Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Mendard Lutengano Kigola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na pongezi, Serikali inafanya vizuri sana. Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Mawaziri wanafanya kazi vizuri sana. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe ushauri kidogo. Kila mwaka tunasoma hiki kitabu, bahati nzuri kitabu kinaandikwa vizuri sana, lakini kuna barabara ambazo zinafanyiwa upembuzi yakinifu kila mwaka na kuna barabara nyingine zimeshafanyiwa upembuzi yakinifu, imeshapita hata miaka mitatu, minne lakini ujenzi bado haujaanza. Nataka niishauri Serikali, kwa barabara zile ambazo zimeshafanyiwa upembuzi yakinifu, naomba zianze kujengwa sasa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, barabara ile ya Mafinga mpaka Mgololo, barabara ya Nyololo mpaka pale Mtwango, upembuzi yakinifu ulishafanyika toka mwaka 2013, ulishakamilika. Kwa hiyo, ujenzi bado. Mheshimiwa Waziri, naomba hiyo barabara kwa sababu Serikali iliahidi kwamba itajenga kiwango cha lami na ukizingatia kule kuna viwanda vingi sana, naomba ianzwe kujengwa kwa kiwango cha lami kama ilivyokuwa imeahidiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara moja kubwa ambayo inatoka Mafinga kwenda Igawa, naishukuru sana Serikali imeanza kuitengeneza barabara hiyo vizuri sana.

Naiomba Serikali, ile barabara kuna sehemu naweza nikasema inapita kwenye vijiji vikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, pale Nyololo pana wafanyabiashara wengi sana, wanafanya biashara kuanzia asubuhi mpaka usiku. Sasa naomba wakitengeneza pale, ile barabara iwe pana halafu itengenezwe kama stendi, halafu ziwekwe na taa za barabarani kwa sababu pale pana wafanyabiashara wengi sana, itawasaidia sana wafanyabiashara wa pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu naiomba tena Serikali kwa barabara hiyo hiyo, nadhani hata Mheshimiwa Rais atakuja kuifungua ile barabara. Pia pale Mbalamaziwa ni sawa na Nyololo, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri pale Mbalamaziwa basi patengenezwe stendi kubwa ambayo iko ndani ya barabara ili magari makubwa yanapopaki pale ajali zipungue, kwani kuna ajali huwa zinatokea mara nyingi sana. Kwa hiyo, naomba stendi ziimarishwe, zitengenezwe vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sehemu nyingine kuna vijiji vinaingia kwenye barabara, sasa kuna stendi ndogo; naomba na zile stendi ndogo basi zioneshwe vizuri ili tuhakikishe kwamba kwenye stendi ndogo ili kupunguza ajali, basi tupanue zile barabara ziwe pana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo la Mufindi Kusini kuna barabara ambazo ni za TANROADS. Zile barabara kwa kweli Serikali inatengeneza vizuri sana na ukizingatia kule Mufindi tuna mvua nyingi na tunaenda kwa kalenda; kuanzia mwezi wa Sita huu mpaka mwezi wa 12 barabara ndiyo zinatengenezwa. Sasa naomba ile bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 ambayo inaishia, naomba basi zile barabara za TANROADS zianze kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, barabara ya kutoka Nyololo mpaka pale Mtwango ambayo Serikali iliahidi kwamba itajenga kwa kiwango cha lami, lakini itaendelea kuboresha kwa kujenga kiwango cha changarawe mpaka pesa itakapopatikana, basi mwaka huu mwezi wa Sita tuanze kuitengeneza ikae vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya kutoka pale Mgololo inaenda mpaka Nyigo inapitia Nyihawaga na yenyewe ni barabara ya TANROADS, naomba basi Serikali na yenyewe ianze kuijenga. Kuna barabara ya kutoka Mbalamaziwa mpaka kule Kwatanga ni barabara ya TANROADS, naomba ianze kutengenezwa. Kuna barabara ambayo nairudia tena ya kutoka Mafinga hapa mpaka pale Sawala, imeharibika sana, naomba ianze kutengenezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utengenezaji wa barabara, naomba twende kiutaalam, ile mifereji (outlets) ya kutoa maji itengenezwe kiwango kizuri, kama kuna uwezekano tuweke hata kiwango cha kokoto ili maji yaweze kupita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na barabara zile za Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA). Kuna barabara kwa mfano kule Idete bado hazijatengenezwa kwa viwangovizuri. Kuna barabara ya kutoka Luhunga mpaka kule Iyegeya, haijatengenezwa vizuri. Kuna barabara ambayo inatoka Maguvani mpaka pale Mtambula mpaka Kasanga, wananchi wanalalamika sana ile barabara. Naomba sana waweze kuitengeneza ile barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni mawasiliano. Serikali iliahidi kwamba itajenga mnara katika Kata ya Idete, Kata ya Maduma, Kata ya Kasanga, pale Udumuka hakuna mawasiliano kabisa na pale Kiyowela. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua mawasiliano ni ya muhimu sana. Sasa katika kata hizi nilizotaja, mawasiliano hakuna kabisa. Naomba Serikali kama ilivyokuwa inaahidi iweze kujenga minara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, naipongeza sana Serikali. Ahsante sana.