Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anaozifanya pamoja na Mawaziri wote; Waziri Mkuu, Waziri mwenye dhamana na Naibu Mawaziri wa Wizara hii ambayo tunachangia pamoja na Makatibu wake na wote wanaomsaidia katika Wizara hii. Kazi zinazofanyika tunaziona, ni nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende sasa kwenye Jimbo langu la Halmashauri ya Mji wa Makambako. Pale Makambako kuna eneo fulani panaitwa Idofi ambapo Wizara walikuwa wamesema tuandae kwa ajili ya kujenga One Stop Centre na eneo hili kazi iliyofanyika kuwaomba wananchi wale ni kazi kubwa, ngumu na ambayo mpaka sasa hatuelewi nini kinachoendelea na kwa sababu bado hawajalipwa fidia na kwenye kitabu nilikuwa naangalia sioni mahali ambapo panaonyesha utayari wa kujenga one stop center kwa ajili ya manufaa ya watu wa Makambako, ombi langu niombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapo atueleze One Stop Center ipo au haipo. Na kwa sababu pana msongamano sana wa magari na nini pale, wenyewe mnaona mnapokwenda Songea, Mbeya, pana msongamano mkubwa sana wa jam ya magari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili; niishukuru tena Serikali kwa namna ambavyo imetenga bajeti kwa ajili ya kutengeneza kilometa sita za Mji wa Makambako ambazo Mheshimiwa Rais aliahidi na sasa naziona hapa, nawapongeza sana na shughuli hiyo nimeiona pale sasa imeshaanza kwa mita 150, najua kwamba sasa wakati mkandarasi anaendelea na bajeti hii itakuwa imeshafika muda wake mtaendelea kuikamilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna barabara ambayo ni ya TANROADS, unapokwenda Songea road pana Kijiji kinaitwa Ilunda, kutoka Ilunda kwenda Igongolo pana kilometa tisa ambazo ni za TANROADS, ukiendelea mbele barabara hii mbele inaendelea inakwenda Ilengititu, inakwenda Kifumbe, Mahongole inakuja kutokea Makambako na utaona sasa barabara hii kwa kilometa tisa ambazo zimetengenezwa pale barabara mbele inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu ni kwamba barabara hii sasa iingizwe kwa TANROADS ili kusudi kwa mzunguko huu pale ni kilometa 19, ili mzunguko wa barabara kwenda kutokea Makambako uweze kuwa mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima niipongeze tena Serikali kwa barabara ya kutoka Nyigu kwenda Igawa ambayo inapita pale kwangu Makambako, kazi inayofanyika ni nzuri sana. Ombi langu ni kwamba zile barabara za pembeni na zenyewe, naona wanaendelea, basi nina imani kwamba mtakamilisha vizuri kama ambavyo iko ile waliyokamilisha pale Mafinga.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze tena barabara ya kutoka Makambako kwenda Songea ambayo nimeiona iko kwenye bajeti. Ombi langu kwa Wizara, barabara hii kwenda Songea ukitoka Makambako kwenda Njombe vichepu vya basi kipo kimoja tu kiko pale Mtwango, utaona hakuna mahali ambako mabasi yanaweza kusimama na nyumba zimejaa kutoka Makambako mpaka Njombe. Ombi, muone namna ya kupanua mabega ili kuwe na vituo vya basi kwa ajili ya barabara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye mawasiliano, katika mawasiliano kutoka…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba dakika moja tu, kuna jambo muhimu. Nije kwenye suala ambalo Rais analifanya, Mheshimiwa Rais wetu amekaa hapa ndani kwa miaka 20 akisikiliza hoja mbalimbali ambazo zilikuwa zinasemwa pande zote mbili. Hoja hizo sasa ndiyo zinatekelezwa.