Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Maftaha Abdallah Nachuma

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala kwa kunijalia afya njema. Pia nikushukuru wewe kuweza kunipa nafasi niweze kuchangia kwa dakika hizi tano kwenye Wizara hii ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaalam mmoja anaitwa Kunzi alisema mwaka 1988/1989 alipomaliza kuandika kitabu chake akasema kwamba failure to plan is planning to fail (ukishindwa kupanga maana yake umepanga kufeli). Nilikuwa nasikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri hapa, maneno yake mengi amezungumza, lakini sijaona hata mstari mmoja kwenye kitabu chake hiki ameeleza ana mkakati gani juu ya elimu ya watu wazima Tanzania. (Makofi)

Mheshmiwa Mwenyekiti, elimu ya watu wazima taarifa ya Kamati imeeleza hapa kwamba wako vijana wengi, wapo Watanzania wengi sana hawajui kusoma na kuandika. Hawa wawekewe mkakati maalum, wapewe masomo maalum na watengewe bajeti kwenye Wizara hii. Elimu ya watu wazima imekufa, tunaomba sana Wizara mwaka huu iweze kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kugharamia elimu ya watu wazima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Nne ilinikuta mimi nikiwa mwalimu na nilikuwa Headmaster wa Mchinga Sekondari, shule ambayo Mheshimiwa Bobali kaizungumza hapa, nimekaa pale kwa miaka mitano kama Mkuu wa Shule. Tulikuwa na mpango huu kwa muda mrefu sana wa kuipandisha hadhi ile shule iweze kuwa ni kidato cha tano na sita, miundombinu yote tulikamilisha, mimi naungana mkono na Mheshimiwa Bobali hii shule iweze kupanda kuwa ya kidato cha tano na sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo lilikuwa ni zuri sana ni suala la BRN, mpango ambao Serikali waliuiga kutoka Malaysia na kule Malaysia walikuwa wanaita The Big Fast Result. Serikali ya Awamu ya Nne ikasema tuige mpango huu wa kuinua kiwango cha elimu na sekta nyingine tano ili tuweze kuwa na matokeo makubwa. Mimi nashangaa sana kwamba hivi sasa huu mpango wa BRN (Big Results Now) wameuacha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu ulikuwa una tija sana katika shule zetu za msingi na sekondari. Walimu walikuwa wanafanya kazi kwa bidii sana kwa sababu walikuwa wanaahidiwa kwamba somo lako wakifaulu wanafunzi kwa kiasi hiki utakuwa motivated kwa kiasi hiki cha pesa, kwa kiasi hiki cha tour lakini na mambo mengine.

Kuuondoa Mpango wa Big Results Now kwenye Wizara hii ya Elimu maana yake tunarudisha nyuma elimu yetu. Tunaomba sana Serikali irudi kwenye BRN, ilikuwa inafanya vizuri sana, ilikuwa inachochea sana elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwaka 2014, shule yangu ya Mchinga sekondari pale ilikuwa ni shule ya kwanza katika shule za Serikali, Kanda ya Kusini kupitia mpango huu wa BRN. Tuliweza kusimamia vizuri sana, tulipeleka vijana wengi, takribani 21 kwenda form five na six. Naomba sana mpango huu tuweze kuuresheja ili kuweza kurudisha morali katika shule zetu za sekondari na za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni hili suala la uhaba wa madarasa. Ni kweli kabisa kwamba shule zetu zina enrollment kubwa sana, kutokana na Mpango wa Elimu Bure wanafunzi wengi wanaingia darasa la kwanza madarasa hayatoshi. Shule ya Msingi Mbae, Mtwara Mjini hii ni mara yangu ya tatu nazungumza hapa, ina wanafunzi zaidi ya 600, madarasa yaliyopo ni mawili pekee. Wanafunzi 600 madarasa mawili, ni jambo la ajabu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Wizara ipeleke pesa Shule ya Msingi Mbae iliyopo Mtwara Mjini tuweze kujenga madarasa na vyoo, hata vyoo pale hakuna, naomba sana Wizara iangalie suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la upungufu wa walimu wa sayansi pia ni jambo muhimu sana. Nashauri kwamba vyuo vyetu ambavyo vilikuwa vinafundisha walimu wa masomo ya sayansi viwekewe msisitizo, vitengewe bajeti ya kutosha na walimu wafundishwe masomo ya sayansi sawasawa. Hivi sasa imekuwa walimu wengi wanakimbia kwa sababu hakuna motivation. Walimu wengi wa sayansi waliofundishwa na Serikali wanakwenda katika shule za private kwa sababu kule kuna malipo ya kutosha, incentives za kutosha, motivation ya kutosha, shule zetu za sekondari za Serikali zinakosa walimu wa sayansi kwa sababu hatuna vivutio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati fulani ilielezwa sana hii sera kwamba tunahitaji walimu wa sayansi waweze kubaki katika hizi shule za Serikali, tutawapa motivation maalum, lakini mpaka leo hakuna wanachopata cha ziada walimu wa sayansi katika shule zetu za Serikali. Tunaomba yale yanayozungumzwa yaweze kutekelezwa ili elimu yetu iweze kuwa kama maeneo mengine.

T A A R I F A . . .

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Taarifa yake naichua lakini ni kwa sababu PPP tunayozungumza Tanzania siyo kwenye elimu tu, tunazungumza kwenye sekta nyingi kuwe na ushirikiano huu sekta binafsi na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nizungumze suala lingine kwamba elimu yetu wanafunzi wanaishia katika elimu ya juu. Tulitembelea baadhi ya Vyuo Vikuu Tanzania katika Kamati yetu ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, tumefika pale MUCE (Mkwawa University College of Education) kuna ufisadi mkubwa unaofanywa na watendaji ambao Serikali ama sisi Watanzania tumewapa dhamana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kuna jengo la maabara linajengwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)