Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi niende moja kwa moja kwenye point zangu; kwamba kidato cha tano na cha sita Wilaya ya Kilombero mwaka huu wametupa shule moja ndani ya Jimbo la Kilombero pale Sanji. Sasa mimi siwezi kusema sana, lakini Jimbo la Mlimba linaeleweka yaani ni kubwa, pana, miundombinu mibovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tulikuwa tumeomba na sisi tupate kidato cha sita, kwa hiyo kwa sababu bajeti ya mwaka huu inapita na mmeshapanga hicho kwa hiyo naomba mkumbuke kunako majaliwa kipindi kijacho cha mwaka ujao wa fedha mtuwekee na sisi ndani ya Jimbo la Mlimba na tumeshapendekeza hizo shule za kuweka kidato cha sita, hiyo itasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madeni ya walimu. Ukizungumzia kuhusu madeni ya walimu nchi nzima ni shida. Walimu wameshahakikiwa na katika kazi zao kule katika ofisi zao wameshaweka vizuri, sasa kwa nini Serikali hailipi hawa walimu madeni yao, kigugumizi cha nini jamani? Hamuoni kama mnawavunja moyo hawa walimu? Afadhali huku mjini watu wanapiga biashara labda ice cream nini wanauza shuleni, kule kijijini hamna wenzenu, walimu wanategemea mshahara tu na wakisema waende wakalime mara mvua imekuja imebeba mazao yote. Sasa hawa walimu wanaishi vipi katika mazingira hayo? Naomba tafadhali lipeni na mtupe majibu katika bajeti hii ni lini mnalipa madeni ya walimu nchi hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu walimu wa sanaa mnasema wametosha. Tangu walivyoajiriwa mwaka 2014 ajira hamna tena, lakini cha kushangaza Serikali hii hii inadahili walimu hao hao wa sanaa, wazazi maskini wanasomesha hawa watoto wao na Serikali inatoa pesa kwa ajili ya kuwapa mikopo baadhi yao lakini mnasema wametosha. Sasa kama ndiyo hivyo basi msitishe hawa walimu wa sanaa, la sivyo kwa sababu nchi hii sasa inaenda kwenye viwanda basi badilisheni mtaala, badala ya kuwapeleka kwenye ualimu muwapeleke katika masuala ya ufundi hawa wanaosoma degree, waanzishe viwanda vidogo vidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji watu wa kuanzisha viwanda vidogo vidogo na viwanda vya kati. Kwa hiyo badilisheni acheni mambo ya sanaa lakini hata mkisema walimu wanatosha, hawatoshi. Kule kijijini ratio; kwa kawaida ratio yenu ni 1:40; 1:45; 1:25. Leo nina chekechea mimi tena satellite area hakuna mwalimu lakini wanafunzi 100 chekechea, hivi kuna elimu pale? Kwa hiyo, si kwamba walimu wanatosha, lakini Serikali bado haijajipanga ni namna gani wathibitishe hiyo ratio mliyoipanga ili walimu waende wakafundishe hizo shule, hali ni mbaya kupita kiasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kukariri, jamani eee, hivi kukariri hamna, sasa kukariri hamna watoto wasichana Mama Ndalichako na wewe mwenyewe ni mwanamke watoto wasichana wasipokariri waende wakaolewe wakiwa bado wadogo? Mimi naona hiyo kukariri acheni, watoto waendelee kusoma ili wapate elimu wakue shuleni baadae hata wakitupwa huko mbali kama ataolewa yeye, atakuwa mkulima yeye, lakini hiyo kukariri achanane nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upungufu wa maabara. Somo la Baiolojia ni asilimia 51.5, Fizikia asilimia 43.5, huko vijijini huu upungufu huko vijijini kwetu hakuna walimu hao jamani. Sasa matokeo yake eti mtoto anayefundishwa private, anayefundishwa mjini, mwenye walimu, mwenye maabara anafanya mtihani mmoja na mtoto wa Mlimba. Huo ni uonevu ama si uonevu huo? (Makofi)

Mheshimiwa Waziri akija anijibu, huo si uonevu? Kwanini mnampa mtoto wa Masagati, mtoto wa Utengule, mtoto wa Mlimba anafanya mtihani mmoja na mtoto wa Dar es Salaam au wa mijini ambaye ana maabara, ana walimu ana kila kitu, huo ni uonevu, ni ubaguzi haukubaliki ndani ya nchi yetu, haikubaliki kabisa, kwa hiyo hilo naomba mliangalie, tunaoteseka ni sisi wa vijijini siyo wa mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nauliza hivi remote area zile shule za satellite yaani kwenye jimbo langu kutoka shule ya msingi mpaka kwenye kitongoji ni kilometa 20, hapa katikati kuna mito ya ajabu. Mimi leo mpaka mfuko wa jimbo nahangaika nao nawaambia wananchi jengeni madarasa mawili halafu mimi naleta bati na nimeshapeleka bati Mpande kule Kata ya Mchombe, Ijia na sehemu nyingine nyingi. Kule Tanganyika, Masagati, Lwamate mpakani na Njombe lakini walimu hamna. Vigezo mnavyoweka mjini hebu legezeni masharti na vigezo vya vijijini jamani. Haki ya Mungu unaenda unalia, watoto 200 hakuna mwalimu, mwalimu wa kujitolea, hebu nendeni mkaangalie halafu mjue mpange mipango yenu. Hamuwezi mkalinganisha… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)