Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, napenda kuchukua nafasi hii muhimu kuishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi na Mheshimiwa Rais kwa jitihada zake anazochukua siku hadi siku kuhakikisha kilimo kinakua na wakulima wanapata unafuu. Mfano, kuwapunguzia kodi mbalimbali na tumeona kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri kuna changamoto nyingi za kodi na tozo mbalimbali zinakwenda kutatuliwa na kupatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Wizara na Serikali kwa ujumla, Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na viongozi wote wa Wizara. Tumeshuhudia juzi uwekaji wa jiwe la msingi la maghala na vihenge vya kisasa kabisa ambavyo vitachangia kwa kiasi kikubwa kuhifadhi mazao yetu yasiharibike na kupata soko na vilevile katika vihenge na maghala hayo, tutakuwa na uhakika wa usalama wa chakula hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, usalama wa chakula ni muhimu kwa sababu ni usalama wa Taifa. Tutakapokosa chakula hata hayo majeshi yetu yatashindwa kutulinda sisi na mipaka yetu. Kwa hiyo, nashauri Kitengo hiki cha NFRA kiongezewe fedha zaidi ili kuweza kununua mazao mengi kwa ajili ya usalama wa chakula lakini pia kuwasaidia wakulima wetu kupata masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyotambua kwamba karibu asilimia 65 ya malighafi za viwanda zinategemea mazao ya kilimo. Ni vyema sasa sekta hii ya kilimo ikaongezewa fedha zaidi ili kuhimili mahitaji yote ya kilimo ndani ya nchi yetu na kupata malighafi za viwanda vyetu ili tuweze kupata ajira kwa vijana wetu katika kilimo, viwanda na kuongeza Pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuliboresha au kulifanikisha suala hili ni lazima tujikite zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji. Kilimo cha umwagiliaji kitakuwa ndiyo nguzo muhimu ya kumkomboa mkulima mkubwa na mdogo kwa sababu mabadiliko ya hali ya hewa au mabadiliko ya tabia nchi yanayumbayumba na hivyo kusababisha kilimo chetu pia kiwe kinayumbayumba na hakina uhakika. Kwa hiyo, tukiwekeza zaidi kwenye sekta hii ya umwagiliaji tutaweza kupata masoko ya ndani na nje na tutapata malighafi za viwanda vyetu. Hilo liende sambamba na miundombinu ya barabara kule ambako kunazalishwa mazao mengi ili mazao hayo yasiharibike shambani na yaweze kufika kwenye maeneo ya masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mbegu bora ni la msingi zaidi. Ili kupata mbegu bora ni lazima tuviimarishe kwa kuviongezea mtaji vituo vyetu vya utafiti kama TARI na vinginevyo. Tukiviongezea fedha vituo hivi vikafanya utafiti wa mbegu bora tutaweza kupata mbegu bora ambazo zitasaidia hata kukabiliana na upungufu wa mafuta na sukari ambao tunao hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuishauri Serikali iongeze fedha au ipeleke fedha kwenye TFRA kwa sababu ya majukumu yake. Hii ni kutokana na hali ya sasa hivi ambapo kuna milipuko ya magonjwa na wadudu mbalimbali wanaoharibu mimea yetu, ni bora tukajua ni viuatilifu gani vinafaa kwa maeneo gani na kwa wadudu gani waharibifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuimarisha sekta binafsi ili iwekeze katika kilimo cha wawekezaji wadogo na wakubwa, ni vyema kukajengwa mazingira mazuri kwa wawekezaji hawa ili waweze kuwekeza kwa kiwango kikubwa. Hii ni pamoja na hatua mbalimbali zilizoanza kuchukuliwa na nyingine ziko kwenye mikakati ya kuchukuliwa ya kuangalia kodi na tozo mbalimbali ili kuwawezesha wawekezaji wetu kuvutika na uwekezaji katika sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, katika kuwekeza katika fani ya kilimo ni lazima kuwe na zana bora za kilimo. Kwa hiyo, ni vyema Benki ya Kilimo ikaongezewa mtaji ili itoe mikopo kwa wafanyabiashara au wakulima ili waweze kukopa vifaa vya kilimo kama matrekta kwa bei nafuu. Vinginevyo tutafute njia mbadala ya kuhakikisha wakulima wetu katika kila kijiji wanapata trekta na zana bora za kilimo na baadaye walipe kidogokidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linatakiwa liende sambamba na teknolojia ya usindikaji. Teknolojia yetu ya usindikaji iliyopo sasa tunapoteza mafuta mengi katika mashudu. Kwa hiyo, ni vyema tukapata teknolojia mpya na ya kisasa ili kuhakikisha mafuta yetu mengi hayapotei katika mashudu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, kuna masuala ya ushirika. Suala la ushirika limeongelewa sana na tumelieleza kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi ukurasa wa 112, Ibara ya 57(a) ambayo inasema, kuhakikisha kuwa shughuli zote zenye mwelekeo wa ushirika zitapewa msukumo stahiki kwa kuhamasisha na kusimamia kwa nguvu uanzishwaji wa vikundi vya ushirika kama vile SACCOS na vinginevyo, vyama vya mazao, ufugaji na vinginevyo. Mwisho inamalizia hapa, ushirika ndiyo silaha kuu ya wanyonge na nguzo kuu ya ujenzi wa siasa ya ujamaa na kujitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufuata kipengele hicho cha Ilani, vyama vya ushirika tulivyonavyo, kama kuna makosa madogomadogo ni vyema sasa tukayafanyia marekebisho, tukaviunda upya ili kweli viwe mkombozi wa mkulima mnyonge na wanyonge wengine hapa nchini Tanzania. Kwa sababu tumeona kwamba ndiyo nguzo kuu na silaha na mkombozi wa mnyonge kwa njia ya ujamaa na kujitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka jana tulikamata shilingi hapa ya Mheshimiwa Waziri kuhusu zao la minazi. Mwaka huu kitabu hiki cha Waziri sijaona akiongelea kuhusu zao la minazi. Zao hili ni la biashara, sasa hivi tunaagiza nazi kutoka nje ya nchi na kama sisi Tanzania tutaimarisha kilimo chetu cha minazi tutaweza kusafirisha nje ya nchi mazao yatokanayo na minazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwa mara nyingine kuwatakia kheri, wafanye kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.