Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la Jeshi kupambana na matukio ya kigaidi nchini. Ni vizuri Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania hususani Kitengo cha Upelelezi wa Kijeshi (Military Intelligence) kitoe msaada wa kipelelezi kwa Jeshi la Polisi ili kubaini na kukabiliana na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na watu wasiojulikana dhidi ya raia wasio na hatia. Kuna baadhi ya raia wanafikiria kuwa Polisi wamezidiwa mbinu na nguvu ya kukabiliana na magaidi hao hii ni kwa sababu Askari Polisi walishindwa kuyadhibiti matukio haya wakati yalipotokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kuna matukio mbalimbali ya kigaidi ambayo yametokea kama kuvamiwa kwa vituo vya polisi, kuporwa silaha Askari pamoja na wananchi kuuawa na hususani viongozi wa Serikali za Mitaa katika Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani. Matukio ya kigaidi bado yanaendelea katika nchi yetu. Naishauri Serikali kutumia intelijensia ya Jeshi kupeleleza wahusika wa matukio haya kwa lengo la kuyakomesha au kutumia vyombo vya nje kwa uchunguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Jeshi la Wananchi kama kisima cha fikra. Ukiachilia mbali jukumu la kulinda mipaka ya nchi, Jeshi ndiyo mbadala wa kila kitu nchi inapokuwa kwenye mkwamo. Ni vizuri Jeshi liwezeshwe kitaaluma na kubobea katika kila aina ya utaalam katika sekta zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi zilizoendelea, Jeshi ni kitovu cha utafiti na ugunduzi wa teknolojia za hali ya juu. Jeshi linatakiwa kufanya kila kitu nchi inapokuwa kwenye mkwamo. Ni dhahiri halitaweza kufanya kila kitu ikiwa halina utaalam katika kila sekta. Je, Serikali imewekeza kiasi gani katika shughuli za utafiti na ugunduzi katika Jeshi letu? Serikali itenge bajeti ya maendeleo ya kutosha ili iweze kukidhi mahitaji ya kufanya tafiti katika sekta mbalimbali ili kuwezesha ugunduzi na uvumbuzi wa teknolojia mpya katika sekta hizo kwa maendeleo endelevu ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, maboresho ya Sheria ya Ulinzi wa Taifa. Sheria ya Ulinzi wa Taifa ya mwaka 1996 ni ya zamani sana na kwa vyovyote vile haikidhi mahitaji ya mazingira ya sasa. Serikali imekuwa ikiahidi kuwa itaifanya maboresho sheria hiyo ili iendane na maendeleo ya sayansi na teknolojia lakini mpaka sasa ahadi hiyo haijatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwa ni ahadi ya Serikali kwamba mapendekezo ya upande wa pili wa Muungano (Zanzibar) juu ya sheria hiyo yangetekelezwa baada ya kusuasua kwa muda mrefu lakini mpaka sasa bado hayajapatikana. Tatizo hili linakwaza utendaji na maslahi ya Wanajeshi kwani sheria kutofanyiwa maboresho kwa miaka 52 sasa ni jambo lisilokubalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi. Kumekuwa na mgogoro wa mipaka kati ya nchi yetu na Malawi jambo ambalo linapelekea vikao vya usuluhishi kati ya nchi zote mbili kuitishwa kujadili namna ya kupata muafaka kwa suala hilo. Vilevile kulikuwa na tatizo la kuondolewa kwa alama za mipaka kati ya nchi yetu na Kenya katika maeneo ya Migori-Kenya na Tarime- Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi la kurejesha alama hizo limechukua muda mrefu sasa bila mafanikio. Ni vizuri Wizara husika katika nchi zote mbili ziongeze kasi ya urejeshaji wa alama hizo au kuna kitu kimejificha nyuma ya pazia juu ya kasi ndogo ya urejeshaji wa alama za mipaka kwa usalama wa Taifa letu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, Serikali kushindwa kulipa fidia kwa wananchi wa maeneo yaliyochukuliwa na JWTZ na JKT. Nasikitika kwa kitendo cha Serikali cha kuwanyang’anya na kuwadhulumu wananchi kwa kuchukua maeneo yao kwa ajili ya JWTZ na JKT na kukataa kuwalipa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitoa ahadi za kuwalipa fidia kwa maeneo yaliyochukuliwa na Jeshi mara kadhaa lakini haijatekeleza ahadi hizo jambo ambalo limewafanya wananchi waliochukuliwa maeneo yao kukata tamaa. Bajeti ya kulipa fidia huwa inatengwa lakini Serikali kwa makusudi huwa hailipi fidia hizo jambo ambalo tunaona ni sawa na kuwakomoa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, ushiriki wa ulinzi wa amani nje ya nchi. Pamoja na ushiriki wetu wa ulinzi wa amani nje ya nchi kupitia Jumuiya za Kikanda na Kimataifa, je, tangu utaratibu huu uanze hadi leo hii, ni Wanajeshi wangapi wamepoteza maisha na wangapi wamejeruhiwa? Vilevile ni kwa nini wajane wa Wanajeshi waliofariki hawatunzwi inavyostahili kama kipindi ambacho marehemu huyo/hao wangestaafu au wangekuwa hai?

Mheshimiwa Mwenyekiti, saba, ajira Jeshini. Pamoja na utaratibu uliowekwa wa kuajiri kwa kuchukua vijana kutoka JKT na JKU bado utaratibu wa ajira haujawekwa wazi vya kutosha. Kumekuwa na malalamiko kadhaa hususani kwa vijana wanaohitimu mafunzo ya JKT lakini kupata ajira Jeshini inakuwa ni vigumu au kuna vigezo vya ziada vinavyohitajika kuwaajiri vijana wanaohitimu JKT?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nane, bajeti ya maendeleo inayotolewa haiendani na azma ya kulifanya Jeshi kuwa la kisasa na lenye ufanisi. Mazoea haya mabaya ya utekelezaji duni wa bajeti ya maendeleo katika Wizara hii yanaonekana kuota mizizi na sasa yamekuwa ni kama desturi. Utekelezaji huu duni wa maendeleo unairudisha nyuma Wizara na unapunguza ufanisi, ubora na tija ya Majeshi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali kutotekeleza bajeti ya maendeleo ya Wizara hii siyo tu kunalifedhehesha Jeshi letu lakini pia kitendo hiki kinawaweka wananchi katika hali ya hatari kubwa (milipuko ya silaha katika maghala, ulemavu, uharibifu wa makazi na kadhalika). Ni vizuri Serikali ikajenga maabara ya kisasa zenye vifaa vinavyokidhi teknolojia ya kisasa ili kuwezesha Jeshi kufanya tafiti katika nyanja mbalimbali na kulisaidia Taifa kusonga mbele kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tisa, Jeshi kudhibiti shughuli za ndani za kisiasa. Siyo vizuri Serikali kulitumia Jeshi letu kwa shughuli za ndani za kisiasa. Vilevile siyo vizuri Jeshi kutumika katika masuala ya uchaguzi. Hii ni kazi ya Jeshi la Polisi lakini pia utakuta Jeshi linafanya shughuli za ndani za kisiasa. Ni vizuri Serikali kuliacha Jeshi lifanye kazi yake kwa mujibu wa sheria na kanuni zao za utendaji.