Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Zaynab Matitu Vulu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha siku ya leo kujadili hotuba ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Nampongeza Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuunga mkono hoja, naomba nipate maelezo ya kina juu ya juhudi za Serikali kuhusiana na zao la nazi maana ni zaidi ya miaka 10 sasa zao hili limekuwa linapotea kwa kushambuliwa na wadudu mwishowe hufa. Mimi natoka Mkoa wa Pwani ambako sehemu kubwa tunalima zao hili na ndilo linaendesha maisha ya Wanapwani. Zao hilo halihitaji mvua na wala halina matatizo kipindi cha jua. Zao hili huvunwa mara nne kwa mwaka. Kwa taarifa tu, maeneo mengi kwa sasa watu wananunua nazi zinazotoka Mombasa. Kwenye mnazi tunapata samani, mafuta ya kula, kujengea nyumba na maji (madafu) ni kiburudisho na pia hutumika kama tiba mbadala inapobidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na kituo cha utafiti wa zao la nazi pale Mikocheni. Kwa masikitiko sijaona juhudi zozote za kusaidia tiba ya mdudu huyu mharibifu. Pia naomba Serikali iwe na mpango wa kuwasaidia waathirika wa minazi hiyo ama kwa kuwapa zao mbadala au miche mipya ya minazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina hakika Mheshimiwa Waziri na Naibu wake mtalipa Kipaumbele ombi langu na kunipatia majibu stahiki, kwani nimekuwa nauliza jambo hili katika kila bajeti sijapata jibu. Pia naomba mfikirie kuanzisha bodi ya zao hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la wavuvi hasa wadogo wadogo ambao wanatozwa leseni ambao kipato chao ni kidogo. Naomba Serikali ijiwekeze kwenye viwanda vya samaki ili kuwasaidia wavuvi wadogo wadogo ambao wanauza samaki kwa wenye viwanda. Wavuvi hawa hupata hasara maana wenye viwanda hushusha bei kila baada ya masaa na mvuvi anapoingia baharini au ziwani hana uhakika wa wingi wa samaki na hao anaowapata huuza kwa bei ndogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria za wavuvi wadogo na wakubwa ni vyema zikaagaliwa tena hasa ile ya uvaaji wa vifaa vya kuokolea kwenye kina kirefu cha maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, uchomaji wa nyavu za wavuvi nao uangaliwe upya. Ni vema kuzuia uingizaji wa nyavu hizo ili wasiweze kuzipata. Naomba msimamo wa Serikali juu ya suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.