na mbegu. Madeni haya ambayo yanaongezeka kila mwaka yanawafanya wanalima huku wakiwa na mzigo wa kulipa madeni kila mwaka, matokeo yake hawapati kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iwapatie ruzuku wakulima kama mataifa makubwa duniani wanavyowapatia ruzuku wakulima wake. Kwa nini hapa tunaacha wakulima kuwa ni watu wa kuhangaika wenyewe? Tuanze na wakulima wa pamba, tuwasamehe madeni yao na wapewe ruzuku ili sasa turudishe hadhi ya maisha ya wakulima wa pamba ambao walitufanya tukasifika duniani na watu kuendesha maisha vizuri kabisa ikiwemo kujenga makazi bora na kusomesha watoto wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha umwagiliaji kipindi hiki ni muhimu sana kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanasumbua sana kutabiri misimu ya masika, vuli, kipupwe au ukame. Ni nini mikakati ya Serikali kibajeti hasa kwa maeneo ambayo wananchi wameshaonesha utayari kwa vyanzo au uwezo kidogo walionao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha umwagiliaji kinaweza kabisa kuliokoa Taifa na mahitaji ya chakula, kuongeza pato la Taifa na kuboresha maisha ya wananchi. Nini mikakati ya Serikali hasa kulitumia Ziwa Victoria kama wafanyavyo wenzetu wa Misri ambao kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia Mto Nile kutokana na Ziwa Victoria ndio uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa hilo? Ni hatua gani Serikali inachukua pamoja na ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi katika kuwekeza katika shughuli za kilimo, uzalishaji na usindikaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwanza ina rasilimali kubwa sana ya maji huku 53.25% ya eneo la mkoa likiwa katika Ziwa Victoria. Ni kwa mantiki hiyo kilimo cha umwagiliaji kinaweza kufanywa kutegemea maji ya ziwa hilo, pamoja na mabonde ya mito yanayopeleka maji katika ziwa hilo. Eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji katika Mkoa wa Mwanza ni takribani hekta 39,411 lakini mpaka sasa ni hekta 1,429 (sawa na 3.93%) ndizo zinazotumika kwa kilimo cha umwagiliaji. Serikali iweke mikakati madhubuti kuongeza idadi za hekta ili wananchi wanufaike na hiki kilimo cha umwagiliaji.