Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Jeshi letu ya kuhakikisha inalinda mipaka ya nchi yetu kwa weledi, uaminifu na uzalendo wa hali ya juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kuna matukio ambayo yameanza kujitokeza hivi karibuni ya Jeshi kujiingiza au kuingizwa kwenye siasa za vyama. Mambo haya yanatakiwa kukemewa na kila Mtanzania makini anayeipenda nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo kilichofanywa tarehe 23 Septemba, 2017 wakati Maafisa Wanafunzi wakitunukiwa Kamisheni na Rais na Amiri Jeshi Mkuu cha kupokea wanachama wapya wa CCM hakitakiwi kurudiwa tena. Ni udhalilishaji wa Jeshi na nchi. Jeshi letu lina wajibu wa kulinda nchi na siyo chama cha siasa. Tanzania ikiwa ni nchi yenye mfumo wa vyama vingi, chama chochote cha siasa kinaweza kushinda uchaguzi na kuunda Serikali. Tukiona Jeshi linalotakiwa kuwa neutral linaegemea upande wa chama fulani linashusha hadhi ya Jeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe, Jeshi la Polisi limeshachafuka na kushuka hadhi yake. Jeshi pekee tunalolitegemea limejijengea heshima kubwa ni Jeshi letu la Ulinzi. Tunaomba hadhi hii isivurugwe na watu wachache wenye maslahi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya pili ni kuhusu ajira. Kuna malalamiko kutoka kwa vijana wa Operation Kikwete ambao wamefanya kazi na kulitumikia Jeshi kwa takriban miaka mitatu, wanashiriki operation mbalimbali ndani ya nchi yetu ikiwemo Operation Kibiti. Mbali na ushiriki wa operation zote na kulitumikia Taifa kwa moyo, wameambulia kurejeshwa nyumbani na nafasi zao kuchukuliwa na vijana ambao hawana uzoefu (wengine hata mwaka wa uzoefu hawana). Malalamiko yanahusu ajira mbalimbali zikiwemo ajira mpya za Jeshi la Polisi zilizotangazwa hivi karibuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana waliochukuliwa inasemekana hata usaili wa JWTZ walikuwa hawajafanya. Kwa lugha nyingine, kumekuwa na ubaguzi wa ajira baina ya vikosi vya Operation Kikwete na Operation Magufuli. Kuna sintofahamu kubwa sana ya vijana walioko mtaani. Tunaomba Waziri azungumzie hili na kutoa ufafanuzi wa sintofahamu hii na hisia za vijana ambao wanadhani hawajatendewa haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wanasema ajira zilizotolewa ndani ya JWTZ kupitia Mheshimiwa Rais akiwa Arusha hazikufuata utaratibu. Waliopata nafasi hizo ni watoto wa wakubwa Jeshini. Tunaomba ufafanuzi ili kuondoa sintofahamu hii.