Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia rehema za kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu jioni hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naunga mkono hoja. Napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Profesa Mbarawa kwa hotuba yake nzuri. Niwapongeze Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Kwandikwa na kaka yangu Mheshimiwa Nditiye na watendaji wote wa Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa juhudi zake anazoendelea kuwatumikia Watanzania bila kuchoka. Nafurahi kila ninapomwona anapofanya ziara anapotatua matatizo ya wanawake wanaokuwa wamemtolea matatizo pale kwenye ziara, anapoyatolea majibu pale pale, kwa kweli huwa nafarajika sana kama mwanamke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie Barabara ya Kidawe –Kasulu - Nyakanazi-Kabingo. Sisi watu wa Kigoma ukisimama usizungumzie barabara hiyo unakuwa hujajitendea haki wewe mwenyewe, lakini unakuwa hujawatendea haki wananchi wa Mkoa wa Kigoma. Kwa muda mrefu sana wananchi wa Mkoa wa Kigoma wanapata shida sana, barabara hiyo haipitiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kipindi hiki cha mvua mwezi wa Tatu na wa Nne, mvua ilikuwa inanyesha kila siku iendayo kwa Mungu na magari yalikuwa hayapiti, likipita gari moja kubwa likikatisha barabara msururu wa magari kama 20 unafata nyuma akinamama na watoto wanapata shida sana. Ndio maana ninaposimama hapa jioni hii ya leo naomba Serikali iendelee kuweka juhudi za kuhakikisha barabara hiyo inakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nyakanazi- Kabingo mkandarasi alishapewa pesa, lakini hajaweza kumaliza kukamilisha barabara hiyo. Nakumbuka mwaka jana Rais alipokuja Kigoma mkandarasi alileta vifaa vyake vingi vya maonyesho kuonyesha kama yupo kazini, lakini alipoondoka Mheshimiwa Rais zile juhudi zikaishia palepale. Naomba basi kwa vile ameshapewa pesa na pesa yake amekamilishiwa tunaomba barabara hiyo iweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mweyekiti, barabara ya Kidahwe - Kasulu mkandarasi alikuwa hajakamilishiwa malipo yake akawa amesimama kuweza kujenga barabara hiyo, lakini kwa sasa ameanza, naomba naye aendelee kuhimizwa ili aweze kumaliza kazi hiyo na apelekewe pesa kusudi barabara hiyo iweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa mazungumzo ambayo tayari wameshaanza na Benki ya ADB, naomba juhudi zifanyike. Barabara hiyo inapita katika misitu minene ukizingatia kwamba Mkoa wetu wa Kigoma umekumbwa na wimbi kubwa la wakimbizi. Wakimbizi wanapelekwa katika Mkoa wetu wa Kigoma, sasa usalama ni wa mashaka kwa sababu watu wote ambao sio waadilifu wanaenda kujificha katika misitu hiyo wanafanya ujambazi na ni kwa nini? Kwa sababu barabara ile haipitiki kiurahisi, ndio maana wanapata nafasi ya kwenda kujificha pale kufanya uhalifu. Kwa hiyo, naomba juhudi zifanyike barabara hiyo iweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishukuru kwa pesa ambazo zimetolewa na Falme za Kiarabu. Naomba zile kilometa 51 za kutoka Uvinza mpaka Malagarasi ziweze kufanya kazi zitakapopatikana ili kipande kile kiweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kipo kile kipande cha Chagu mpaka Kazilambwa, nacho naungana na Mheshimiwa Sakaya kipande kile ni kibaya sana. Wananchi wa Mkoa wa Kigoma hawana namna nyingine barabara zinapokuwa zimeharibika napengine inapotokea pengine usafiri wa treni umesitishwa, hakuna barabara nyingine wanayoitumia tofauti na barabara ya kupitia Uvinza - Tabora - Manyoni - Dar es Salaam. Kwa hiyo tunaomba barabara ile na yenyewe ikamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kigoma - Nyakanazi ndio barabara inayounganisha Mkoa wa Kigoma na mikoa ya jirani, kwa hiyo ni barabara muhimu sana, tunaomba barabara hiyo ikamilishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza juhudi za Serikali kwa kazi kubwa iliyokwishaanza ya standard gauge. Naomba isiishie Dodoma tu naomba ifike Tabora hadi Kigoma. Usafiri wa reli ni muhimu sana kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma na maeneo ya Kanda ya Ziwa. Kwa hiyo, tunaomba standard gauge napo Kigoma iweze kufika kwa sababu nyie wenyewe humu ndani huwa mnatutania Kigoma mwisho wa reli. Kwa hiyo, tunaomba ianzie kule kule ambako ndio kuna historia. Reli ikikamilika wananchi watapata nafasi ya kusafiri kwa gharama nafuu na itakuwa ni rahisi kusafirisha mizigo yao kuipeleka sokoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze kwenye mawasiliano ya mitandao ya simu. Mkoa wa Kigoma umepakana kabisa na nchi jirani za Burundi, DRC na Rwanda na wakati mwingine ukipiga simu kwa watu ambao wapo mipakani wanaitika watu wa nchi jirani. Tunaomba maeneo yale ambayo minara haipo Serikali iweze kufanya mazungumzo na watu wa mashirika wanaopeleka minara ili tuweze kupelekewa minara katika maeneo mbalimbali ili tuweze kupata mawasiliano bila shida yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo kwangu ni hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana.