Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Alfredina Apolinary Kahigi

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. ALFREDINA A. KAHIGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniamsha siku ya leo nikiwa mzima wa afya na kuweza kuchangia hotuba ya Wizara ya Ulinzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru wewe mwenyewe kwa kunipa nafasi ya kuweza kuongea. Namshukuru Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Naibu wake kwa hotuba nzuri ambayo ametusomea hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nitachangia mambo machache katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wizara hii nimeona kuna changamoto ambazo napaswa kuziongelea kama mbili/tatu hivi. Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii, kuna tatizo la upotevu wa watu wazima na watoto wadogo katika nchi yetu. Nchi yetu ilikuwa kweli ni ya amani na utulivu lakini hili janga ambalo limejitokeza kwa sasa hivi linatutia simanzi kubwa sana, linatuaibisha, sijui ni watu gani ambao wanataka kutuchafulia amani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri pamoja na Jeshi lake la Polisi suala hili walifanyie kazi kwa hali ya juu sana maana sasa hivi watu hatuna amani, tuna watoto wakienda shuleni tunakuwa na wasiwasi watatekwa, watauawa kwa sababu ya watu waovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika sana Serikali yangu maana ndiyo mnaobeba huu msalaba. Kuna watu wengine wanajipenyeza wenye nia mbaya ya kuchafua jina la nchi yetu ili mwonekane ni wabaya kumbe wakati mwingine Serikali haina ubaya wowote. Naomba Waziri alifanyie kazi kweli kweli suala hili. Sina ubaya wowote na Serikali yangu, sina ubaya wowote na maaskari lakini inasikitisha, walifanyie kazi. Hiyo ni namba moja kwa sababu dakika ni kidogo nitaongea kidogo kidogo kusudi niweze kueleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye suala la Polisi. Maaskari sina ugomvi nao, nawapenda sana na wao wanipende sana lakini maaskari jamani wajirekebishe. Kuna matrafiki, huko njiani wanasumbua sana hasa hawa wa PT. Kuna makosa mengine ni madogo madogo mnaweza mkaongea, lakini wanakupiga faini, wanatusumbua yaani sasa vyombo vya moto inaonekana kama hatuna amani navyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na lenyewe hilo waliangalie, wawaambie hao maaskari waache kusumbua watu, hasa wa bodaboda wanawasumbua sana na wakati mwingine na kuwapiga wanawapiga. Kwa kweli haki za binadamu zinavunjwa na maaskari wakorofi ambao wanafanya vitu ambavyo hawakuagizwa kuvifanya waache. Waheshimiwa Wabunge, wanaviona vitu vingine sisemi kwamba ni mimi hapa mama Kahigi, hapana, wanafanya mambo ya namna hiyo, yanatuudhi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo nakuja upande wa nyumba za maaskari. Nyumba za maaskari zinasikitisha sana kwani zimepitwa na wakati. Nyumba za mabati utadhani maaskari wetu ni bata au kuku kulala kwenye nyumba mbovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba tumeambiwa wanajengewa nyumba 400 ni kidogo sana, naomba wakaze buti, wawajengee nyumba, wakae katika nyumba nzuri na wawe na maisha mazuri na familia zao wajisikie kama vile ambavyo sisi tunavyojisikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka katika hilo, nafikiri wamenisikia, watawashughulikia, nakuja kwenye maslahi yao. Maaskari wengine wanaongezwa vyeo lakini mshahara hawaongezwi. Naomba na lenyewe hilo waliangalie, wawaongeze mshahara ili wafanye kazi zao wakiwa na mioyo safi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoka hapo nakuja kwenye suala la passport. Kwa kweli passport ni kitu kizuri sana lakini kiasi ambacho wameweka kwa wananchi wetu wa vijijini nina wasiwasi hawataweza kulipia hizo passport. Kulipia Sh.150,000 ni labda kwa Wabunge na watu wenye vyeo vya hali ya juu ndiyo watakaoweza. Naomba wapunguze gharama hiyo ili watu wetu waweze kuwa na passport. Mtu mwingine anapata safari ya kwenda nchi za nje lakini passport inamkwamisha anashindwa kwenda kwa sababu hana hela ya kuweza kulipia hiyo passport. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nako natoka, la mwisho ni kuhusu kesi kukaa muda mrefu. Naomba upelelezi uwe unafanyika haraka sana, wasifanye kukawa na mrundikano wa kesi, wafanye haraka haraka, kesi ziende mahakamani watu waweze kuhukumiwa, mambo yaende sawasawa sio watu kuwazungushazungusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.