Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya mimi kuchangia jioni ya leo katika bajeti hii ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuchangia Wizara hii ya Maji kwangu mimi naomba Mungu anisaidie nipate akili ya kusema vizuri kwa sababu ninaweza nikaruka humu Bungeni. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu aliwahi kusema ni bora kuongoza maskini mwenye matumaini kuliko kuongoza maskini asiye na matumaini na maskini mwenye matumaini ni yule aliyelima mihogo au ana shamba anaweza kumkopa mwenzake fedha kwa kumuomba kwamba mahindi yake yakifika atauza atamlipa lakini yule ambaye hana kitu kabisa huyo ni maskini asiye na matumaini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bunge hili mimi naona ni maskini nisiye na matumaini maana kila bajeti inayokuja sioni kwenye Jimbo langu la Bunda kuna chochote mle ndani. Kwa hiyo, inavyofika wakati huu naona kwamba hivi Bungeni humu nafanya biashara gani humu ndani? Si bora tu nitoke nikachunge ng’ombe huko? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Bunda na Bunda kwa ujumla kuna miradi mbalimbali na mimi nashangaa watu wanasema hamna fedha, nadhani fedha zipo ila usimamizi wake ni kidogo sana au tuna ugonjwa unaoitwa D by D, hii ambayo wataalam wametupatia. Wizara ya Maji inatoa fedha kwenda kwenye Halmashauri, mamilioni ya fedha yanaenda, watekelezaji wa miradi ile ni watu wa TAMISEMI, wahandisi wako TAMISEMI na pengine hata Waziri wa TAMISEMI au Naibu wake, watumishi wake hawajui fedha ngapi imeenda huko, inajulikana kwa Wizara ya Maji tu peke yake. Waziri wa Maji anapokwenda kukagua maji anakuta fedha zimeliwa. Ukimuuliza Waziri sasa huyu achukuliwe hatua gani anakwambia mimi hao siyo wangu mpaka niende kushauriana na Mheshimiwa Jafo, hii biashara hatuiwezi hii, hii biashara itakuwa ngumu sana.

Kwa hiyo, ni vizuri tukaangalia huu ugonjwa wa D by D tunaufanyaje katika hizi Wizara mbili, vinginevyo tutapata shida sana na ndiyo maana tumeshauri hapa mara kwa mara kwamba Wakala wa Maji Vijijini uwepo ili Waziri apewe vitu vyote, fedha na watu wake aweze kuwatumikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie miradi ya Wilaya ya Bunda kwa ujumla, tuna Mradi wa Kibara shilingi milioni 400, zimetumika pale kama shilingi milioni 300 na zaidi maji hayatoki, lakini kwenye taarifa utaonesha maji yanatoka. Kuna Mradi wa Buramba, shilingi milioni 353, maji hayatoki, kuna Mradi wa Kinyambwiga shilingi milioni 395, maji hayatoki, kuna Mradi wa Kwing’ombe shilingi milioni 700, mradi umeisha na Mwenge ukafungua, maji hayatoki, kuna Mradi wa Nyamswa Salamakati, shilingi milioni 252 zimetumika, maji hayatoki, kuna Mradi wa ufadhili wa Bomamaji, walikuja wafadhili pale Bomamaji wakatoa shilingi milioni 987 zimeliwa, ripoti ikatolewa haifanyiwi kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi mkubwa wa maji wa Bunda ambao bomba lake linatoka Nyabeho nao unasuasua. Mbaya zaidi kuna mradi wa Mgeta, Nyang’aranga zikatolewa shilingi milioni 495 zimefika shilingi milioni 910 maji hayatoki na Waziri ameshafika pale akiwa Naibu Waziri. Sasa hili linakuwa ni tatizo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi ni kwamba ukimuuliza Waziri hapa nimezungumza habari ya malambo kule kwetu sisi Bunda malambo hayo ndiyo visima tunaita, ndiyo ng’ombe na binadamu wanakunywa. Tukamwambie atutengenezee malambo ambayo yalitengenezwa na Chifu Makongoro yatatusaidia huko tunapokwenda, akakubali hapa Bungeni kwamba atatengeneza hayo malambo akasema leteni mpango. Tumepeleka mpango tukamkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara, kuidhinisha huo mpango uende kujengwa ukija kumuuliza Waziri anakwambia malambo sichimbi mimi, anachimba Wizara ya Kilimo lakini Wizara hii ya Maji ndiyo yenye malambo. Sasa najiuliza hii ni kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa kwamba kiasi cha shilingi bilioni moja bajeti ya 2016/2017 hatukuitumia, Halmashauri ya Bunda haikupata taarifa. Bajeti ya mwaka 2017/2018 tumewekewa shilingi bilioni moja tumeleta mpango wa maji wa malambo sita hayachimbwi wala hamna kibali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Bunda una mradi mkubwa wa maji na kuna kitu kinaitwa chujio. Mimi nimwombe Waziri, pale wanasema kuna shilingi bilioni 12, wanasema ni nyingi labda hizi ni za wizi. Sasa kama ni za wizi ngapi zinatosha sasa kwa sababu katika kuchimba, mimi siyo mtaalamu lakini katika mambo ya kuchimba hilo chujio kuna vitu vinaitwa clarifier, flocculant, rapid stand, refilter, mitambo na kuna vitu vingi mle ndani. Wataalam wa Wizara si waende waangalie kwamba ni fedha ngapi zinatosha kuweka hiyo chujio. Kwa sababu maji ya Bunda kila siku yanaletwa maji machafu, kila Waziri anayekuja mnanywesha maji machafu kwa nini sasa msipeleke wataalam watuambie hili chujio badala ya shilingi bilioni 16 ni bilioni ngapi? Wakati fulani tunaweza tukawa tunawalaumu watu tu kwamba mkandarasi amekula, amefanyaje, twendeni tukajiridhishe na mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze habari ya fedha, tumezungumza mwaka jana kwenye bajeti Sh.50 kuongezeka kwenye mafuta kwa ajili ya kupata fedha za kuhudumia maji lakini imekuwa wimbo. Sasa Wabunge tukubaliane, wakati fulani mimi nasema na tutaendelea kusema, humu ndani tukifa wote watasema Wabunge wa Tanzania wamekufa, hawatasema CCM wala CHADEMA. Ifike muda tukubaliane kwamba kwenye mambo yale ambayo tunakubali ni halali tuache UCCM wala UCHADEMA tukubaliane hoja. Kwa nini tunaweka shilingi 50 kwenye mafuta iende kwenye maji halafu haiwekwi, nani anaizuia na sisi ndiyo wawekaji wa fedha? Kwa hiyo, nafikiri Waziri anapokuja hapa atuambie anafanyaje kuhakikisha kwamba hiyo fedha kwa kipindi hiki itakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Waziri, najua wakati fulani tukisema haya mambo yanamgusa Waziri, Naibu na watendaji wake, lakini watu hawa nao ni wapya. Hebu tuweke mtazamo mzuri, hivi Waziri anaposema shilingi bilioni moja imekwenda Bunda, lakini haikutumika, anatulaumu sisi Wabunge, hivi nani ana utaratibu wa kuwaambia Halmashauri fulani kwamba jamani kuna fedha zenu hapa mbona hatujaona proposal yenu ya kuanzisha miradi? Kwani wataalam wa Wizara ya Maji wana kazi gani? Kwani nani anaweza kujua mradi Bunda iko miradi mitano wanaandika imekamilika lakini haitoi maji, nani anaweza kujua? Ina maana Wizara ya Maji haina watu wa IT ambao wanaoweza kujua vitu hivi? Siku hizi watu wanafanya vitu kwenye computer kwa nini haya mambo hayafanyiki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua bajeti tutampitishia Mheshimiwa Waziri najua na wewe una bidii sana ya kufanya kazi lakini mimi kwangu uadilifu si hoja. Kwangu mimi mtu awe mwadilifu na awe mbunifu. Unaweza kuwa na mwadilifu anakaa na hela tu kwenye droo hapo watu wanakufa bila maji. Kwa hiyo, tunajua Waziri wewe ni mwadilifu jitahidi kufanya innovative na creative kwenye ofisi yako ili watu waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe ile proposal yangu ya Bunda ya malambo, sisi malambo ndiyo visima, atupitishie ili watu wakapate maji. Toka mwaka 2008 hii miradi imeanza kuzungumzwa humu ndani na bajeti zinakuwepo, lakini haitekelezeki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengi, naunga mkono hoja, ahsante.