Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi nichangie Wizara hii ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tunashuhudia Wizara hii kwa muda mrefu, lakini kwangu nilichokiona muhimu sana katika hii Wizara ni uadilifu wa Wizara. Uadilifu wa Wizara ya Elimu sasa hivi umekuwa mkubwa sana kwa sababu fedha zote zinazotoka kwenye Wizara zinakwenda chini zinafika salama na zinafanya kazi salama. Zamani ilikuwa fedha zikija huku zinarudi tena Wizarani huko huko lakini siku hizi zinafanya kazi vizuri sana. Kwa hiyo, nisifu uadilifu wa Wizara hii umekuwa mkubwa, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima, Katibu, Naibu na wote wanafanya kazi vizuri sana, kwa kweli wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako malalamiko machache ambayo naona pale vijijini kwa sababu vitabu vile vya wanafunzi wa darasa la nne wanafanya mitihani havijaenda, lakini nimepiga simu kule wameniambia ndio vimeanza kwenda. Kama vinaenda kweli naomba vifike salama kwa sababu wanafunzi wanavihitaji vifike kwa wakati lakini tunafikiri kwamba Serikali imefanya vizuri kupeleka hivyo vitabu mapema na vinaendelea kusambazwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu Jimbo langu la Bunda na hili nimelisema muda mrefu. Wizara ya Elimu imetupa majengo mazuri sana kwenye Shule ya Makongoro ambayo ina wanafunzi wa high school na wale wa kidato cha nne lakini jengo la Bwalo la Makongoro
limejengwa mpaka kwenye lenta limeshindwa kumalizika na fedha yake ilikuwa imepungua. Tunaiomba Wizara itusaidie kwenye hilo jengo ili liweze kumalizika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekondari ya Nyamang’unta na Sekondari ya Salama kuna majengo ya maabara yameshindwa kukamilika. Tunaomba mtusaidie ili yaweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Msingi Salawe na Shule ya Msingi Stephen Wassira, majengo yalianguka na watoto wawili walifariki na taarifa zilitolewa kwenye vyombo vya habari na tukatoa taarifa Wizarani, TAMISEMI inajua na Wizara ya Elimu inajua. Mliahidi kutusaidia tunaomba mtusaidie hizo shule mbili ziweze kupata majengo yake kwa sababu watoto walipotea na wananchi walipata mateso ya kuhangaika muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule za Chamriho Sekondari na Mihingo Sekondari watoto wake wanatoka kilometa 17 kutoka eneo la kijiji wanachokaa na wasichana wale wakianza 50 wanamaliza 12 au watano. Kwa hiyo, tunahitaji shule hizi mbili zipate mabweni ili watoto wa kike waweze kusoma katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala muhimu sana ambalo mimi sijui kama mnaliona lakini lina-affect sana hii industry ya elimu kwa maana ya kiwanda cha elimu hiki ambalo ni masuala ya mikopo. Kama hatutaweza kudhibiti mikopo ya mabenki kwa walimu; mwalimu anapokea mshahara wa shilingi 2,000,000 lakini anaenda kupokea mshahara wa shilingi 150,000 na siyo walimu tu na watumishi wengine wote wa Serikali hii, kama hizi sheria za mikopo za mabenki kwa watumishi wa Serikali hatuwezi kuzidhibiti vizuri maana yake ni kwamba hakuna uaminifu utakaokuwepo. Ni lazima tuone mshahara unabaki kama sheria inavyosema. Mtu anapokea mshahara shilingi 300,000 anapokea shilingi 50,000 wengine wanapokea shilingi sifuri. Kwa hiyo, tufanye tathmini ya kujua hii mishahara ya watumishi na hasa walimu ambao wakati fulani hawana hela za akiba tuone tutadhibiti vipi ili walimu waweze kutumika vizuri kwenye shule zetu.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ni kiwanda na tatizo liko hapa elimu yetu nzuri au mbaya? Ili kutambua elimu nzuri au mbaya ni namna gani tunazalisha? Je, tunazalisha watu wenye ubora kulingana na soko lilivyo au ni watu wasio na ubora kulingana na soko? Kwa sababu unaweza kuzalisha jambo, kwa mfano sasa hivi tunazungumza habari ya viwanda na kama tunazalisha watu wa historia, tunazungumzia watu ambao hawako kwenye mambo ya ustawi wa jamii na kwenye mambo ya ufundi kama walivyosema wenzangu, shule za ufundi hazipo, hivi tunalenga nini hasa?

Kwa hiyo, kwenye soko letu tunakokwenda huku mbele halitakuwepo, hatutapata watumishi wanaoweza kwenda kwenye viwanda. Elimu inataka unazalisha nini, ni suala la demand and supply. Kwa hiyo, tuweze kujua kwamba elimu yetu hii tunayozalisha watoto wakoje, ndiyo hilo wanasema quality education na quality in education, ni vitu viwili tofauti. Kwa hiyo, tuangalie michango yetu inakwendaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la matangazo la Baraza la Mitihani. Mimi huwa mara kwa mara najiuliza sana, mtu anakaa pale kwenye tv anatangaza, mitihani kidato cha kwanza au mitihani primary shule bora, St. Mary, St. Augustine, sasa unalinganisha na nini? Shule yangu ya Mihingo ina mwalimu mmoja toka inaanza. Shule yangu ya msingi watoto wanasoma nje, wana matatizo mbalimbali, unakuja kusema imekuwa ya mwisho kwa kulinganisha na nini, unalinganisha nani sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri kwamba mambo haya tuweze kuweka categories ili tulinganishe maana sasa hii mitihani tunalinganisha na nani? Huyu amekuwa bora kwa kulinganisha na nani? Hivi kweli leo unaweza kuleta hapa Barcelona ukasema inacheza sijui na Yanga halafu useme imekuwa ya kwanza eti kwa sababu tu ni sheria inaruhusu?

Kwa hiyo, nafikiri hata mitaala hii nayo tuiangalie upya wakati fulani haileti maana sana kwenye mambo haya ambayo yanakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule nyingi tumezungumza kwenye mambo ya sera. Mimi nafikiri huo mfumo unaouzungumza kwamba kuwepo na kongamano zito, alizungumza Mzee Mkapa, akazungumza Mzee Jakaya na hata Mheshimiwa Magufuli akitoka mtasema Mheshimiwa Magufuli alizungumza. Kwa hiyo, nafikiri kwamba hii mijadala hii iendelee kuwepo na hakuna mtu anazuia mjadala, nami nawaomba Wizara ya Elimu pale watu wanapotaka kufanya mijadala ya elimu basi tuwaunge mkono ili tuweze kuona kitu bora tutakachokuja kufanya katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naunga mkono hoja.