Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. John John Mnyika

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika majumuisho naomba majibu ya Serikali kuhusu masuala yafuatayo mahsusi ya Jimbo la Kibamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, Kata ya Goba kuna shida ya maji mitaa yote. DAWASCO/DAWASA waliahidi kwamba maji yatapatikana baada ya ujenzi wa matenki ya maji Sabasaba na Changanyikeni. Hata hivyo, ukweli ni kuwa maji hayajapatikana kwa wakati kwa kuwa mabomba ya maji hayajaanza kabisa kusambazwa. Wizara ieleze lini mabomba yataanza kusambazwa kwenye Kata nzima ya Goba.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Msigani ina mitaa mitano; mitaa ya Msingwa, Malambamawili, Temboni, Msigani na kwa Yusuph yapo mabomba ambayo yalijengwa awamu ya kwanza (maarufu kama mabomba ya Mchina) na ya sasa (maarufu kama mabomba ya Kihindi) ambayo mpaka sasa hayatoi maji. Ni lini yataanza kutoa maji? Aidha, yapo maeneo katika mitaa hiyo ambayo hakuna kabisa mabomba. Ni lini maeneo hayo mabomba yatasambazwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Saranga, mitaa saba ina mabomba ya maji lakini si maeneo yote maji yanatoka. Hivyo, DAWASCO ifuatilie katika maeneo ambayo maji hayatoki. Hata hivyo katika kata hiyo kuna mitaa miwili ya Saranga na Ukombozi ambayo hayana kabisa mabomba ya maji. Wizara ieleze ni hatua gani ya haraka zinachukuliwa kuhakikisha kwamba mabomba ya maji yanasambazwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Kibamba miradi ya maji inasuasua, kuna maeneo mabomba yamerundikwa bila kuchimbiwa kwa muda mrefu na mitaro imeachwa wazi. Hivyo, hatua zichukuliwe kuhakikisha mabomba hayo yanachimbwa na pia maeneo ambayo hayana mabomba nayo mabomba yatandazwe kwa haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Mbezi mitaa ya Msakwi na Msakwi Kusini hali ya maji ni mbaya. Yapo mabomba ambayo kwa muda mrefu hayatoi maji. Aidha, mitaa ya Mpiji Magohe na Msumi haina kabisa mabomba ya maji hivyo Wizara ieleze ni lini mabomba ya maji yatasambazwa katika maeneo hayo. Wizara ihakikishe fedha zilizopaswa kupelekwa kwa Manispaa ya Ubungo zinafikishwa kwa haraka kupunguza ukubwa wa tatizo. Lakini izingatie kuwa misaada hiyo hailingani na ukubwa wa mahitaji na kasi ya ukuaji wa maenezo ya wakazi katika mitaa hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kunajitokeza tatizo katika eneo linalojengwa barabara ya lami kutoka Mbezi kwenda Goba ambapo TANROADS walijenga juu ya mabomba bila tahadhari hivyo mabomba yamepasuka wananchi kukosa maji na miundombinu kuharibika hasa karibu na Mazulu Kanisani na Njiapanda ya Goba na Makabe. Hali hiyo iko pia Mbezi mwisho round about.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Kwembe ipo mitaa ambayo mabomba yamewekwa lakini mpaka sasa maji hayatoki, ni lini maeneo hayo yatatoka maji? Aidha, limejitokeza tatizo katika maeneo hayo la mkandarasi kutoshindilia vya kutosha na kuweka kifusi mwaka baada ya kuchimba mitaro na kuwekwa mabomba. Matokeo yake ni kuwa mvua zimenyesha na udongo kuondoka na mabomba kubaki wazi na miundombinu ya barabara kuharibika. Kabla ya wakandarasi kumaliziwa malipo yao watakiwe kwenda kurekebisha miundombinu hiyo. Aidha, kuna mitaa kwenye kata hiyo ambayo haina kabisa mabomba, ni lini yatasambazwa? Kwa ujumla kuchukua hatua kamili DAWASCO ikutane.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa dharura na madiwani na wenyeviti wa mitaa na watendaji wa Jimbo la Kibamba mapema mwezi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, upatikanaji wa maji katika eneo linalohudumiwa na Ruvu Chini si wa uhakika pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanyika kwenye mitambo ya Ruvu Chini. Hali ni tete zaidi wakati wa ukame ikilinganisha na kipindi cha mvua. Hali itakuwa mbaya zaidi kutokana na mabadiliko ya tabianchi (climate change). Hivyo, ujenzi wa Bwawa la Kidunda unapaswa kuharakishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Waziri pamoja na taarifa ya Kamati zinajenga matumaini hewa kwamba ujenzi unakwenda kuanza. Hata hivyo, ukweli ni kuwa randama ya Wizara inaonesha kuwa ili mradi ukamilike kinahitajika kiasi cha dola za Marekani milioni 215. Taarifa nilizonazo ni kuwa mpaka sasa Serikali imeshindwa makubaliano na masharti ya kupata mkopo kuhusu mradi huo. Hivyo Wizara ieleze katika majumuisho ni namna gani fedha za mradi huo zitapatikana kwa kiasi cha kutosha katika mwaka huu wa fedha na ni lini mradi huo utakamilika? Wizara izingatie kuwa miaka nane iliyopita tumehoji kuhusu mradi huo na Wizara imekuwa ikitoa majibu ya kutoa matumaini bila utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya mchakato unaoendelea wa kuunganisha DAWASA na DAWASCO, naomba Wizara katika majumuisho itoe maelezo ya kina juu ya mchakato huo. Aidha, kama Mbunge wa Jiji la Dar es Salaam naomba kupatiwa nakala ya taarifa zilizoombwa na Kamati kuhusu mchakato huo hasa kwa kuzingatia pia suala hilo linapaswa kuhusisha marekebisho ya sheria au kutungwa kwa sheria mpya ya kusimamia masuala ya maji katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo ya jirani ya Mkoa wa Pwani yanayohudumiwa na mabomba ya Ruvu Juu na Chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bunge la Kumi kutokana na ukubwa wa matatizo ya maji nchini na haja ya Wabunge kupata majibu ya kina nilitoa hoja na Serikali ikakubali kwamba kwenye kila Mkutano wa Bunge Serikali ilikuwa ikiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji. Kwa hali ilivyo kwa sasa ya wastani wa upatikanaji wa maji vijijini wa asilimia 56 tu kwa vijiji na asilimia 69 kwa mijini pamoja na hoja ya nyongeza ya fedha, upo umuhimu wa Bunge hili la Kumi na Moja Serikali kuweka utaratibu wa Wizara ya Maji kutoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kila Mkutano wa Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, fursa ya maswali ya Wabunge pekee haitoshi ndiyo maana kwenye Mkutano wa Bunge, Wabunge husimama kutaka maswali ya nyongeza bila kupata nafasi. Katika kujibu michango ya Wabunge, Serikali ieleze itakavyotekeleza utaratibu huo.