Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Abdallah Majurah Bulembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. ALHAJ ABBDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Awali ya yote nami nianze kwa kulipongeza Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania. Pamoja na hayo nimpongeze Mheshimiwa Waziri, hongera sana kwa kazi anayoifanya, yuko peke yake na inaonesha nawe ni jemadari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Katibu Mkuu, ndugu yangu Turuka; Naibu Katibu Mkuu, Mama Immaculate Ngwale; Mkuu wa Majeshi Jenerali Venance Mabeyo; Mnadhimu Mkuu Bwana Yacoub H. Mohamed; Mkuu wa JKT na wakubwa wengine wote ambao sikuwataja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee napongeza sana, mwaka 2017 nilikuwemo kwenye bajeti hii, hiki walichofanya Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Jenerali Mabeyo cha kuweza kuwaalika Majenerali wetu wote wastaafu, nawapongeza sana. Inatia moyo na inaonesha wapo na busara yao wanaitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa Maaskari wetu. Askari wetu wengi wako uraiani. Zamani sisi wakati tunakua, tulikuwa tunajua wanajeshi wanakaa kambini, lakini sasa Askari wetu wa Jeshi la Wananchi wako Mtaani. Naiomba Serikali yangu na Wizara, ni vizuri tukaendelea kuwaweka maaskari wetu kukaa kwenye vikosi; wakikaa huku uraiani ndio zile tabia ambazo fulani wamesema kwamba wanajiingiza kwenye mambo ambayo siyo sawa. Askari wa Jeshi la Wananchi eneo lake ni kikosini, ni kwenye detach, anapohitajika wakati wowote aweze kupatikana. Huo ni ushauri katika Serikali yangu, waliangalie tunafanyaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, ukiendelea hapo, ukiangalia, vikosi vingi leo vimeanza kusogelewa na wananchi. Vikisogelewa na wananchi, Jeshi hili linavyo vitu vingi sana vya siri na visivyotakiwa kuonekana uraiani. Mfano hai, kama mnakumbuka pale Mbagala tukio lililotokea ni kwa sababu wananchi wamesogelea Jeshi. Sasa hata Jeshi kufanya mambo yake inakuwa ni ngumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, naiomba Serikali yangu, kama walivyosema, eneo la Jeshi siyo la kusogelea sogelea maana wale ni walinzi wa nchi hii na wana vitu vingi sana vinavyotakiwa kukaa kwenye siri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemaji amesema neno hapa. Jeshi letu nafikiri ndiyo chombo muhimu kuliko sehemu yoyote ndani ya Wizara hizi; lakini Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Mpango wako hapa, inakuwaje Jeshi linapewa asilimia 60? Jeshi la Wananchi linapewa mapato kwa mwaka asilimia 60. Jeshi! Hapana! Hela ya Jeshi isicheleweshwe, isiwekewe kitu chochote. Hawa ndio watu muhimu zaidi kuliko sisi hapa wote tuliokuwepo huku, lakini wanawapelekea asilimia 60! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wanajitolea kufa. Ndiyo kama tunaosema wale 19. Sisi tunawapokea, tunawapa pole, kwa heri. Naishauri Serikali yangu, bajeti ya Jeshi isiguswe, isipunguzwe ni eneo muhimu. Mahitaji yao ni makubwa. Jeshi letu ni zuri, lina morali, lina majemadari wengi, makamanda wengi, ni la wananchi kweli, lakini haki ni stahili zao. Dunia inabadilika. Inaonekana Kenya kukiwa na kifaa, Jeshi la Tanzania halina; Rwanda ina kifaa, Jeshi la Tanzania halina, tunaongelea bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemaji mmoja amesema, bajeti yao ilikuwa kama trilioni tatu, tumewapa kidogo mno hii. Sasa hata hicho kidogo wanakimega! Hapana. Nafikiri Serikali ifanye operation kama inavyofanya kwenye madawa, inawapelekea bajeti kamili. Suala la hela ya Jeshi iende, wapate pesa zao, wafanye hayo wanayomudu kuyafanya bila kuweka suala lolote. Bahati nzuri niko Kamati ya Bajeti, Mheshimiwa Mpango huko nitakuwa nakumbusha kwamba jeshi haki yao imeenda? Tuwape. Hawa wako kwa ajili yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende JKT. JKT nawapongeza sana kwa kazi mnazofanya, nawapongeza kwa ukuta wa Mererani na Jeshi zima. Kazi waliyofanya ni kubwa, watu walisema haiwezekani, sasa imewezekana, lakini siku ile Rais alisema, wale vijana 3,000 wataendelea kuajiriwa. Naomba waajiriwe na wala wasicheleweshwe kwa sababu, kazi waliyoifanya ni ya mfano, imeonesha jeshi lipo, likitumwa linafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa nao wana tatizo. Ukiangalia SUMAJKT mambo yao wanayafanya kama Jeshi. Vifaa vyao bado ni duni. Hawawezi kufanya competition na wenzao, teknolojia yao bado ni ya chini. Sasa kama tunawasifia SUMAJKT wote humu ndani, tuwawezeshe basi tuwape vifaa liwe eneo la kujitegemea na kusaidia nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wale vijana wanaokwenda kwa mujibu, bajeti yao ni ndogo. Nimeangalia kwenye kitabu cha Waziri hapa. Sasa tumesema watoto warudi kule, wapitie JKT, wajenge Utanzania, bajeti haipo. Tunafanyaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri, hapo ni muhimu sana. Wapeni nguvu JKT waimarishe vijana wetu na nina imani kuna vijana wetu wengi humu, Waheshimiwa Wabunge wameenda kule JKT akiwepo akina Mheshimiwa Ester Bulaya, baada ya kuja, mambo yamebadilika, maana wamepiga kwata. Sasa kwa sababu ni eneo la kujenga Utanzania tuiunge mkono JKT, haki yake anaomba apewe ili kuweza kutuendeleza. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siko Kamati ya Ulinzi, lakini walinzi mnisamehe, hili la mipaka naomba kusema kidogo. Zamani kulikuwa na detach za wanajeshi katika mipaka yetu; Kigoma, Rukwa, Kagera, kwa nini wameziondoa? Aah, kuna nini kimetokea? Kwa sababu, nikisema haya ya akina Jenerali Mboma au nani wanajua huko juu kwamba kulikuwa kule kuna detach za Wanajeshi. Watu wakitaka kusogelea wanaogopa, lakini leo wamewaondoa wanajeshi kule. Kwa nini wamewaondoa? Wamebaki Askari. Askari sawa, ni Jeshi, lakini akishasimama mwanajeshi hata wale wenzetu wa nje wanajua mpaka ule hauingiliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nataka kutoa mfano, mtu anaweza kutoka Burundi akaja mpaka Tabora asionane na mtu yeyote kwa sababu, mpaka ule uko wazi. Kwa nini? Naomba sana Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Mabeyo hebu waturudishie detach zile, zilikuwa zina faida yake. Zilikuwa zinasababisha hata wanaoingia hawa wahamiaji haramu wanapungua, lakini leo, mpaka ni mkubwa, ulinzi ni kidogo, watu wanaingia wanavyotaka. Wananchi wetu wanauawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile Kigoma walikuwa wanauawa kila siku kwa sababu mipaka iko wazi, wale watu wa nje wanatoka na bunduki zao, wanateka magari yetu, wanasomba vitu wanarudi kwao. Naomba detach hizi za Jeshi zirudishwe kama hakuna sababu nyingine. Mheshimiwa Waziri anaweza akanijibu akija au atajua atakavyoniambia, lakini ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie maduka ya Jeshi. Maduka ya Jeshi yamefungwa, lakini yalikuwa yanawasaidia wanajeshi kupata afueni, wana exemption. Baada ya kuyafunga maduka yale, hawajawaongeza chochote kwenye mishahara yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maduka haya wameyafunga kwa nini? Kwa sababu, mwanajeshi alikuwa anaweza kwenda kule kununua mabati, cement na kadhalika. Kwa nini tunawapa exemption watu wengine, lakini hawa ndugu zetu wanaolala hoi kila siku wanatulinda, wanakesha maporini, wanaenda nje wanakufa, tunaona kama hili neno kuwawekea hii exemption ni kosa? Kwa nini jamani? Bati leo imefika Sh.300,000/= badala ya Sh.250,000/=, mwanajeshi atajenga huyu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwanajeshi ana nini zaidi ya kusimama barabarani na kuweka gari pembeni? Mwanajeshi kazi yake, akiamka asubuhi ni kazi, usiku ni kazi, lakini tumemwondolea yale maduka. Mimi sijui sana kwenye Serikali yangu huko ndani waliangalia nini? Nasema hawa Wanajeshi kama tumeondoa mduka ya bei rahisi, wawaongezee kitu kwenye mshahara wao. Saa za kazi kule kwao wakishakuwa wanawapa kitu zinaweza zikaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ninavyoambiwa, saa za kazi sasa zimeongezeka kwenye Jeshi; sasa mtu anaingia saa 12.00 anaondoka saa 8.00 za usiku, hana chochote. Naomba Mheshimiwa Waziri wakati anakuja anijibu kuhusu maduka haya, aniambie kwa nini wameyafunga maduka haya? Hata kama walikuwepo watu wanaenda kupata faida kwa ajili ya maduka, si wawazuie kule ni jeshini? Eeh, kama mtu anatoka kule kwenda kununua friji ya bei rahisi, wamzuie. Jeshini unaingiaje kirahisi rahisi? Eeh! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba maduka haya kwa kweli wasiyaache kwa sababu, ndugu zetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia la mwisho, Kagera Sugar. Pale kwenye Mto Kagera, kuna Kanisa lile lilipigana vita, Waheshimiwa Wanajeshi lile walifanyie utaratibu basi, ile hali iliyoko haifai, kwa sababu ni eneo la Vita vya Kagera. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante.