Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika bajeti iliyopo mbele ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja Mheshimiwa Rais aliwahi kusema kwamba anadhani kuna baadhi ya Mawaziri hawamuelewi, lakini mimi nataka niseme kwamba inawezekana Mheshimiwa Tizeba na Mheshimiwa Mwijage ni miongoni mwa Mawaziri ambao hawamuelewi Mheshimiwa Rais anataka nini. Hili nalizungumza katika Tanzania ya viwanda pamoja na mapinduzi ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitajikita katika zao la mkonge. Jana sindano zilikuwa za pamba leo zihamie kidogo kwenye upande wa mkonge. Mkoa wa Tanga peke yake una mashamba 27 ya mkonge, nchi nzima ya Tanzania inayo mashamba 53, mashamba 14 yapo katika Mikoa ya Pwani, Morogoro, Kilimanjaro na shamba moja liko Mkoa wa Arusha. Lakini mashamba haya mengi yametelekezwa na mpaka sasa ninavyozungumza hapa hata mkonge wa kusafirisha korosho na mazao mbalimbali tunaagiza duty kutoka nje ya nchi. Kwa hiyo, hapa utaona moja kwa moja kwamba kama tunakusudia kuwa na Tanzania ya viwanda bila kubainisha tunakusudia kuwa na viwanda vya namna gani, itakuwa hii ni hadithi ambayo itakwenda kukumbana na kifo muda si mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nchi hii ilipopata uhuru Mwalimu Nyerere alianzisha maeneo mbalimbali na mazao mbalimbali ya kimkakati ya kukuza viwanda vya ndani, miongoni mwa viwanda hivyo vilikuwa ni viwanda ambavyo vinachakata mazao ya mkonge ikiwemo TANCORD, ambayo wakati huo iko Tanga, kuna Amboni Spinning, kuna Ubena Spinning iko Morogoro na TPM ambacho kiko Morogoro na mpaka sasa hivi ndichoo kiwanda pekee ambacho kinazalisha magunia ya mkonge. Kiwanda kingine kiko Moshi, Kiwanda cha Magunia cha Moshi. Sasa utaona kwamba sasa hivi mkonge unaozalishwa nchini kwa mujibu wa takwimu za Wizara ni tani 26,495 na mwaka huu wanataraji kwamba tutazalisha mpaka tani 43,127, lakini viwanda hivi havipati malighafi za kutosha kwa singa nyingi zinasafirishwa kwenda nje kama malighafi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo viwanda vya ndani vinakosa material na miongoni mwa viwanda vinavyokosa ni pamoja hii TPM ya Morogoro, hawa wana uwezo wa kuzalisha magunia mpaka milioni 10 kwa mwaka, lakini sasa hivi uwezo wao ni kuzalisha maguni milioni moja peke yake, na soko la ndani peke yake lina uwezo wa kupata magunia milioni tatu ambayo tunaweza tukasafirisha mazao mbalimbali ikiwemo korosho. Hapa tatizo lipo wazi kwamba tatizo ni kwamba ni kwenye kodi, viwanda hivi vinavyozalisha ndani vina kodi mbalimbali corporate tax, kuna VAT na kadhalika. Wanaoagiza duty kutoka nje hawalipi kodi kwa sababu hivi ni vifungashio ambavyo tumeridhia katika Common Market Protocol kwamba vifungashio vinavyokuja kufungasha mazao havitozwi kodi, matokeo yake ni kwamba tunakosa kodi kwa viwanda vya ndani kushindwa ku-supply bidhaa zao kupitia malighafi ambazo zinatoka na mazao ya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana uliangalie hili kwa jicho la karibu sana kwamba ili kujenga uwezo wa viwanda vya ndani na kuelekea Tanzania ya viwanda ni lazima viwanda vinavyochakata mazao ya mkonge viweze kusimamiwa ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili nizungumzie suala la kilimo cha kahawa. Kahawa ilikuwa ni zao ambalo kule Kilimanjaro ni zao la wanaume, lakini sasa hivi wanaume wa Kilimanjaro wanashindana na wanawake kwenye ndizi, Baba Paroko pale ni shahidi kwamba hata wanawake wanaenda kutafuta purchasing power nje ya nchi kwa sababu wanaume wa Kilimanjaro pesa hazipo! Ni kwa sababu ya kilimo cha kahawa kimekufa na hapa tunahitaji tufanye utafiti, mabadiliko ya tabianchi sasa hivi yameikumba nchi yetu maeneo mengi kahawa haizalishwi tena. Kule Lushoto tulikuwa tunazalisha kahawa tani 300 mpaka tani 500 kwa mwaka, sasa imeshuka mpaka tani 150. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hesabu ziko sawa tu kwamba tulikuwa na shamba Kwehangala ambayo iko Jimbo la Bumbuli heka 450 sasa hivi shamba lile limekuwa ni viwanja vya kawaida tu watu wamerasimishiwa. Kwesimu heka 350 yote haya yalikuwa ni mashamba ya Usambara Coffee Growers sasa hivi hayatumiki tena kama mashamba ya kuzalisha kahawa. Kata sita Jimbo la Mlalo zinalima kahawa, Kata 14 Jimbo la Bumbuli zilikuwa zinalima kahawa, Kata nne Jimbo la Lushoto zilikuwa zinalima kahawa. Karibu Kata 25 ambazo zilikuwa zinalima kahawa sasa hivi hazilimi kahawa pia imeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi. Kwa hiyo tunawaomba sana TaCRI wafanye utafiti ili kuweza kuboresha zao hili liweze kurudi katika kama ilivyokuwa zamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo Lushoto peke yake hata maeneo mengine ya Tarime walikuwa wanalima kahawa, Mbozi walikuwa wanalima kahawa, Ileje - Mbeya kule walikuwa wanalima kahawa sasa hivi uzalishaji wa kahawa umeshuka sana ni lazima mazao haya yaweze kurejeshwa kama ilivyokuwa zamani na yatarejeshwaje? Ukurasa wa 69 hapa tumeona kwamba Wizara inazungumzia kwamba TaCRI watakuwa moja kwa moja wanawajibika kwenye Wizara na miongoni mwa majukumu yao itakuwa ni kufanya utafiti pia kugawa mbegu na kutoa elimu kupitia Maafisa Ugani, sasa hili la Maafisa Ugani ndiyo ambalo mimi ningeshauri muanze nalo. Maafisa ugani walioko huko hawaelewi kabisa hata huko Usambara kulikuwa kuna kahawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TaCRI pia wafanye utafiti kutokana na mabadiliko ya tabianchi ni aina gani ya mbegu ambayo inaweza ikawa bora kwa hali ya hewa iliyopo sasa. Sambamba na hilo ni lazima sasa AMCOS za kahawa pia ziboreshwe. Vile vyama vyetu vya Ushirika vya zamani, Usambara Cooperative, TARECU na kadhalika vimekufa, kwa hiyo tunahitaji sasa kutoa elimu mpya ya ushirika kwa wakulima hawa wa kahawa kwa kule Usambara ili kuongeza tija lakini kuongeza uzalishaji na sisi tuweze kushiriki katika uchumi huu wa Tanzania ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika kwamba Waziri mwenye dhamana bado sijaona kama ana jitihada maksudi za kufufua zao la kahawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na semina mbalimbali zinazoendelea lakini tunahitaji sasa hizi semina ziweondoke maofisini, zihamie kwenye maeneo kahawa inakozalishwa. Kumekuwa na miaka miwili ya kuendesha semina maofisini, sasa naomba uanze kwenda site, acha kuvaa suti ni wakati wa kuvaa gumboot na kuingia site kuhakikisha kwamba wakulima huko wanazalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni tozo kwenye nguo ambazo zinaingizwa nchini ili kunusuru viwanda vyetu vya nguo. Viwanda vya nguo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)