Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Nishukuru pia Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi na fursa ya kuweza kuchangia katika hoja hii muhimu kwani maji ni uhai, maji ni kilimo, maji ni uchumi, maji kwa kweli ni kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi naomba nianze kwa kuungana na wachangiaji wenzangu kuishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi njema inayoifanya ya kuhakikisha inapeleka maji mijini na vijijini kwa kiwango ambacho kimeripotiwa katika taarifa hii. Ni ukweli usiopingika kwamba kazi ya kupeleka huduma za maji hasa mijini imefanyika vizuri na ndiyo maana hata Mheshimiwa Msigwa mwaka 2010 nilikuwa naye Kamati ya Maji, mara baada ya kuona Serikali ya CCM imepeleka zaidi ya asilimia 99 katika mji wake wa Iringa alifikiria hata ajiondoe kwenye Kamati kwa sababu hali ilikuwa ni nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niungane na mchangiaji aliyemaliza mwanangu Msigwa hebu usiwe na ndimi mbili, ulisema tununue ndege kwa ajili ya uchumi ulipokuwa Maliasili tumenunua, leo unasema tena ndege hazifai. Jana ulisema tujenge standard gauge, leo unasema tena tusijenge, kupanga ni kuchagua. Rais wetu ameamua kupeleka fedha na kujenga miundombinu ya kiuchumi ili kutengeneza fedha sasa za kwenda kujenga miradi ya maji kwa fedha zetu wenyewe bila kutegemea wafadhili. Ni kilio cha muda mrefu cha Wabunge, tulikuwa tunategemea fedha ziletwe na wafadhili, miradi inasimama tunategemea Benki ya Dunia…

T A A R I F A . . .

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nafikiri anataka nisaidie tu kuendelea kutoa elimu kwamba huwezi kudai maji kama huna fedha. Kwa hiyo, miradi inayofanyika hii ya kujenga miundombinu ya kiuchumi lengo lake Tanzania iweze kujitosheleza kwa fedha na kuweza kupeleka maji vijijini, maji mijini na ndiyo maana nimesema kupanga ni kuchagua na nchi yoyote duniani huwezi ukafanya mambo yote kwa wakati mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, jana hapa Mzee Chenge ameeleza vizuri sana kwamba Serikali sasa imeamua kupeleka fedha za ndani kujenga miradi ya maji. Sasa kama huna fedha zako za ndani, hujaimarisha utalii ukanunua ndege, hujajenga miundombinu ya kuleta uchumi, hizi fedha za kupeleka maji vijijini utapata wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka kusema na Wabunge na kwa kweli na Watanzania wanaotusikiliza, mimi ni mama na ni mdau mkubwa wa maji, Ilani ya CCM tumedhamiria kuwatua wanawake ndoo kichwani. Nataka niwahakikishie ni kweli kama ambavyo amesema Waziri kwenye kitabu chake ukurasa wa saba kwamba ifikapo mwaka 2020 tutapeleka miundombinu ya maji kwa kiwango cha asilimia 85. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwahakikishie kwa sababu miradi mingi iko kwenye mchakato na miradi ya maji inajengwa kwa muda mrefu. Kama lipo tatizo la fedha kutumika vibaya, tumpe nafasi Waziri, naungana na Mheshimiwa Bulembo, hatuna haja ya kuunda Tume kwa sababu kuunda Tume unaongeza gharama. Waziri Mheshimiwa Kamwelwe ana nia njema, kwa muda mfupi tumemuona, yuko smart na ni mtu anayefuatilia, waende wakae chini wakokotoe na mimi kwenye mchango wangu wa maandishi nimempa kabisa na njia za kukokotoa kwamba kuna miradi tuliyofadhiliwa na Benki ya Dunia tupate taarifa ni vijiji vingapi, fedha ngapi zilikwenda, vingapi vimekamilika na vingapi bado na hiyo pesa iko wapi na kama ilitumika vibaya waliohusika wako wapi, Waziri anaweza kazi hiyo. Vilevile miradi ambayo inaendelea fedha yake iko wapi, waliomaliza zile certificate walipwe ili ifikapo mwaka 2020 miradi iwe imefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusema kwamba tuendelee kuiamini Serikali yetu ambayo ina nia njema na imejiandaa vizuri. Kama ambavyo Serikali imeweza kupeleka fedha za dawa na fedha za maji tutapeleka kwa sababu ndiyo kipaumbele pia cha Serikali ya CCM. Kama ambavyo tumeweza kujenga shule katika kila kata na siku moja suala la maji litabaki kuwa historia. Kama ambavyo tumeweza kupeleka madawati kila shule na mpaka yamebaki ya ziada tutafanya, kama ambavyo tunafanya miradi mikubwa ya kimkakati ya kuchimba gesi na mingine na mingine. Tuendelee kuwa na imani, imani huzaa imani na subira huvuta heri. Hakuna nchi yoyote duniani inaweza ikaendelea kwa kuwa na miradi mingi na huu ushauri tumekuwa tukiutoa sisi Wabunge kwamba twende na miradi michache inayotekelezeka, lakini ya kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa niendelee kuishauri Serikali, jamani kilio cha Wabunge wengi mmekisikia na mimi ninayezungumza ni mdau naongea na wanawake. Tunaomba katika mwaka huu wa fedha hii miradi ikamilike na mwaka wa fedha ujao katika vipaumbele mtakavyovipanga maji, maji, maji, maji na bajeti ya maji iwe ni kubwa na fedha zote zipelekwe kama ambavyo zimepitishwa. Nina imani Serikali kwa kuwa ni sikivu wametusikia, kilio cha Wabunge ni kikubwa, kilio cha wanawake ni kikubwa na mimi hivi karibuni nilikuwa vijijini wamesema na mimi nahakikisha tutahakikisha maji yanapelekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie mradi wa Mgango - Kiabakari - Butiama. Mheshimiwa Waziri nimefurahi kweli nimeona katika ukurasa wa 37 umezungumziwa. Hivi mnataka Mke wa Baba wa Taifa Mama Maria ndiyo aje kuomba maji hapa? Huu mradi umeanza tangu mwaka 1978, umefanyiwa tathmini miaka 15 iliyopita kupitia wafadhili wa BADEA wametenga USD 32, leo hapa naona mmeandika 30.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi tangu nimekuwa Mbunge huu sasa ni mwaka wa kumi na kitu, tunazungumzia uendelezaji wa huu mradi hivi kuna shida gani na huu mradi? Hivi kweli Mama Maria aje kutuomba maji hapa Bungeni? Nataka nikuombe Mheshimiwa Kamwelwe utakapohitimisha leo uzungumze na wananchi wa Butiama na Mama Maria Nyerere akusikie. Hivi huu mradi wa BADEA unakuja lini? Kama mradi huu haupo, Serikali ina mkakati gani wa kutenga fedha zake za ndani kama ambavyo mmefanya katika miradi mingine, tupeleke maji kutoka Kiabakari - Butiama mpaka Mgango. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jamani Baba wa Taifa alikuwa ni kiongozi, alikuwa hajipendelei, aliangalia Watanzania wote na ndiyo maana mpaka leo hata barabara ya kwenda kwake haijajengwa ndiyo inajengwa sasa, tena mmeweka wakandarasi kumi, tumevumilia tunakubali. Mwalimu aliangalia watu wote, alipeleka maji mpaka Kilimanjaro yanatiririka yenyewe kupitia kwenye milima, hakujiangalia yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali mpo hapa, hizi fedha za BADEA ni lini zinakuja na zipo kwa nani? Nakuomba jioni hii utakapo-windup hapa tuambie ili kama fedha hazipo tukawaambie wananchi wa Butiama, tukaongee na Mama Maria Nyerere kwamba huu mradi wa maji sahau mama hautakuwepo, tuendelee kuchimba maji na kutumia Mto Kialani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona nizungumze hili kwa uchungu kwa sababu nimekaa miaka kumi, huu mradi nimeupigania muda mrefu, Serikali iliniahidi kwamba BADEA ipo na hapa naiona, lakini leo nimesikitika kwamba eti sasa unaenda kufanyiwa tena upembuzi yakinifu, upi na wakati upembuzi yakinifu ulishafanyika. Hebu leo Mheshimiwa Waziri toa kauli yako na sina mashaka na wewe utafanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa pia kujua huu mradi utahudumia wananchi wa Kata ya Mgango pale ambapo chanzo kipo, kwa sababu wale wananchi chanzo kinatoka pale lakini hawahudumiwi na mradi huu. Napenda kujua hizi fedha pia zitakazotengwa na BADEA watapeleka maji Kiliba na Tegeluka, Kata hiyo hiyo ya Musoma Vijijini au itaishia hapo peke yake na kupeleka Kiabakari hawa ambao ndiyo wa chanzo cha maji watabaki kuwa watazamaji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujua hii Wilaya ya Musoma Vijiji, Wilaya aliyozaliwa Baba wa Taifa, Wilaya ambayo imeasisiwa miaka mingi iliyopita kutokea Mrangi mpaka Busekela, kutokea Busekela mpaka Kukilango na Bugwema, hivi tatizo la maji ni la nini wakati Wilaya imezaungukwa na ziwa? Nimepekuapekua humu sikuona vizuri, hebu tuambie Wilaya hii ya Musoma Vijijini na Butiama Serikali ina mpango gani kuwafikishia wananchi maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kuipongeza Serikali kwa kusikiliza kilio cha muda mrefu cha Wabunge kupeleka huduma ya maji katika Mji wetu wa Musoma na miji mingine mingi hapa nchini, hali sasa hivi ni nzuri ikiwepo na Jiji la Dar es Salaam, napongeza sana. Dar es Salaam sasa miundombinu ya maji imejengwa, hata juzi nilipokuwa kwenye kampeni Kinondoni haikuwa tena hoja, naomba niipongeze Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu sasa naiomba Serikali pelekeni fedha DAWASA na DAWASCO kwa ajlili ya kujenga miundombinu ya maji maana iliyokuwepo imechakaa na mabomba yanapasuka kusababisha upotevu wa maji na kwenye taarifa ya Waziri umesema. Bila kujenga hii miundombinu na pressure ya maji haya yanayokuja kwa sababu ni mengi tutakuwa hatujafanya chochote na maji yatakuwa yanapotea bila sababu yoyote. Ukiwemo na Mji wa Musoma, Bukoba na miji mingine yote ambayo miundombinu yake imechakaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilete ombi maalum huo mradi wa BADEA unachelewa, nawaomba tu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Naunga mkono hoja, ahsante sana. Mengine nimeleta kwa maandishi myazingatie, ahsante.