Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana kwanza naomba kwa kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wa Maji; na kwa faida ya Bunge lako tukufu niseme tu kwamba sisi Watanzania ni ndugu. Maana yake ni kwamba Kamwelwe ni Kandege, Kakunda ni Kandege na Kandege ni Kandege kwa hiyo, tuko vizuri tunatumia jina moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitoe ufafanuzi kwa maeneo machache; kuna Waheshimiwa Wabunge ambao wamezungumza kwamba shule zote na taasisi zote za huduma za jamii zipatiwe huduma ya maji. Nitoe taarifa kwamba tumeshaziagiza Halmashauri zote kuweka kipaumbele cha kupeleka huduma za maji kwenye taasisi zote ikiwemo shule, zahanati, vituo vya afya na hospitali na tunalifuatilia sana kwa karibu agizo hilo kuhusu utekelezaji wake na tumewaambia Wakurugenzi wa Halmashauri tunawapima kwa kutekeleza vipaumbele hivi. Aidha, tumeagiza majengo yote ya shule na majengo ya taasisi yawekewe mifumo ya kuvuna maji mvua ili kusudi kupata maji ya uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili; wako Wabunge ambao wamezungumzia umuhimu wa kuhamisha watumishi wetu mara kwa mara ili kuongeza ufanisi. Hilo ni wazo zuri, tumeshaanza kulifanyia kazi. Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita tu tumeshahamisha watumishi 26 na zoezi hili linaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utekelezaji wetu, sisi katika serikali za mitaa, tunatekeleza kazi zetu kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 145 na Ibara ya 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Sheria Na. 7 kwa Halmashauri za Wilaya; Sheria Na. 8 kwa Halmashauri za Miji. Vilevile tunafuatilia sana utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Maji Na.12 ya mwaka 2009. Katika sheria zote hizo, kazi za Halmashauri na Serikali za Mitaa kwa ujumla ni utekelezaji wa miradi ikiwemo miradi ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi za Serikali Kuu kwa ngazi za Mikoa na Wilaya ni ufuatiliaji na usimamizi. Kazi ya Wizara ya Maji ni kubwa mno, kutunga sera, mikakati, sheria, kanuni, miongozo ya kitaalam, ufuatiliaji na tathimini. Miradi mikubwa inayohudumia wilaya zaidi ya moja, vilevile miradi mikubwa mikubwa ambayo inahudumia Mikoa zaidi ya mmoja. Lakini kubwa zaidi wanafanya kazi kubwa sana ya kutafuta fedha za kutekelezea miradi hiyo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ushirikiano wetu ni mkubwa sana sana. Na changamoto katika kazi hizi kubwa huwa hazikosi. Kwa hiyo tunaendelea kutatua changamoto kwa ushirikiano.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningesema mengi lakini mengi namuachia mwenyewe Mheshimiwa kaka yangu atayazungumza yanayohusu mambo yote ya kitaalamu kuhusu miradi ya maji atazungumza. Naomba sana kuunga mkono hoja, ahsante sana.