Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi tena niweze kuchangia kwenye hii Wizara. Hii ni Wizara nyeti sana kwa sababu asilimia 85 ya wakazi wa Jimbo langu na Tanzania nzima ni wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muda huu, naomba tu niende moja kwa moja kwenye mambo machache ambayo napenda Wizara ya Kilimo ikayarekebishe ili watakapokuja hapa waweze kutupatia majibu. Kwanza kabisa, nataka niwakumbushe kwamba pamoja na nia njema kabisa ya Serikali ya kutaka wakulima wa korosho walipwe kupitia kwenye bank account lakini zoezi hili limekuwa na usumbufu mkubwa. Kwa hiyo, tunaomba upande wa Serikali waangalie namna bora ya kufanya kuwasaidia hawa wakulima. Wamekuwa wakikesha kwenye benki ukifika pale Masasi, Ndanda kwa kweli imekuwa kero mpaka watu wanajuta kwa nini walikuwa wanalima korosho ili pesa zao wakapatie kule benki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna hujuma nyingine inafanyika kwenye zao la korosho ambayo ni ucheleweshwaji mkubwa wa malipo ya wakulima. Tulipokutana hapa na hata tulipokaa kikao cha wadau wa korosho, tulisema kwamba ndani ya siku saba mnunuzi atakuwa amelipwa malipo yake na ndani ya siku hizo hizo saba tunategemea mpaka mkulima naye atakuwa amepata pesa zake. Kwa hiyo, tunaomba hili nalo likaboreshwe Mheshimiwa Waziri akija hapa aje na majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu nikufahamishe kwamba kuna hujuma kubwa sana zinafanyika ndani ya zao la korosho zaidi kwenye ugawaji wa viatilifu. Serikali imepanga na wanasema wataboresha uzalishaji wa zao la korosho. Ni kweli dalili zinaonesha hali nzuri kabisa na kwamba Serikali ina nia njema lakini wasimamizi wa jambo hili hawana nia njema ndiyo ambao wanamwangusha Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015/2016, korosho zilivunwa tani 155 na hela nyingi tu zilipatikana, tukaendelea kuboresha zao hili. Mwaka 2016/2017, zilivunwa tani 265,000 lakini baadaye 2017/2018 tunaratajia kwenda kupata tani 311,000. Sasa ili tupate tani hizo lazima kuwe na mipango mizuri kutoka hatua za awali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo mimi limekuwa likinishangaza kila mara. Nilipoanza tu kwa mara ya kwanza kuchangia hapa Bungeni nilitoa taarifa za kampuni moja, mimi naendelea kuiita ya kitapeli mpaka pale nitakapojithibitishia, inaitwa Hammers iko Mkoa wa Mtwara ndiyo ambayo kila mwaka imepata tenda za usambazaji wa viuatilifu vya zao la korosho. Mwaka jana walishindwa ku-deliver tani 700 katika tani 3,000 walizopewa order, na ukienda kwenye ripoti ya CAG anaeleza sababu za msingi kwamba hii kampuni haina uwezo na nina taarifa kwamba hata sasa hivi imepewa kazi ya kusambaza. Wenye kampuni hii wanafahamika, wanafanya hujuma kubwa sana kwenye zao la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wengi wanashikiliwa kwenye vituo vya polisi kwa kuambiwa wanahujumu uchumi. Huu uhujumu uchumi wa waziwazi tunaowaonesha hapa sasa hivi mkaufanyie kazi. Kuna Jukwaa la Wakulima wa Korosho liko kule Wilayani Masasi na wanafanya vikao vingi sana kwa Mheshimiwa Bwanausi kule Lulindi, tumeazimia Serikali isipochukua hatua juu ya ubadhirifu unaofanywa na kampuni ya Hammers kwa sababu wenyewe wanafahamika, sisi tutakwenda kufungua kesi mahakamani kwa maana ya kutaka kusaidia wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye taarifa ya CAG, anasema kwamba wamegundua Hammers walipopewa tenda ya kupelekea viuatilifu ikiwa ni pamoja na salfa walikuwa wanapunguza kwenye ile mifuko kwa hiyo kumepatikana hasara ya tani 144 sawasawa na thamani ya Sh.837,000,000 sasa hii ni uhujuma kiasi gani? Tunasema Serikali inataka kwenda kuboresha uzalishaji wa korosho, wanaopewa tenda kuleta viuatilifu wamekuwa wakihujumu kila mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine tumeambiwa kwamba nchi yetu inaelekea kuwa nchi ya viwanda hatuoni kabisa mkakati wa wazi unaounganisha Wizara ya Viwanda pamoja na Wizara ya Biashara. Hili zao la korosho ni la moja kwa moja ambalo linatakiwa liwe processed kabla ya kusafirisha ili tuweze kuongeza forex hapa sisi tulipo lakini hakuna mkakati wa moja kwa moja, Wizara hii imekuwa haipewi pesa za kusimamia shughuli zake za maendeleo, Wizara hii imekuwa na yenyewe inalalamika kama ambavyo wananchi wa kawaida kabisa wamekuwa
wakilalamika. Sasa hatuoni juhudi za moja kwa moja za Serikali hasa zaidi za Chama cha Mapinduzi kwa sababu ndiyo kinachoongoza ya kutaka kweli kuwakomboa wakulima hawa ambao tunaambiwa kilimo ni uti wa mgongo wa nchi yetu. Sasa leo tuko karne ya 21 lakini bado tunaambiwa kilimo ni uti wa mgongo na wazee wetu bado wanatumia jembe la kukokota na ng’ombe na wengine jembe la mkono ili kuweza kupata mazao. Tutapata kweli mazao ya kuweza kushindanisha na soko la dunia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la umwagiliaji. Tunatambua kabisa Wizara ya kilimo, wao wanasema hili suala liko upande wa Wizara ya Maji lakini kwa nini hiki Kitengo cha Umwagiliaji kisiwekwe pamoja na kitengo hiki cha Wizara ya Kilimo? Kwa sababu wao ndiyo wanatakiwa kuhakikisha mazao ya kilimo yanapatikana kwa wakati lakini pia kuonesha namna ambavyo watatumia hiyo ardhi yao. Matokeo yake kitengo hiki kimepelekwa kwenye sehemu ambapo wao wanachoangalia ni upatikanaji tu wa maji, nani ataendeleza yale mashamba ambayo yanatakiwa kuwepo pale?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hayo tu.