Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika bajeti hii muhimu ya sekta ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa dhati kabisa kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Serikali kwa kazi nzuri wanayoifanya hususani katika sekta hii ya elimu. Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 tuliahidi kutekeleza elimu bila malipo na tumeona tangu Serikali ya Awamu ya Tano imeaingia madarakani Serikali inafanyakazi nzuri katika ahadi hii ikiwemo ruzuku ya kusaidia elimu bila malipo imetoka bilioni 19 hivi sasa imefikia bilioni 23, kwa hiyo tunaipongeza sana Serikali. (Makofi)

Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Profesa Ndalichako kwa hotuba nzuri na pia niwapongeze Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ikiongozwa na Mheshimiwa Peter Serukamba na Wajumbe wote kwa taarifa nzuri ya Kamati na ni matumaini yangu kwamba Mheshimiwa Waziri pamoja na Mheshimiwa kaka yangu Naibu Waziri Olenasha kazi nzuri mnayoifanya mkiweka taarifa nzuri ya Kamati na michango ya Wabunge nina imani kabisa tutaleta maboresho makubwa katika sekta ya elimu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, mimi nina mambo kama manne na muda ukiruhusu basi nitazungumzia mambo matano:

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianzie na suala la maslahi ya walimu nchini. Hapa Bungeni toka nimekuwa Mbunge tunakwenda mwaka wa tatu, katika kipindi cha maswali na majibu katika bajeti zilizopita tumezungumzia sana juu ya kero zilizopo kwenye maslahi ya walimu nchini, tumeona speed ya kutatua kero hizi haiendei katika speed ambayo inaridhisha. Moja ya changamoto ya speed ndogo katika kutatua kero za walimu nchini ni tatizo la muundo wa kitaasisi. Kuna mambo mengine ukiyafuatilia unaambiwa hili suala liko chini ya Afisa Utumishi wa Wilaya, ukitoka kwa Afisa Utumishi wa Wilaya wanasema hili liko Wizara ya Utumishi, ukienda Utumishi wanasema hili liko Wizara ya Afya. Niishauri Serikali, sina shida na structure ilivyo ya kitaasisi, lakini Serikali mtambue kwamba lazima muwe coordinated vizuri katika kuhakikisha mnatatua changamoto za sekta ya elimu nchini kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, kuna walimu Karagwe na nchini toka mwaka 2012 mpaka hivi sasa hawajapandishwa madaraja, kuna walimu nchini ikiwemo Karagwe walimu waliopandishwa madaraja toka mwaka 2012 mpaka hivi sasa mishahara yao haijarekebishwa ku- reflect daraja walilopandishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna walimu ambao waliondolewa madaraja lakini mpaka hivi sasa wako kwenye daraja hilo hilo, hawajui kama watakaa kwenye daraja hilo mpaka wanastaafu; kuna walimu ambao Serikali iliwahamisha kutoka shule za sekondari kwenye shule za msingi lakini mpaka hivi sasa hawajapata stahiki zao. Kule Karagwe Serikali imetoa shilingi milioni 50 lakini mahitaji halisi ni zaidi ya shilingi milioni 400, wakati Mheshimiwa Waziri ana- wind up nitake kusikia kutoka TAMISEMI na Wizara ya Utumishi na kwa sababu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Ndalichako ndiye una dhamana ya kusimamia sera ya elimu nchini tunaomba tusikie majibu ya Serikali mmeji-coordinate vipi kuhakikisha mnatatua kero za walimu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa kuzungumzia ni uwekezaji katika sekta ya elimu. Wawekezaji katika sekta ya elimu ni wabia wa Serikali na ni wasaidizi wa Serikali katika kutoa huduma ya elimu nchini. Kwa hiyo, Serikali mnatakiwa muwaangalie hawa kama partners, Serikali mnatakiwa mtambue kwamba uwekezaji katika elimu is social investment siyo business as usual. Kwa hiyo kwa kutambua hilo, Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imezungumzia vizuri changamoto hii. Nipende kuomba Mheshimiwa Waziri hii perception iliyopo kwamba kuna tag of war kati ya Serikali na sekta binafsi naomba katika winding up yako uwahakikishie wawekezaji katika sekta ya elimu na Watanzania kwamba Serikali na hawa wawekezaji mko pamoja na wote ni partner katika kutoa elimu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tax payments na non- tax payments katika sekta ya elimu ambazo wote tukitambua kwamba elimu ni social investment lazima mziondoe kwa sababu hii ni social investment siyo business as usual. Kwa mfano…

T A A R I F A . . .

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimwa Mwenyekiti, taarifa ya ndugu yangu Mwambe siipokei kwa sababu Roma haikujengwa siku moja. Kama nilivyosema kwenye utangulizi wangu toka Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani tumeona jitihada nzuri zikienda kwenye kuboresha sekta ya elimu na ndiyo maana nimesema kupitia Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na Wabunge Serikali ichukue ushauri huu ili tuzidi kuboresha sekta ya elimu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye point yangu ya tatu na jambo hili nimelisikia hata kwenye taarifa ya Kamati na mdogo wangu Mlinga amelizungumza, zuio la Serikali la wanafunzi wetu kukaririshwa mimi sijaelewa mantiki yake labda Mheshimiwa Waziri wakati una-wind up nisikie rationale ya kuzuia wanafunzi wasikaririshwe ni nini, kwa sababu ukiangalia takwimu katika ufaulu zina-alarm sana, ukiangalia division zero na four asilimia isiyopungua 60 hawaendi form five na vyuo vikuu kwa sababu wanapata division zero na four kwa vile kujifunza ni building blocks na kuna baadhi ya syllabus usipozielewa syllabus zinazofuata hutazielewa vizuri. Ukizuia wanafunzi wasikariri ili waweze kujenga maarifa na weledi mzuri kabla hawajapanda darasa lingine pia ndivyo unazidi kuchangia katika kufeli kwa wanafunzi kupata division zero na four.

Kwa hiyo, ushauri wangu Serikali mkae na wadau wa elimu muangalie jinsi ya kuliweka hili vizuri kwa sababu inabidi tuhakikishe watoto wetu tunawaandaa kufaulu lakini kuwa tayari kwa ajili ya soko la ajira pale wanapohitimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili, hii asilimia 60 au zaidi ambayo inaishia form four kwa kupata division zero na division four niishauri Serikali kuwa na mkakati maalum wa Vocational Training Institutions ziweze ku-absorb vijana wetu hawa as many as possible kwa sababu tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda, tunahitaji skill set siyo mpaka mtu awe na degree, anaweza akawa ana certificate ya ushonaji, anaweza akawa na certificate ya kutengeneza grill lakini tunawaangaliaje na tuna mkakati gani ndani ya sekta ya elimu kama Waziri mwenye sera na una-coordinate vipi na Wizara nyingine kuhakikisha kuna mkakati mahsusi ndani ya Serikali wa kuhakikisha wanafunzi wetu hawa wanaopata division zero na four wanakwenda kwenye Vocational Training Institutions na pale wanapomaliza tunahakikisha tunawapa mikopo ya bei nafuu ili na wenyewe waweze kuanza maisha na kupunguza tatizo la ajira nchini na kama mnavyofahamu vijana hawa tusipokuwa na mkakati mahsusi ndipo utakuta hata uhalifu nchini unaongezeka. Kwa hiyo, nipende kuiomba Serikali, pamoja na hili suala la zuio la kukaririsha
mliangalie vizuri. Pia muangalie hawa ambao wanaishia form four tuna mkakati gani kuhakikisha wanaenda kwenye short courses, wanapata certificate na wakishapata hizo skills tunawasaidiaje kupata mikopo ya bei nafuu ili waweze kujikimu na maisha. (Makofi)

Jambo la nne sasa niende Jimboni kwangu Karagwe. Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana nilivyokuja kwako nilikwambia kwamba Karagwe wakati naingia kama Mbunge tulikuwa hatuna hata A-Level moja, ulinisaidia sasa hivi tumejenga mabweni mawili pale Bugene Sekondari, A- Level imeanza, sasa nikuombe Mheshimiwa Waziri jiografia ya Karagwe ilivyo nimeshakuomba kwamba tusaidie tupate A-Level tatu, Nyabihonza Sekondari imezungukwa na Kata Nane ambazo hazina A-Level kuna mrundikano mkubwa sana wa wanafunzi sasa hivi Bugene Sekondari kwa sababu kwanza miundombinu bado ni michache lakini Wilaya yangu nina wananchi zaidi ya 360,000 na asilimia kubwa ya Taifa hili ni vijana.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nakuomba Bugene sekondari tusaidie ikamilike iwe full-fledged A-Level lakini wakati unafanya hivyo pia nisaidie Nyabihonza Sekondari, Nyakasimbi Sekondari na Kitundu Sekondari na zenyewe zikamilike ili ziweze kusaidia na Wilaya ya kaka yangu Mheshimiwa Innocent Bilakwate, Wilaya ya Kyerwa, Wilaya ya Ngara tuwe tuna A-Level ambazo zitakuwa zinasaidia hii elimu bila malipo ambayo Serikali imeanzisha, wale watoto wakienda sekondari tuwe tuna A-Level ndani ya Mkoa ambazo zitasaidia kuandaa Taifa la kesho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, point ya mwisho ni Sheria ya Elimu Namba 25…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)