Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na mkakati wa zao la michikichi Mkoa wa Kigoma. Mwezi Februari, 2017 Serikali ya Mkoa wa Kigoma kupitia kikao cha RCC ilipitisha mpango wa kuendeleza zao la michikichi. Mpango huu ulikuwa na shabaha ya kuongeza uzalishaji wa mafuta ya mawese nchini mpaka tani 400,000 kw mwaka kwa kulima hekta 100,000 za michikichi katika Wilaya tatu za Mkoa wa Kigoma. Mpango huu ungewezesha kufunguliwa kwa viwanda vya kati nane vya kusindika mawese na mazao ya mawese na mazao na kutengeneza ajira 6,400. Mpango huu ungewezesha familia 100,000 kulima michikichi kwa kila familia hekta moja(ekari 2.5) na kuongeza kipato cha familia kwa jumla ya shilingi za Kitanzania 13,000,000 kwa mwaka na hivyo kuwaondolea kwenye umaskini watu 600,000 na kuwafikisha kwenye kipato cha kati ndani ya miaka mitatu tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu pia ungewezesha Tanzania kutoagiza tena mafuta ghafi kutoka Malaysia na Indonesia na kuokoa shilingi dola milioni 294 (shilingi bilioni 646) ambazo Tanzania hutumia kila mwaka kuagiza mafuta hayo. Ukijumlisha uzalishaji wa alizeti na mawese nchini, mpango huu ungewezesha Tanzania kujitoshereza kwa mafuta ya kula na ziada nje ili kupata fedha za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa mpango huu unahitaji dola milioni 45 tu na Benki ya Maendeleo ya Afrika ina facility hiyo ya uzalishaji wa mafuta ghafi ambapo Mkoa wa Kigoma uliomba Serikali iombe huko ili kupata mbegu, kutoa mafunzo ya ugani na kuandaa sheria ndogo za Mahakama za Serikali za Mitaa kuwezesha mkakati hu kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo haijachukua hatua yoyote katika kusaidia Mkoa wa Kigoma kutekeleza Mpango huu, hata barua kutoka Ofisi ya Rais, Mkoa wa Kigoma haijajibiwa na Wizara na Waziri wa Kilimo na Chakula hajakanyaga Mkoa wa Kigoma tangu aanze kazi licha ya kuwa ndiyo Mkoa pekee nchini haujawahi kupewa msaada wa chakula tangu dunia iumbwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naisihi Serikali iusaidie Mkoa wa Kigoma kutekeleza mkakati wa michikichi kupitia mpango wa kuendeleza zao la mchikichi ili nchi ipone kutoka kwenye kuagiza mawese na mafuta ya kuzalisha sabuni ambayo ni by product ya michikichi kupitia mafuta ya mise.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri Wizara za Fedha, Kilimo na Viwanda zikae na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ili kuweka mkakati wa utekelezaji wa mpango huu ili ifikapo mwaka 2022 Tanzania iwe muuzaji (net exporter) wa mafuta ya kula badala ya kuwa muagizaji (net importer). Ahsante sana.