Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Pascal Yohana Haonga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbozi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, lakini kabla sijaendelea, naomba nitoe pole kwa familia ya Mheshimiwa Sugu ambaye yuko ndani kwa sababu ya uonevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa pole hiyo, pia akitoka Mheshimiwa Sugu nitakuja kumpa pongezi kwa sababu tunajua hata Mandela naye amewahi kupitia hatua kama hiyo na naamini kwamba yeye ndio atakuwa Mandela wa Tanzania huko mbeleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nianze kuchangia Wizara hii ya Mambo ya ndani na naomba nianze na kusoma Ibara ya (14) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. “Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa sheria.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumetokea mauaji yanayofanywa na baadhi ya Maaskari wetu, Maaskari ambao tumewasomesha kwa kodi zetu, Maaskari ambao hatujui kitu gani, either kwa maagizo kama wanavyosema yametoka juu. Mauaji haya yanasikitisha sana na yanavunja Ibara ya (14) Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dada yangu, Mheshimiwa Anatropia amezungumza vizuri sana. Ameuawa ndugu yetu Suguta Chacha Heche; amekamatwa, amepigwa pingu, anachomwa kisu na Askari. Inasikitisha sana na inatia huzuni sana. Ameuawa Aqualina, lakini kuna Maaskari walikamatwa kama sita hivi. Hao Maaskari wako wapi? Leo anakuja DPP anasema kwamba hao Maaskari; yaani leo tunaambiwa kwamba hilo shauri limeshafungwa wakati Maaskari sita walikuwa wamekamatwa tangu awali, hatujui Maaskari hao wamepelekwa wapi; na hatujui kesi imekuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanampongeza Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya ndani, Mheshimiwa Comredi Mwigulu Nchemba. Nimwambie ukweli wanaompongeza wanamharibu na wanaompongeza hawamtakii mema. Namshauri jambo moja tu, kujiuzulu Uwaziri wa Mambo ya Ndani. Namshauri pia IGP pia aweze kujiuzulu. Siyo dhambi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikumbushe kitu kimoja. Kuna watu hawakumbuki historia ya Taifa letu. Mheshimiwa Mwinyi, Rais Mstaafu amewahi kujiuzulu miaka ya 70 kwa sababu ya wale wafungwa kule Shinyanga walifariki gerezani akajiuzulu na baadaye akaja kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kujiuzulu haimaanishi kwamba wewe umetenda dhambi, lakini watu wa chini yako maana yake hawaendi sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu mwingine inaitwa Meja Jenerali Abddallah Said Natepe, ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Alijiuzulu kwa sababu kuna watu walikuwa Magerezani, walikuwa wanatuhumiwa; walifungwa kwa kesi ya uhaini, wakatoroka. Walipotoroka, akaamua kujiuzulu kulinda heshima yake, lakini pia kuchukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mheshimiwa Comredi Mwigulu Nchemba amekaa hapo kwenye kiti hicho, sikutegemea kama angeweza kuwepo hata dakika tano hadi sasa kwa sababu kilichotokea kwenye Wizara yake ni madudu; ni takataka. Anachong’ang’ania sijajua ni kitu gani!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu leo kama kuna watu wanauawa, kuna watu leo wanatekwa, kuna watu wamepotea kwenye nchi hii, Beni Saanane hatui yuko wapi hadi leo, ni mwaka mmoja na nusu; Azori Gwanda. Nasi hatuwatetei CHADEMA tu, tunawatetea na wengine. Azori Gwanda alikuwa ni Mwandishi wa Habari. Yule Diwani wa Kibondo kule alikuwa ni mtu wa CCM. Sisi tunawatetea wote ndugu zangu, hatuwatetei CHADEMA tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba hiyo nafasi, hicho kiatu kimempwaya. Nadhani angeweza kuondoka kwa sababu nafasi haiwezi hata kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua yeye alikuwa ni miongoni mwa watia nia kwenye Chama chake kwa nafasi ya Urais, nadhani ndoto za Urais zitakuwa zimeshaanza kuota mbawa kwa sababu madudu aliyofanya kwenye Wizara hii hayajawahi kufanywa hata mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye hoja nyingine. Leo Magereza zinajaa, Mahabusu wako Magerezani, wafungwa wako Magerezani, siyo kwa sababu labda uovu umeongezeka.

Hapana ni kwa sababu kulikuwa na uonevu wa hali ya juu sana. Mheshimiwa Mwenyekiti, leo watu wanaonewa. Mheshimiwa Sugu kawekwa ndani kwa sababu ana uhuru wa kutoa maoni, ametoa maoni yake, leo amefungwa ndani miezi mitano. Uonevu wa namna hiyo hauwezi kuvumilika hata kidogo.