Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi nishukuru kwa kunipatia nafasi hii.

Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuweza kukutana na kuchangia Wizara hii ya Viwanda na Biashara. Lakini mara zote nimekuwa nikisema katika michango yangu kwamba Watanzania sijui tumekumbwa na balaa gani. Kwa sababu hapa viwanda vinazungumzwa kinadharia ziadi, lakini ukienda katika uhalisia mimi nasema hakuna kitu kwa sababu gani? Viwanda vilikuwepo, tulikuwa na viwanda vingi tu kwa mfano katika Jiji letu la Tanga tulikuwa na Kiwanda cha Mbolea, tulikuwa na Kiwanda cha Chuma (Steel Rolling Mills), tulikuwa na Gapex, tulikuwa na Kiwanda cha Sabuni (foma), tulikuwa na Amboni plastic, tulikuwa na CIC, tulikuwa na Kiwanda cha Mafuta ya Nazi (Nicoline), tulikuwa na Viwanda vya Sabuni Gardenia pamoja na railways. Tujiulize vitu vyote hivi viko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nimuweke sawa mchangia aliyechangia Mheshimiwa Devotha Minja katika historia ya Tanzania Tanga ndio ulikuwa mji wa pili kwa shughuli za kimaendeleo kwa sababu ulikuwa ni mji wa viwanda na uliweza kukusanya makabila yote Tanzania mpaka tukaweza kuingiza majirani zetu kama watu kutoka Malawi, kutoka Rwanda na Burundi, Uganda na Kenya wamekuja kufanya kazi Tanga lakini viwanda vyote vile vimekufa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tatizo kubwa ambalo naliona kwanza hatuna umeme wa uhakika, lakini pia umeme ni ghali kuliko dunia nzima na hayo si maneno yangu nafirikiri katika siku za karibuni Mheshimiwa Rais pia aliwahi kuzungumza kwamba Tanzania gharama za umeme ni kubwa ndio maana wazalishaji au wenye viwanda wanashindwa kuja. Hata hivyo hata kama una fedha unataka kuweka kiwanda umeme unakatika mara kwa mara utaajiri watu wakae-shift masaa manane mazima, masaa manne umeme hakuna, hilo haliwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nasema kwanza tupate umeme wa uhakika, lakini pili tupunguze utitiri wa kodi. Tanzania kodi zetu sio rafiki wa wafanyabiashara na wazalishaji na wenye viwanda. Kwa hiyo, lazima Serikali hapo ijitathimini na ijilinganishe na nchi majirani zetu. Kwa nini wawekezaji wengi wanakwenda Kenya, wanakwenda Rwanda, wanakwenda Msumbiji sasa hivi wanakwenda Uganda. Kwetu kuna matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda lingine ninaloweza kulizungumzia sisi ni wakulima wakubwa wa pamba, lakini tujiulize kwa nini Tanzania hadi leo tunaongoza kwa kuvaa mitumba, tena bahati mbaya zaidi hata leo kulikuwa na mjadala katika redio ya Clouds, kwamba kwanini Watanzania mpaka nguo za ndani, chupi, sidiria, soksi, gloves pia tunaingiza za mitumba wakati baada ya Sudan katika Afrika tunaoongoza kwa uzalishaji wa pamba ni sisi. Sasa lazima Serikali ijiangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwijage, usivitaje tu viwanda kinadharia, leo hata vijiti vya kuchokolea meno hizi toothpicks pia zinatoka China, handkerchief made in China sijui mijiti ya kuchomea mishikika pia made in China miaka 57 baada ya uhuru. Sasa tunaposema Tanzania ya viwanda tusizungumze kinadharia na tusizungumze kimisamiati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi kama Singapore, Malaysia, Vietnam hata China katika miaka ya 1970 huko tulikuwa angalau tunalingana lingana nazo. Kwa nini sasa hivi wenzetu wametuacha kiasi hiki? Kwa sababu hatuko serious, sisi katika kila jambo tunaingiza siasa na hapa ndiyo tunapoharibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri kama tunataka viwanda kweli tumejaza magofu ya viwanda wengine wanafugia mbuzi, wengine wamegeuza ma- godown, kuna viwanda vimebinafsishwa kwa watu binafsi, tujiulize hawa tuliobinafsishia viwanda hivi wanafanya shughuli gani sasa hivi? Wameweka yamekuwa ni ma- godown wengine wanafungua mashine zilizokuwa ni vyuma vya pua wanakwenda kuzalisha vyuma vipya au wanatengeneza scraper. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali iko wapi? Na pia tujiulize hivi viwanda baada ya kubinafsishwa hizi fedha zilizopatikana zimefanya shughuli gani? Nashauri ni vyema viwanda vile ambavyo vimekufa vikafungwa mitambo mipya ya kisasa tukapata umeme wa uhakika ili viwanda vyetu viweze kufanya kazi. Lakini pia tunapotamka viwanda tusifikirie kwamba itakayojenga hivyo viwanda ni Serikali maana yake hapa tunalolichukulia ni suala la viwanda kama vile Serikali ndiyo inayojenga viwanda. Tuweke mazingira mazuri ya kodi iwe rafiki kwa wawekezaji, lakini tuwe na umeme wa uhakika, na vilevile pia tuwe na attraction kwa hawa wawekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema hapa Mheshimiwa Kuchauka kuwa leo mtu akitaka leseni au akitaka kibali cha kujenga anasumbuliwa kuna urasimu wa jambo la saa moja Tanzania litachukua siku nne lakini akienda Kenya au Uganda jambo la saa moja ndani ya dakika 20 keshapata kibali.