Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi kuchangia Wizara hii ya Viwanda na Biashara. Nitaanza upande wa viwanda na uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili suala ambalo linaendelea sasa hivi kwa Kiswahili linasema kuongeza thamani au kwa Kingereza ku-add value. Suala hili kama hatukulifanyia utafiti wa dhati litatuletea mtafaruku mkubwa. Maana yangu kusema hivyo ni kwamba, kila mwenye kiwanda sasa hivi anapigania kuzuia wananchi wasiuze mali zao akiwa anasema yeye yupo tayari kununua mali yote na kui-add value. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano. Hapa tunakatazwa kuuza mahindi nchi za nje tunaambiwa tuuze sembe lakini watu wa Kongo sembe wanachanganya na muhogo, sasa utawauziaje sembe na wenyewe wakachanganye muhogo, wanakwambia wanataka mahindi ili wakasage waweke muhogo. Kwa kuwa Waziri yuko hapa aliangalie kwa makini sana suala hili, kama mtu anasema anataka ku-add value ni lazima aoneshe uwezo wa kiwanda chake ataweza kweli kununua mali za Watanzania ili watu wasikae na mali zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano kwenye ngozi. Sasa hivi karibu ngozi zote zinatupwa, zimezuiwa na zimewekewa export levy ya 80% na indication price iliyowekwa na TRA ni senti 58 ya Dola ambayo ni Sh.1,300 lakini bei ya ngozi leo duniani ni senti 35 ambayo ni Sh.800. Itawezekana vipi sasa mtu alipie Sh.1,300 auze Sh.800? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumesaini mkataba na Uganda na Kenya kwenye hilo suala la ngozi. Wenzetu Waganda na Wakenya wana-under value invoice, wanalipia kwa bei chini na kununua mali zetu, ni kwa nini na sisi wananchi wetu wasiruhusiwa kuuza mali zao ili kuondoa huu mtafaruku ambao unaendelea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaungana na Wabunge wenzangu kwenye suala hili la Liganga na Mchuchuma ingawaje mimi mtizamo wangu uko tofauti kidogo. Mtizamo wangu mimi ni kwamba, madini haya kwa utafiti wa wataalam wetu wanavyosema yako mengi kiasi cha kutosha miaka 100 lakini miaka 100 kwa dunia inavyokwenda haraka ni kweli teknolojia hiyo au chuma hicho kitakuwa kinatakiwa duniani. Kwa nini tusiwe na option mbili, tukawa na option ya kuuza udongo wa chuma kama ulivyo na tukawa na option ya kuyeyusha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya analysis ya madini yaliyomo mle ndani nchi nyingi duniani wakati bei ya chuma au madini fulani yanapanda wanauza kwa ajili ya kupata pesa muda ule na kujikimu. Sasa hivi hapa kwetu tunalia kwamba, hatuna pesa ya maji lakini tuna mlima zaidi ya miaka 50, kuna ubaya gani kufanya analysis na baadhi ya mawe yale yakaendelea kuuzwa ili tupate pesa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwenye Jimbo letu la Kahama au Wilaya yetu ya Kahama na Mkoa wa Shinyanga mwaka huu tuna mavuno mazuri sana ya mpunga. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri hili neno la add value aliangalie. Sisi tunataka kuuza mpunga au mchele kwa Waganda lakini tunabanwa na sheria inayosema huwezi kuuza mpunga lazima ukoboe mchele, lakini wakati unasubiri kukoboa mchele hilo soko litakuwa linakusubiri kweli kule Uganda? Haiwezekani. Ni lazima Mawaziri wafikirie sana suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kwenye suala la biashara. Kwenye mkutano wa Mheshimiwa Rais ni kweli mambo mengi sana yalijitokeza pale. Ukiangalia maswali mengi ya wafanyabiashara ilikuwa ni kwenye tatizo la Sheria ya Importation na Sheria ya Kodi ya Mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Importation inatusumbua, sisi tunatumia tarrif ambayo haisumbui sana ukienda kwenye vitu kama mafuta ta dizeli, sukari, simenti na vinywaji kwa kuwa hawa wanatumia ujazo au kilo lakini unapokwenda kwenye item ndogondogo, nitatoa mfano wa item moja, kwa mfano wewe ume-import glass, glass kwenye tarrif inaitwa glassware, lakini kuna glass ya Sh.10,000 na ya Sh.1,000 lakini TRA ata-pick glass ya Sh.10,000 kuku-charge wewe wa glass ya Sh.1,000/=. Kwa hiyo, tunamwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kuwa yuko hapa ni miongoni mwa kero nyingi sana ambazo wafanyabiashara wamezionesha wakati wa kufanya importation. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna tatizo kubwa sisi tunaotoka mikoa ya mpakani. Kuna hii sheria mpya ya ku- declare pesa. Wananchi walioko Kongo, Burundi, Uganda wanataka kuja kununua mali kwetu Mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Geita. Haiwezekani mtu atoke Uganda au atoke Kongo afike Mutukula aoneshe Dola zake 50,000 apande basi, ni kitu ambacho hakiwezekani hata iweje. Tumeshuhudia wote hapa mtu anatoka kuchukua pesa pale Mlimani City anavamiwa anauawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Waziri wa Fedha kwa kuwa yuko hapa alifikirie, hili neno tume-copy kwa Wazungu, kwao ni sawa, London uki-declare hakuna mtu atakuvamia lakini ku-declare kilometa 300 upite porini ambako mpaka mabasi yanafanyiwa escort na wewe ulionesha dola, tumekwama kabisa watu wa nje wamekataa kuja kununua mali kwetu kwa sababu hiyo, hawawezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia nchi hizo ni zile ambazo hazina mfumo wa kibenki, Kongo hakuna benki, Burundi kuna vita, watu hao wote wanatembea na cash. Nafikiri Waziri wa Fedha kwa kuwa yuko hapa ajaribu sana kulifikiria suala hili ambalo linatusumbua sana. Sisi Mwanza tunauza samaki, mchele na vitu vingi lakini mpaka sasa tumekwama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia kwa kuwa na Waziri wa Nishati yuko hapa tungeomba sana wenzetu wa TANESCO waruhusu, kama walivyoruhusu kwenye transformer, kwa wafanyabiashara hasa wanaotaka kuanzisha viwanda kama wanaweza kuvuta umeme kwa gharama yao halafu wakawarudishia wakati wa bili inapoanza. Kwa kuwa, yeye sasa hivi analalamika kwamba hana pesa ya kununua nguzo au vifaa vya umeme itasaidia watu wanaotaka kuanzisha viwanda waweze kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huo, naunga mkono hoja, ahsante sana.