Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kuipongeza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuifanya Tanzania yenye viwanda kutimia. Pia kupongeza kauli ya Serikali iliyotolewa jana na Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu mafuta. Hali iliyopo nje kwa wapiga kura wetu ni mbaya, kwanza mafuta yamepotea, pili mafuta yamepandishwa bei sana. Tuzidi kuiomba Serikali kutatua sintofahamu zilizopo baina ya wafanyabiashara, TRA na Wizara ili mwezi wa mfungo wa Ramadhani mafuta yapatikane na kwa bei ya chini kama ilivyokuwa hapo awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili nizungumzie pia hali ya upoteaji wa sukari na upandaji bei. Kumekuwa na tabia ya wafanyabiashara kuficha mafuta, sukari na bidhaa nyingine za chakula na ifikapo mwezi Mtukufu wa Ramadhani wanaviachia na kuvipandisha bei na kuwasababishia Waislamu wanaofanya ibada hii muhimu kupata adha kubwa ya kupata mahitaji yao muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la makontena yaliyozuiliwa bandarini kwa kigezo cha kulipia kodi, hii ni hatari sana. Tende hizi zinatumiwa na Waislamu kipindi cha mfungo wa Ramadhani kwa mujibu wa kalenda yetu tunatarajia mfungo kuanza tarehe 17 Mei, 2018 na tende hizi ni kifungua kinywa muhimu sana kwa mwezi huu wa Ramadhani. Tuombe Serikali iliangalie hili suala ili basi TRA waweze kuruhusu makontena hayo na hatimaye Waislamu waanze mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda katika Mkoa wa Kigoma; Mkoa wa Kigoma tunalima zao la michikichi, tuliomba kupitia bajeti iliyopita kwa nini Wizara wasitoe ruzuku kwenye zao la michikichi ili kuwawezesha wakulima wengi ndani ya Mkoa wa Kigoma kulima zao hili kwa wingi tofauti na ilivyo sasa kuna mzungu, raia wa kigeni anavyo vitalu vya michikichi anauza kila mche mmoja shilingi 5,000 na ekari moja inahitajika michikichi 40 hadi 45.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo wakulima wengi wanaendelea kutumia michikichi yao ya asili tangu babu zao. Kwa kufanya hivyo hawapati mafuta ya kutosha, lakini wangepata miche ya ruzuku ya michikichi ya kisasa wangeweza kupata mafuta mengi ya kukidhi mahitaji ya walaji na pia kipato chao kingeongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wawekezaji wengi toka nje ya nchi wako tayari kuingia ubia na Watanzania kwenye viwanda vya kuunganisha pikipiki (bodaboda). Tatizo kubwa linalowakuta Watanzania ni kukosa Government Guarantee, kuwapa assurance wawekezaji kuingia ubia na Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niiombe Serikali kupeleka umeme Wilaya ya Uvinza ili kuwawezesha wananchi kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya mafuta ya mawese, mafuta ya mise na utengenezaji wa sabuni sambamba na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja, ahsante.