Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Anastazia James Wambura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika bajeti hii muhimu. Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia neema zote katika maisha yangu. Vilevile nimpongeze sana Waziri Mheshimiwa Mbarawa pamoja na Naibu Mawaziri wake, Makatibu Wakuu pamoja na timu yote ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kazi nzuri ambayo wanafanya katika Wizara hii muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue pia nafasi hii kuipongeza sana Serikali yetu ya Awamu ya Tano, Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kuvunja rekodi ya bajeti ya Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi kwa sababu imetenga shilingi trilioni 4.2, ni kitu ambacho hakijawahi kutokea, hongera sana Serikali. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa ajili ya kuruhusu kazi ifanyike katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuunga mkono hoja kwa asilimia 100. Naunga mkono hoja ili fedha hii ambayo imetengwa iweze kutoka kazi iende kufanyika katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa Mkoa wetu wa Mtwara katika fedha hizi ambazo zimetengwa imepata zaidi ya shilingi bilioni 42. Nichukue nafasi hii kwa niaba ya wana Mtwara kushukuru sana Serikali kwa sababu fedha hizi zinakwenda kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Mkoa wa Mtwara takribani shilingi bilioni 12.8 na shilingi bilioni 10 kwenye ujenzi wa barabara yetu ya uchumi ya Mtwara – Tandahimba - Newala - Masasi na nyingine zilizobaki zinakwenda kufanya matengenezo ya barabara za mkoa na barabara kuu za lami pamoja na zile za changarawe. Pamoja na hayo pia fedha hii inakwenda kutengeneza madaraja, kutengeneza maeneo korofi na kazi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inatia faraja kwamba fedha hizi siyo kwamba zinakwenda Mtwara tu, kuna fedha kiasi tofauti kinakwenda katika mikoa mingine. Kwa mfano, nichukulie katika utengenezaji wa viwanja vya ndege utaona kuna fedha zinakwenda kutengeneza Kiwanja cha Kigoma, Mpanda, Tabora, Songwe, Mwanza, Arusha, Mtwara ipo pia, Sumbawanga, Shinyanga, Kilimanjaro, Geita, Iringa, Musoma, Songea, Dodoma, Tanga, Manyara, Lindi, Simiyu, ni maeneo mengi tu fedha inakwenda kutengeneza viwanja vyetu vya ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, naomba ninukuu maneno ya wanafalsafa ambao wanasema kwamba, everything will be okay in the end. If it’s not okay, it’s not the end. Kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Mbarawa asonge mbele, kwa sababu huu siyo mwisho wa kazi mwaka ujao naamini kabisa wataendelea katika maeneo mengine.

Pamoja na hayo niombe kutoa kilio cha wana Mtwara katika eneo la barabara ya Mtwara – Tandahimba - Newala - Masasi. Mwaka uliopita tuliambiwa kwamba kiasi ambacho kimetengenezwa pale ni asilimia 16 ya kilometa 50 ambalo ni eneo la Mtwara Mnivata. Sasa asilimia 16 ukiangalia itakuwa ni kama kilometa 8 lakini mwaka huu tuna shilingi bilioni 10 za matengenezo ya kipande hicho hicho. Kwa hiyo, ukichukua zile kilometa 200 kuna maeneo mengine tunaambiwa ni kilometa 209 lakini document zingine tunaambiwa ni 221 ni kwamba tunaweza tukachukua miaka mingi sana kumaliza eneo hili. Kwa hiyo, niombe mwaka ujao Wizara iangalie uwezekano wa kuongeza kasi ya matengenezo ya barabara hii kwa sababu ni muhimu sana katika uchumi wa nchi yetu lakini kwa wakulima wa Mtwara kwa sababu mara nyingi unapopita…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)