Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

Hon. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika hotuba ya Waziri wa Kilimo. Watanzania wote tunakubaliana kwamba zaidi ya asilimia 60 ya wananchi hupata ajira zao kupitia sekta ya kilimo. Pia tunakubaliana kwamba sekta hii hutoa chakula chote cha wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha ni kwamba kilimo hapa nchini kinachukuliwa kama cha kujikimu tu na wala hakuna mpango mkakati wa kuonesha kwamba kilimo chetu kimejiandaa kufanya biashara ya kuhakikisha tunauza mazao kwa wingi nchi za nje ili kuongeza fedha za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kilimo chetu kinategemea mvua kwa kiasi kikubwa. Katika ukurasa wa saba wa hotuba ya Waziri ameonesha kuwa mwaka 2016/2017 uzalishaji ulipungua kutokana na uhaba wa mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna dhamira ya kufanya kilimo cha umwagiliaji, Wizara itafanikiwaje kama Idara ya Umwagiliaji bado iko chini ya Wizara ya Maji? Nashauri Waziri alete pendekezo Bungeni kusema kwamba Idara ya Umwagiliaji ihamishiwe Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Same Mashariki lina mito mingi na ardhi zaidi ya hekta 300,000 ambazo zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji. Nimeomba Wizara ya Maji tusaidiwe miundombinu ya umwagiliaji. Ni mwaka wa tatu huu maji ya mito yote yanaenda baharini na Wizara haikujali hata kujibu kama wana mpango gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Kilimo amesema kuwa mazao ya kilimo huchangia asilimia 65 ya malighafi yanayohitajika viwandani. Je, kumekuwa na mkakati gani kati ya Wizara hizi mbili kuona jinsi zitakavyoshirikiana ili kuhakikisha ni viwanda gani vitawekwa mikoa gani ili kuwe na hakika ya uzalishaji wa mazao hayo kutosheleza mahitaji ya kiwanda tarajiwa? Kwa mfano, Wilaya ya Same imechagua zao la tangawizi kuwa ndilo litatumiwa kuanzisha kiwanda kikubwa cha kuchakata tangawizi. Pia kuna tarajio la kutoa tangawizi nyingi ili kiwanda kiweze kuzalisha kwa soko la nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la wazi ni kwamba tangawizi inahitaji maji mengi sana. Tatizo ni kwamba hakuna miundombinu ya umwagiliaji ya kutosheleza kupanua kilimo hicho. Wakati LAPF wanawekeza kujenga kiwanda kikubwa na kuweka mashine za kisasa, je, malighafi za kutosha zitapatikanaje wakati hakuna miundombinu ya umwagiliaji? Naomba Waziri wa Kilimo aeleze kwamba kilimo kitakuwaje bila umwagiliaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la Maafisa Ugani kwamba huko vijijini na kwenye kata hawasaidii wakulima. Waziri akihitimisha hotuba yake aeleze jinsi Wizara yake itakavyoweza kufanya kazi na TAMISEMI ili kuwaondoa Maafisa Ugani ambao hawana tija na kisha kuajiri na kusimamia utendaji kazi wa hawa Maafisa Ugani kwenye vijiji, kata na kwenye wilaya. Ahsante.