Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

Hon. Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, lakini pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kuniwezesha kusimama mahali hapa ili tuweze kuishauri Serikali ya Chama cha Mapinduzi ili baadae iweze kufanya kazi vizuri na maendeleo yawafikie Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache sana, mimi nilikuwa na mapendekezo matatu tu ambayo nataka kuikabidhi Serikali ya Chama cha Mapinduzi ili wayafanyie kazi.

La kwanza, napendekeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi iangalie uwezekano wa kuiunganisha Wizara ya Kilimo na Wizara ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo la pili, nataka Serikali ikubali sasa ili tuelekee kwenye mapinduzi makubwa ya kilimo na kuijenga Tanzania ya viwanda basi tukubaliane kupiga marufuku uagizaji wa vyakula na malighafi zingine ambazo zinaweza kuzalishwa hapahapa nchini. (Makofi)

Pendekezo la tatu, ni kupendekeza Chama cha Mapinduzi ambao ndiyo marketing manager wa sera zinazotekelezwa na Serikali wabadilishe logo yao, wabadilishe nembo ya jembe na nyundo ambayo haihamasishi mapinduzi ya kilimo hapa nchini. Naomba niyajadili haya bila kufuata mpangilio wa namba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali ya Chama cha Mapinduzi ilipoanza kusema wanataka kuitengeneza Tanzania ya viwanda, hatukuwa tunategemea kwamba tujenge viwanda ambavyo havitatumia malighafi zinazotoka shambani. Tuliamini kwamba Tanzania ya viwanda ni viwanda vile ambavyo vitatumia malighafi zinazozalishwa mashambani ili ziweze kuzalisha bidhaa ziweze kupandisha thamani mazao yetu na Mtanzania huyu ambaye anaitwa mnyonge ambaye kimsingi ametiwa unyonge na Serikali ya Chama cha Mapinduzi aweze kubadilisha maisha yake yale bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tukasema ili haya yafanye kazi vizuri, ni lazima Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ziwe zinafanya kazi kwa pamoja. Kitendo cha kutengana kwa Wizara hizi ndiyo unakuta anakuja Waziri wa Viwanda anakusomea hapa kwamba wamejenga viwanda vingi, lakini ni viwanda vya kutengeneza kandambili, viwanda vya kutengeneza mabeseni, viwanda vya kutengeneza mabanio ya nywele, viwanda vya maji, vitu ambavyo havitusaidii kuboresha mazao yanayotoka shambani. Kama wangekuwa wanafanya kazi kwa pamoja maana yake kwenye mafanikio ya Wizara ya Viwanda angekuja angesema kwamba tulikuwa tunazalisha mafuta ya kula asilimia 30 tu ndani sasa tumepandisha tunazalisha mafuta ya kula kwa asilimia 45.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungekuwa tunaona pia kwenye viwanda kwamba zao la chikichi limetengewa fedha kubwa ili uzalishaji wa malighafi za kutengeneza mafuta zipatikane ndani. Tusingekuwa tunaona kwenye kilimo wakulima wa ufuta wanalalamika kwamba hawana soko la uhakika, tusingekuwa tunalalamika kwamba eti kuna mafuta ghafi yamekwama bandarini yanataka kuingizwa huku ndani tunaanza kupiga kelele hapa inaharibu muda wetu wa kufanya mambo mengine kama malighafi hizo zingekuwa zinazalishwa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna nchi imepiga hatua kwenye mapinduzi ya viwanda bila kupitia kipindi kigumu. Ukienda India watakuambia tulisimamisha kuagiza magari kutoka nje kwa sababu tulitaka tuzalishe ya ndani kwanza ili soko letu la ndani lote litumie magari ya ndani.

Ukienda China hivyo hivyo, sisi hapa bado tunaagiza sukari, mafuta, soya, mihogo mikavu kutoka nje, tunashindwa nini kulima hapa? Tupige marufuku uagizaji wa mazao haya kutoka nje, hata kama tunazalisha mafuta kwa asilimia 30 tuitumie hiyo hiyo, tutaona namna gani kumbe tunaweza tukaongeza, tunaweza tukatengeneza fursa kuzalisha hapa nchini. Hatuwezi kufa kwa kukosa mafuta ya kula, hatuwezi kufa kwa kukosa sukari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii sukari siyo kwamba tunashindwa kulima hapa ndani, ni ukiritimba tu wa kulinda viwanda vikubwa. Ukienda kule Kilombero kila mwaka miwa inalala shambani mnunuzi hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mkulima wa miwa kule Kilombero, tunalima miwa hatuwezi kupanga bei sisi anapanga bei anayekuja kununua. Yeye ndiye anapanga bei ya namna gani atautoa huo muwa wako kutoka shambani kuupeleka kiwandani kwake na namna ya kulipa pia anachangua yeye kwamba nakulipa kwanza asilimia kumi, hii asilimia kumi nyingine nitakulipa mwezi unaofuata yaani mkulima unakuwa kama unasaidiwa wakati unauza mazao yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yupo mfanyabiashara mmoja alijaribu kujenga kiwanda kidogo cha kutengeneza Sukari pale Sanje akapigwa vita mpaka akafunga kiwanda. Kwa hiyo, kuna mikakati ya makusudi kuhakikisha hakuna viwanda vidogo vidogo vya kutengeneza sukari vinajengwa ili wale ma-giant wakubwa ndiyo waendelee kuzalisha sukari hiyo kidogo ili mwisho wa siku Serikali itoe vibali vya kuagiza sukari kutoka nje wapewe wao ndiyo waingize wapate faida kubwa, hatuwezi kuitengeneza Tanzania ya namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni nembo ya Chama cha Mapinduzi, tunasema tunataka kwenda kwenye mapinduzi makubwa ya kilimo lakini wewe Mheshimiwa Waziri unasimama kunadi kwamba tunataka tuachane na jembe la mkono huku umezungukwa na watu waliovaa t-shirt ambazo zimebeba jembe la mkono na nyundo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ni brand, namna ambavyo umeiweka brand yako ndiyo itasaidia kukutangaza kwamba wewe una malengo ya kuelekea wapi. Huwezi kubeba brand ya jembe na nyundo halafu utake ikupeleke kwenye kilimo cha kutumia matrekta. Hebu mkae, mnaweza kulichukua hili kama jambo la kisiasa, lakini hii siyo siasa, ndiyo ukweli, kilimo ni biashara. Watu wanataka kulima, wanataka wabadilike kutoka kwenye jembe la mkono watumie kilimo cha kisasa, unawapelekaje kwa kuvaa jembe la mkono?

Anzeni kubadilisha mindset zenu ndiyo mtaweza kulisimamia jambo ambalo mnataka kulitekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yawezekana mmeamini kwamba kila mambo mnayoyasema huwa hayatekelezeni, lakini I assure you, Tanzania ya viwanda inawezekana. Mpaka leo bado unapita hapo Dumila unakuta nyanya zinaoza, ni kwa sababu wenyewe hamuamini kwenye jambo ambalo mnalisimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa anzeni kwanza kubadilisha mitazamo yenu kama Serikali muamini kwamba tunataka tujenge Tanzania ya viwanda lakini kwa kutumia malighafi zinazolimwa shambani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana watu wanapiga kelele leo, amesema hapa Mheshimiwa Qambalo kuwa Mheshimiwa Waziri ambaye uko ndani ya Serikali huna tofauti na mimi Waziri Kivuli, wote tunaongea maneno matupu ambayo hayaendi kwenye utekelezaji. Kama huna bajeti, bajeti inashuka kila siku, utatekeleza vipi hiyo mipango yako? Wanatushinda Rwanda, wametenga bajeti ya shilingi trilioni saba kwa ajili ya kilimo, nchi ndogo kama ile, sisi tunatenga shilingi bilioni 170, hiyo si nauli tu ya Waziri kutembelea mikoani, itatusaidia kitu gani? Bado Waziri unataka kudanganya watu hapa kwamba eti NFRA itanunua mazao yote ambayo yamesalia huko mikoani, hii haiwezekani.