Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Ezekiel Magolyo Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba na mimi nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwanza kuwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Msalala kwa kunirudisha hapa kwa mara nyingine kwa kura nyingi. Imani yao kwangu nina uhakika italipa kwa sababu uwezo wa kuyatimiza niliyowaahidi kwa kushirikiana na Serikali hii ambayo iko vizuri sana ninaamini kwamba ninao.
Mheshimiwa Spika, naomba kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa ushindi mkubwa alioupata, lakini kipekee nimpongeze sana kwa hatua ambazo ameanza kuzichukua katika kurekebisha hali ya maisha ya Watanzania kupitia mpango wake wa kusaidia kwenye mambo mengi kama ambavyo amekuwa akiahidi.
Mheshimiwa Spika, Mheshiwa Rais, alituomba Watanzania tumuombee na mimi naomba kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba nimeweka mpango wa kuwa ninafunga angalau mara moja kila mwezi kwa ajili ya kumwombea Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yake. Katika kumuombea nitakuwa pia nikimsaidia kupitia Serikali yake kuainisha maeneo ambayo majipu yapo katika hatua nzuri ili yaweze kushughulikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba yake Mheshimiwa Rais aliainisha mambo mengi lakini ukurasa wa nane alisema ifuatavyo naomba ninukuu kwamba; “Suala la madini nalo limelalamikiwa, wanalalamika wenyeji kutofaidika, vilio vya wachimbaji wadogo wadogo kutengewa maeneo ya uchimbaji na kupatiwa mikopo, kutolipa kodi stahiki, usumbufu wa kulipa fidia na kadhalika.”
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa leo naomba nijikite kwenye hili eneo, Wilaya ya Kahama tuna migodi miwili, Mgodi wa Bulyanhulu na Mgodi wa Buzwagi. Eneo hili ni chanzo kikubwa sana cha mapato kwa Serikali na ni chanzo kikubwa cha mapato kwa wananchi ambao wanazunguka migodi hiyo. Tumekuwa tukilalamika kila wakati, niipongeze Serikali ya awamu iliyopita ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa hatua ambazo ilichukua kurekebisha mikataba. Itakumbukwa aliunda Tume iliyoongozwa na Jaji Mark Bomani, mimi na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge akiwemo Mheshimiwa Waziri Mwakyembe tulikuwa Wajumbe na kupitia Tume hiyo kulifanyika mabadiliko kadhaa ambayo yamepelekea kuongezeka kwa mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba niiombe Serikali, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Pofesa Muhongo kwa hatua ambazo ameanza kuchukua kutusaidia kwenye eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukilalamika kwamba wananchi wa maeneo ya migodi hatunufaiki na madini, kwanza kwa sababu migodi hii hailipi kodi sawasawa kwenye Halmashauri, lakini pili, procurement zake nyingi wamekuwa wakinunua vifaa vingi kutoka maeneo ya mbali ya migodi na mbaya zaidi miradi ya ujirani mwema, wamekuwa wakichangia kidogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka mwaka 2014 Mheshimiwa Profesa Muhongo alisimamia mazungumzo baina ya Mgodi na Serikali kwa upande mmoja lakini na sisi wananchi wa maeneo jirani hatimaye Mgodi wa Bulyanhulu, Buzwagi na mingine wakakubali kuanza kulipa ushuru wa huduma kwa Halmashauri kwa asilimia 0.3. Hatua hiyo imesaidia kuongeza mapato ya Halmashauri lakini kama ambavyo Mheshimiwa Waziri utakumbuka katika mazungumzo yale tulikufahamisha, tunaomba uendelee kutusaidia. Hawa jamaa ni jeuri, na utakumbuka katika mazungumzo kuna baadhi ya mambo waliyakubali lakini utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua kwa mfano walisema watakuwa wanalipa hiyo service levy kila robo mwaka, sasa hivi inafika mpaka nusu mwaka hawajalipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini baya zaidi, tulisema kwamba kwa mfano Mgodi wa wa Bulyanhulu umeanza uzalishaji mwaka 2000 na toka wakati huo hawajawahi kuzalisha dhahabu ya chini ya thamani ya dola za Kimarekani milioni 500, ukipiga hesabu ya asilimia 0.3 ya dola milioni 500 ni fedha nyingi sana. Kwa hesabu nilizofanya Halmashauri ya Wilaya ya Msasala inapaswa katika kipindi hicho cha miaka 15 iwe imelipwa kutoka Mgodi wa Bulyanhulu dola za Kimarekani zisizopungua milioni 13 hivi sasa wanatulipa milioni 700, milioni 600 ambazo ni kidogo kuliko tunavyotaka.
Mheshimiwa Waziri, naiomba Serikali kusaidia kama ambavyo tulikuwa tumeanzia, mtusaidie tulipwe madeni yetu dola milioni 12 tunazodai Mgodi wa Bulyanhulu ambayo ni 0.3% kutoa dola 200,000 ambazo wamekua wakilipa, ile difference ile toka mwaka 2000 ni karibu dola milioni 12, fedha hizo zikilipwa ninaamini kwamba maisha ya wananchi yataboreka sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, naomba nimwombe Waziri atusaidie sana katika utekelezaji wa miradi ya ujirani mwema hawa watu wamekuwa hawana imani na Taasisi za Serikali, wamekuwa wakiitekeleza wao wenyewe na kwa mara nyingi wamekuwa wakitekeleza miradi kwa gharama kubwa, kwa mfano, wametujengea kituo cha afya pale Bugalama kwa thamani ya shilingi milioni 850.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha zile zingetolewa kwenye Halmashauri, tukajenga sisi kama ambavyo tunajenga miradi mingine milioni 850 tungemaliza kujenga angalau majengo mengi zaidi yenye uwezo wa ku-accomodate hata huduma za kihospitali yenye hadhi ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba, Mheshimiwa Waziri atusaidie mazungumzo ambayo bado yanaendelea kati yetu na wawekezaji hawa waweze kuziamini Taasisi za Serikali, waiamini Halmshauri ili wanapotekeleza miradi ya ujirani mwema kwa kiasi kikubwa itekelezwe kwa modality ambayo Halmashauri yenyewe itasimamia, na kwa kufanya hivyo tutaweza kupata value for money.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hivi tatizo la sheria ya manunuzi ambalo tunalilalamikia Serikali, kule mgodini ndiyo liko kubwa zaidi, kwa sababu unakuta shule ambayo ingeweza kujengwa kwa milioni 50, milioni 80, wao wanasema wamejenga kwa milioni 300, milioni 400. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo katika mazunguzo hayo tumekuwa na kilio cha wananchi waliondolewa kwenye eneo la Mgodi wa Bulyanhulu mwaka 1996. Waliondolewa bila fidia, tumefanya mazungumzo haya kupitia awamu iliyopita na Mawaziri kadhaa, Profesa Muhongo ulianza kuchukua hatua nzuri za kukaa chini kuzungumza na hawa watu niombe katika mazungumzo ambayo umekua nayo, na nipongeze sana jitihada ambazo umekuwa ukizifanya na nimshukuru Mungu kwa kurudishwa kwenye hii Wizara. Kwa sababu institutional memory imekuwepo, haya ninayoyasema unayajua, naamini kwamba utatusaidia tuzungumze waweze kulipa fidia kwa wananchi waliokuwa waki-occupy lile eneo ambao waliondolewa mwaka 1996 bila fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa dakika chache zilizobaki naomba Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi anisikilize vizuri. Kuna tatizo la Mwakata tulipata maafa tarehe 3 Machi, mwaka jana watu 47 wakafa, wananchi kaya zaidi ya 650 zikakosa makazi, Waziri Mkuu akaja, Rais akaja, na mkaahidi kwamba mngesaidia kujenga nyumba mia tatu na kitu. Mpaka leo hii wale watu wanaishi kwenye maturubai, hizi mvua zinazonyesha zinawanyeshea, ni kitu ambacho hakiaminiki kabisa kwa sababu Serikali ilikuwa inaahidi na kwamba tulitegemea jambo hili lingetekelezwa kwa dharura katika kipindi cha mwezi mmoja, miwili na ndiyo maana ya kuwapa maturubai.
Leo, wale watu wanakaa kama wakambizi, nyumba zilizojengwa ni tatu ambazo zimetoka kwa wafadhili wa Mgodi wa Bulyanhulu pamoja na wafadhili wengine. Msaada au ahadi iliyotolewa na Rais kwamba nyumba zile zingejengwa hakuna kilichofanyika hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kasi ambayo Mheshimiwa Rais anayo, ninaomba sana Mheshimiwa Jenista, baada ya hapa hatua inayofuata ni kufuatana na mimi tena twende mapema iwezekanavyo. Twende pale Mwakata, eeh Mheshimiwa Mwamoto anasema na yeye awepo kwenye msafara huo, twende Mwakata ukawaeleze wananchi ni nini na lini nyumba hizo zitajengwa. Wale wananchi wanaishi maisha ya kisikitisha sana kwa sababu hawana nyumba na wanamatumaini ya kujengewa nyumba na Serikali yao, na ninaamini Serikali yetu sikivu itaweza kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la mwisho, ni ahadi ya kupeleka maji kwenye Mji mdogo wa Isaka pamoja na Mji mdogo wa Kagongwa na baadae yaende hadi Tinde. Hii ni ahadi iliyotolewa na Serikali iliyopita toka mwaka 2008, najua limekuwepo tatizo la fedha lakini tumekuwa tukiahidiwa kila wakati nakumbuka kwenye Bunge lililopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, nitazungumza tena siku nyingine. (Makofi)