Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Yussuf Salim Hussein

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chambani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, Bismillah Rahman Rahim.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na leo nilikuwa nichangie kwa ukali sana, lakini Mheshimiwa Waziri ashukuru kwamba hotuba yake imekuja katika siku Tukufu na katika siku ya leo sisi Waislam huwa tunahusiana uusi kum ibada-Allah wanafsi-bitaquwa-Allah. Kwa hiyo, nitamshauri zaidi kuliko kwenda katika yale mambo ambayo nilikuwa nimeyapanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza sana katika nchi yetu kuhusu kuporomoka kwa maadili. Maadili yanaporomokaje? Vijana wetu tunasema hawana maadili, nyimbo hazina maadili, michezo haina maadili; sasa nani hana maadili? Ni sisi wenyewe ndio hatuna maadili. Hatuna kwa sababu gani? Kwa sababu tumekubali kuwa watumwa tukaacha mila na utamaduni wetu na tukaiga mila nyingine. Mheshimiwa Waziri pale kila siku anaenda na nyimbo za kizazi kipya, sijui nini, lakini hujamsikia akihamasisha ngoma za asili au tamaduni zetu za kiasili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakati wa ngoma zile jando na unyago, misondo, akinamama wanavunja ungo wanawekewa ngoma, wanafundishwa, pale ndiyo tunafundishwa maadili. Leo katika hao wasanii wa kizazi kipya, ukimwondoa Mr Ebbo ni nani anavaa kivazi cha asili cha Mtanzania kuitangaza Tanzania yetu? Hakuna. Wote wanaiga. Ni suruali chini ya matako, anajishika hapa, anajikunjakunja; kwa nini tusiende katika mila na destuli zetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri ahamasishe ngoma zetu za asili ili vijana wetu angalau wajue mila na desturi na asili yao. Leo humu ndani ya Bunge ukiondoa katika hawa watoto wangu, ukimwondoa Mheshimiwa Mtemi Chenge, ukimwondoa Mheshimiwa Musukuma labda na Mheshimiwa Ndassa, ni Mnyamwezi gani anayeweza kucheza Lizombe humu? Mheshimiwa Kigwangalla hawezi.

TAARIFA . . .

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana shemeji yangu. Napokea taarifa yake. Mwenyezi Mungu amweke Mr. Ebbo mahali panapostahili kwa kazi yake aliyoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, turudi katika mila na desturi zetu. Hata utalii tunapoutangaza huko nje, tunapotumia mila na desturi zetu, basi watalii wanavutika zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa katika utalii. Wageni wanapokuja, tunapowawekea ngoma za kiasili wanafurahi zaidi, wanacheza na mpaka wanakwambia sasa tutafutie tena utuwekee. Wanapenda mchezo wa ng’ombe, wanapenda ngoma za kiasili, lakini leo sisi tumeingia katika kizazi tu hiki. Sasa unasema maadili yamepotoka, ni sisi wenyewe ndiyo tunayapotoa. Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kila mwanamichezo hapa amelalamika kwamba michezo inakufa, tunapeleka watu haturudi na medali, tunarudi na aibu, tunatoka kwa shangwe, tunarudi na msiba; ndiyo. Kwa sababu wanamichezo wazuri walikuwa wanapatikana mashuleni. Leo katika shule hakuna huo utamaduni wa hii michezo kuendelezwa, ikafika kipindi ikafungiwa kabisa ikawa haipo, mara inarudishwa. Kwa hiyo, hatujui tunafanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la michezo katika mashule jamani, michezo ni afya. Watoto wanapocheza, utakuta wale watoto wanaofanya michezo mashuleni ndiyo wanakuwa active vilevile katika masomo. Kwa hiyo, pale ndiyo sehemu ambapo tunajenga michezo, lakini ndiyo sehemu ambapo tunapata vipaji. Sasa hapo Mheshimiwa Waziri ukishapata kutoka shuleni: Je, una vyuo vya kuwapeleka na kuwaendeleza? Hili nalo ni swali ambalo Mheshimiwa Waziri aliweke katika kichwa chake, leo nimemwambia na namsaidia tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, limezungumzwa sana, Mheshimiwa Waziri anafungia nyimbo, lakini nyimbo inafungiwa baada ya kuwa imeshatoka baada ya mwaka mmoja, mwaka mmoja na nusu au miezi sita. Tayari kile kibaya ambacho unakiona wewe kipo pale anakifungia kimeshakwenda huko katika Jamii. Sasa kwa niniaunafungia nyimbo? Mimi sijui labda atanisaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nilipokuwa shuleni nilikuwa msanii vilevile. Nilikuwa siendi hewani mpaka kuna Board of Sensor inapita, inasikiliza kile ambacho nitakipeleka hewani na panafanywa marekebisho; aah, hili ondoa, hili peleka, hili fanya hivi. Nikimaliza wanarudi tena ndiyo unaruhusiwa sasa kutoka hewani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo anakwenda kumfungia msanii ameshapata gharama, nyimbo imeshatoka, kama ni maadili yamepotoka, ndiyo leo anakuja kuifungia nyimbo wakati ujumbe umeshatoka? Sasa Mheshimiwa Waziri katika hili naomba hizi Board of Sensors ziwe zinafanya kazi zake kabla ya wimbo kutoka kama ni mavazi, kama ni maneno yenyewe yaliyotumika, kama ni kitu gani, kifanyike kwanza. Sasa unakuja kufunga banda, farasi ameshatoka, sijui unafanya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, anafungia magazeti, redio; sasa hivi vitu kwetu ni vipya. Hapa ilikuwa magazeti ni ya Serikali tu, Redio ni za Serikali tu, hata hiyo television yenyewe ilikuwa hakuna, alikuwanayo Mwalimu pekee, anaangalia, kesho anakwambia nimeota Urusi kuna vita. Sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi vitu Mheshimiwa Waziri anatakiwa avilee. Sasa wakati anavilea hivi vitu anatakiwa aweke utaratibu, havikuwa katika tamaduni zetu. Sasa kama havikuwa katika tamaduni zetu, ni kitu kipya, lazima Mheshimiwa Waziri akae, atulie, aone namna gani atakwenda navyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni changamoto ambazo zitakuwepo nyingi kwa sababu vyombo vilikuwa vinamilikiwa na Serikali, leo watu binafsi wanamiliki vyombo, kila mmoja ana mtazamo wake, ana fikira yake, unaona? Kwa hiyo, Waziri ambaye anasimamia hili anatakiwa avilee. Sasa leo Mheshimiwa Waziri mwenyewe amegeuka kama kuku mvia; anataga yai lake, halafu analila mwenyewe. Sijui tunakwenda wapi? (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kingine ambacho kimetokea hapa, kimezungumzwa na wachangiaji baadhi hapa kwamba Waandishi wa Habari wanapotea; Serikali haitoi taarifa yoyote. Sasa akitokea mtu na mtandao wake, akatoa taarifa, hata kama ni ya upotoshaji, hiyo ndiyo itaaminika, kwa sababu wewe kama Waziri hujafanya kazi yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namshauri kwamba linapotokea tatizo kama hilo, wakati hao ni watu wake, tuwahi kutoa taarifa hii. Sasa taarifa nyingine itakayokuja itakuwa hiyo sasa ni ya upotoshaji au Serikali imeshasema, lakini kama Mheshimiwa Waziri ananyamaza, akitokea mwingine akisema, anakwenda kusema huyo ni mchochezi, huyo fisadi, huyo hivi; nani hakufanya kazi yake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri Mheshimiwa Waziri atoe taarifa kwa wakati. Waandishi wa Habari wanapotea na Waandishi wa Habari hawa, kusema na kuandika ndiyo kazi yao. lazima watasema! Sasa wakisema sivyo, kosa siyo lao, kosa ni lako ambaye hukutoa taarifa kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kingine ambacho nataka kukizungumza cha mwisho kuhusu mapato ya TFF na ZFA. Kuna mgao ambao huwa TFF inapata kila mwaka kutoka FIFA. Zanzibar ukiondoa kiwanja cha Gombani kuwekewa nyasi tokea kuanzishwa haya, ikaondolewa Zanzibar, inategemea TFF haijawahi kupata mgao mwingine. Kwa hiyo, hizi pesa zinakwenda wapi? Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tunalotaka kujua, hapo zamani tulikuwa tunapata Dola laki 2.5 kwa mwaka kutoka FIFA, lakini hapo katikati hizi pesa wakazizuia, wakawa hawazileti kwa sababu ya mambo yaliyojitokeza hapo, ufisadi, accounts zenyewe haziko sawa na kadhalika, kwa hiyo, hizi pesa zikazuiwa. Je, hizo pesa zimeanza kurudi? Sasa zimefikia hiyo laki 7.5 tunayoambiwa au vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo yote yanatakiwa kuwekwa wazi. Mheshimiwa Waziri atakapoweka wazi; atakapozungumza haya mambo kwa wakati, hawezi kusikia malalamiko. Hata yakitoka yale malalamiko, itakuwa tayari Mheshimiwa Waziri ameshayasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, leo nimezungumza kwa upole sana na Mheshimiwa Waziri kumwonesha namna gani aweze kufanya kazi vizuri katika hii Wizara. Hii Wizara inaonekana kama ni Wizara tu hivi nyepesi nyepesi na nini, lakini Wizara hii ndiyo inabeba maisha yetu. Kinapopotea kizazi chetu, inapotoka taarifa ya upotoshaji, inaweza ikaligharimu Taifa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)