Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Andrew John Chenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Naibu wake, Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu na Watendaji wote wa Wizara hii pamoja na wataalam wa taasisi ambazo ziko chini ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba hii ni pana, ni nzuri na inatoa mwelekeo. Sote tumekubaliana kwamba Wizara hii ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ni mojawapo ya sekta za kipaumbele katika Mpango wetu wa Maendeleo katika kuipeleka nchi yetu kufikia uchumi wa kati na nguzo kubwa ni viwanda. Tunaliona hili, wamelisemea vizuri, changamoto zilizopo na jinsi wanavyokabiliana nazo, nawapongeza sana, endeleeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nasumbuliwa sana na suala zima la gharama za uwekezaji nchini, bado ziko juu sana. Hili limesemwa vizuri tu kwenye hotuba unaona hali ya upatikanaji wa umeme, maji na miundombinu mingine yote ya kiuchumi ambayo inaendana na kufanikisha uwekezaji gharama gharama ziko juu. Sasa, kuanzia leo mniite Bwana Reli, kwa sababu nitakuwa naizungumzia katika kila Wizara hata kama haihusiki nayo. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake huo na tutakapokamilisha reli hii tutaona uchumi wa Tanzania utaibuka kama uyoga, ikumbukeni tarehe ya leo, Bwana Reli anasema. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, narudia kama nilivyosema juzi wakati nachangia kwenye Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Pamoja na jitihada nzuri za sasa, napenda Serikali iendelee kutafuta mikopo ya masharti nafuu ili tuweze kushambulia ujenzi wa reli hii tuikamilishe. Hii ni kwa maana ya reli ya kati pamoja na matawi yake yote ya msingi, tufanye kazi hiyo na tutaona uchumi wa nchi utakavyokua kwa kasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishuke kwenye upande wa mradi huu wa siku nyingi sana wa Liganga kwa chuma na Mchuchuma kwa upande wa makaa ya mawe. Kusema ukweli kwa nchi hii kama mpaka leo tunaendelea kuongea kwa lugha hiyo ni tatizo. Hata kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri nadhani ukurasa wa 13, hiyo Kamati ya wataalam, kinachosemwa pale ni kwamba timu hiyo imekamilisha taarifa ya awali wala hatuambiwi ni nini. Maana Waheshimiwa Wabunge, hizi sheria mbili tulizopitisha mwaka jana, mimi nasema Bunge lipo, kama kuna vifungu ambavyo tunaamini kwamba vinakwamisha kwenda mbele, Serikali ndiyo ileile iliyoleta Miswada hiyo Bungeni sasa Serikali hiyohiyo haiwezi ikaogopa kurejea Bungeni na kueleza kwa nini hatuendi mbele. Bunge lipo ndiyo kazi hiyo, watajenga hoja, tutawasikiliza na tutafanya marekebisho twende mbele. Haiwezekani tunaenda mbele tunarudi. Tangu mwaka 2011 Septemba waliposaini mkataba, NDC pamoja na ile kampuni ya China, what is wrong with us Tanzanians? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani tuna vivutio lakini hatuendi mble, jenga hoja, unamwambia mwekezaji bwana, haya hatuyakubali, mwambie ili afunge virago aende lakini hatuwezi kila mwaka tunaenda mbele na kurudi nyuma. Mimi nasema tuufikishe mradi huu mwisho. Mheshimiwa Waziri, tueleze exactly changamoto ni nini kwa sababu navyokumbuka mimi mkataba ule unatoa 20% ya free carried interest kwa Serikali bila kulipa kwa sababu madini hayo ni National patrimony yetu. Pia inaiwezesha Serikali kupitia NDC kupata an additional 49%. Tuliweka wazi kabisa kwamba mikopo yote ya uwekezaji itakayochukuliwa ambayo wana-estimate kuwa three billion US dollars, ni lazima ikubalike na pande zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi huwa nasema tufike mahali mradi huu utekelezwe. Tulikuwa tumepanga by now, mwaka huu wa fedha, kwa upande wa umeme tungekuwa tumefikia hizo megawatt 600 na chuma kingekuwa kimeanza kuzalishwa mwaka 2015. Kwa hiyo, reli hii tungekuwa tunaanza kutumia vyuma vyetu lakini what is wrong with us? Tusimuangushe Rais Magufuli kwa nia yake njema ya kuleta maendeleo ya haraka kwa nchi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma ukurasa wa 69 wa hotuba kuhusu hili suala la tozo na ada zenye kero zinazojirudiarudia, tumelisema, bado tunaelezwa ooh, tunakaribia kumaliza. Mheshimiwa Waziri nadhani unapohitimisha, hebu mtueleze exactly, najua kuna vested interest za Mawaziri, wanataka kuendelea taasisi ambazo ziko chini ya Wizara zao, wanategemea sana mapato yanayotokana na tozo na ada hizi lakini sisi tunataka kujenga mazingira mazuri ya kuwekeza na kufanyia biashara Tanzania. Kama tozo basi ziwe na mtiririko mmoja, tunasema One Stop Centre. Tumeona Benjamin Mkapa wameweka wote pale, tungependa hata Export Processing Zones za maeneo ya mikoani utaratibu huohuo utumike maana humkwazi mwekezaji. Nadhani tuyafanyie kazi haraka haya maana tumeyasema sana mpaka unafika mahali unachoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa jambo la jumla tu. Kusema kweli tunafanya kazi nzuri, amelisema vizuri sana Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu na nilimsikiliza Mheshimiwa Rais kwenye National Business Council siku ile lakini hayo ambayo yameamuliwa pale napenda visiwe vikao hivi ambavyo havina record, havina yatokanayo ili kikao kinachokuja haya mengi haya yawe yameshatanzuliwa, siyo tena wanakumbushana kulikuwa na kikwazo gani, tumalize tunaenda mbele. Mheshimiwa Waziri, wewe ndiyo sekta yako hii, hayo ambayo unadhani yanakukwamisha lazima uwe mwepesi kuyasema na ndiyo maana taasisi ambazo ziko chini ya Wizara hiyo zina wataalam wengi tu. Angalia hayo ambayo wameyafanya, nadhani tukifanya kwa haraka tutayafanikisha lakini sio ya watu wazima tunaongea kila mwaka yale yale hatuendi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nimeona project za kielelezo ni hii reli yetu ya kutoka Tanga – Arusha - Engaruka. Sasa najiuliza, nimesoma speech ya Waziri wa Ujenzi juzi, ninyi mnachotuambia ni nini hapa maana inaonekana hamuongei pamoja. Mnachosema kwenda kutekeleza, mtatekeleza nini maana kule kwenye ujenzi hatukuona chochote ambacho kinaongelewa kuhusu ujenzi wa reli mpya ya kutoka Arusha - Lake Natron na mwaka kesho mtakuja na lugha hizi hizi, kwa hiyo tunabaki hapo hapo. Let’s walk the talk tumalize, yale ambayo hatuwezi kuyafanya tuseme haya hatuwezi kuyafanya sekta binafsi itakuja tu kama tutaijengea mazingira wezeshi na rafiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, nikupongeze sana Waziri na timu yako, endeleeni. Mazingira ndiyo hayo lakini tusibebe mambo mengi kwa wakati mmoja. Tuchukue vipaumbele vichache tuweze kuvisimamia ili twende mbele. Ahsanteni sana, naunga mkono hoja.