Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Bonnah Ladislaus Kamoli

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Segerea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naitwa Bonnah Kaluwa Mbunge wa Jimbo la Segerea. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kunileta hapa katika Bunge lako Tukufu na kuweza kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba pia niwashukuru wananchi wangu au wanachama wenzangu wa Jimbo la Segerea wa Chama cha Mapinduzi ambao waliweza kunipa tiketi ya kuja hapa bila kuwasahau wananchi wa vyama vya siasa kwa jina maarufu vyama vya UKAWA lakini pia wananchi wote wa Jimbo la Segerea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kwa dhati kumuunga mkono Mheshimiwa Rais John Joseph Pombe Magufuli kwa hotuba yake aliyoitoa siku ya tarehe 20 Novemba, 2015 ilikuwa hotuba nzuri ambayo ililenga kuwatatulia matatizo wananchi wetu.
Napenda nianze kwa kuchaangia katika suala la elimu. Napenda nitoe shukrani zangu za dhati na kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Segerea, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuondoa michango mbalimbali ambayo ilikuwepo kwenye shule zetu, kuanzaia shule za msingi mpaka shule za sekondari. Ninaongea hivyo kwa sababu nimekuwa ni mdau wa elimu kwa muda mrefu, tangu nikiwa Diwani nilikuwa nina mfuko ambao ulikuwa unahusika na kulipia watoto ambao wamefaulu lakini hawana uwezo wa kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, watoto wengi wameweza kufaidika na hii kauli ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa kwamba watoto wote waende shule na ikiwa shule ni bure na michango mbalimbali kwa sababu walikuwa wanapata shida na watoto wengi waliuwa hawawezi kwenda shuleni au kujiandikisha au wanachelewa kuanza shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kusema hayo naomba sasa nijikite kwenye masuala ya miundombinu ya elimu. Pamoja na Mheshimiwa Rais kutangaza kwamba elimu itakuwa bure lakini pia kuna changamoto nilikuwa nataka nizishauri kama Mbunge wa Jimbo la Segerea, kwa Jimbo langu ambalo lina shule za msingi 37 ambazo zina matatizo. Pamoja na kwamba shule zetu ni bure kwa sasa, lakini tulikuwa tunamuomba Mheshimiwa Rais aangalie au Mawaziri na watendaji waangalie shule zetu za Jimbo la Segerea zina matatizo makubwa.
Kwanza miundombinu yake siyo mizuri nikiwa na maana kwamba mazingira siyo rafiki kwa watoto ambao wanakwenda shule. Madawati hakuna, watoto wengi wanakaa chini, lakini mifumo mibovu ya vyoo, vyoo ni vibovu, unakuta shule ina watoto 2000 lakini ina matundu ya vyoo mawili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba shule ni bure lakini tuangalie na matatizo haya ya miundombinu, tunajua ndiyo kwanza tumeanza, changamoto ni nyingi, lakini ninaomba katika bajeti hii ambayo inayokuja, kama tunataka shule zetu ziwe bure na tuweze kutoa viwango vizuri na watoto wetu waweze kufaulu vizuri watoto wa kuanzia shule za msingi, basi tunaomba watutengenezee mazingira rafiki ambayo kwa kawaida watoto wanatakiwa wakae 45 kwenye darasa moja, lakini sasa hivi wanakaa watoto150 kwa hiyo watoto wanarundikana wengi, hata hivyo madarasa yemekuwa ni machakavu sana. Kwa Jiji maarufu kama Dar es salaam, itakuwa ni aibu sana kukuta watoto wanakaa chini. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri aangalie katika Bajeti inayokuja miundombinu ya elimu aiangalie sana katika Jimbo langu ambayo kuna shule nyingi na kuna sehemu zingine kwa sabau sasa hivi tumegawanisha Kata, kuna sehemu zingine hazina hata shule za msingi kwa sasa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata kama ya Buguruni ambayo ina wananchi wengi karibia 70,000 lakini hawana hata shule ya sekondari wanakwenda kusoma Kata za jirani. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, tunaomba utuangalie sana katika bajeti yako katika miundombinu ya elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuchangia katika miundombinu ya elimu, naomba nichangie katika masuala ya afya. Jimbo langu la Segerea, kwanza ni Jimbo lenye changamoto nyingi, lina watu wengi, kwa sensa iliyopita tulikuwa tuna watu karibu laki 5 na Jimbo langu la Segrea lina Kata 13, lakini katika Kata 13 tuna zahanati saba, hizi zahanati zote hazina vitendea kazi. Kuna zahanati zingine ambazo hazina hata umeme, wananchi wanakuwa wanapata shida kwa sababu itakapofika saa 12 jioni inabidi ifungwe. Wananchi wengi hawawezi kutibiwa maeneo hayo. Kwa hiyo kutakuwa na mrundikano wa watu wengi ambao wanatoka kwenye Jimbo la Segerea kuelekea hospitali ya Amana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Afya ya mwaka 2010 ilisema kwamba kila Kata inatakiwa kuwa na kituo cha afya na kuangalia kwenye Jimbo langu kwa sababu ya umuhimu wa watu wengi, tunaomba Mheshimiwa Waziri wa afya, atuangalie tupate kituo cha afya kwa sababu mpaka sasa hivi pamoja na kwamba tulikuwa tuna watu 375,000 ambao walijiandikisha kupiga kura lakini Jimbo lenye Kata 13 na lenye watu 375,000 hatuna kituo cha afya. Pamoja na kutokuwa na kituo cha afya, huduma zetu za afya kwenye hizo zahanati ambazo zipo hazikidhi viwango vinavyotolewa. Hakuna madawa, tumesema kwamba watoto kuanzia 0 mpaka miaka mitano wanapata huduma bure lakini wale watoto wakienda wanachokipata pale ni kuandkiwa dawa na kuambiwa muende mkanunue kwa sababu dawa hazipatikani.
Mheshiwa Waziri wa afya, tunaomba utuangalie lakini sambamba na hilo, tunajua kabisa Kata ya Mnyamani tuna mrundikano wa watu wengi lakini pia tuna hospitali moja ambayo pia katika Kata yetu ya Mnyamani kuna Mabwawa ambayo wanayotunzia maji machafu, Mheshimiwa Waziri tunaomba yale mabwawa yaweze kuondoka pale Mnyamani kwa sababu yanaleta hali ya hewa ambayo siyo nzuri kwa sababu yapo karibu na zahanati au na hospitali ambayo ipo kwa wakazi wa Mnyamani na magonjwa mengi ya mlipuko yanatokea Mnyamani kwa sababu mazingira siyo mazuri.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bonnah muda wako umekwisha!
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.