Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Dr. Haji Hussein Mponda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu katika Bajeti hii ya Wizara lakini naomba nianze kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu aliyenipa afya ya kuniwezesha kutoa mchango katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uungwana hata ukipewa kidogo inabidi ushukuru. Nianze kwa kupongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri ambayo wanaianza ndani ya miaka miwili na nusu tunaona matokeo na tuna imani dhamira ya Serikali na mwelekeo wa Tanzania ya Viwanda mwaka 2025 tutakuwa tumeifikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Morogoro ni mojawapo ya mikoa miwili ambayo ina eneo kubwa. Mkoa huu wa Morogoro umepakana na Lindi, Pwani, Ruvuma, Iringa, Dodoma, Njombe, Tanga kwa maana tuna kilometa za barabara zipatazo 2,017. Katika kilometa hizo kilometa 538 za lami na kilometa 1497 ni za changarawe na vumbi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia bajeti iliyowekwa ambayo tunaizungumzia naomba kidogo Serikali, Wizara Mheshimiwa Mbarawa na Naibu Waziri wako na watendaji wengine hebu muiangalie kwa kina sana. Mkoa tumeomba ili tuhudumuie barabara hii yenye urefu wa kilometa 2,017 yenye madaraja 938, tumeomba bilioni 61, lakini tulizopewa ni bilioni 21 maana yake ni asilimia 43 tu ya tulichoomba. Nini Tafsiri yake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa huu wa Morogoro una mikakati na miradi inayofahamika kuiokoa nchi hii kwenye janga la njaa. Kuna mkakati wa Fanya Mkoa wa Morogoro Kuwa Ghala la Taifa (FAMOGATA). Kuna miradi ambayo inafadhiliwa na marafiki zetu Wamarekani na wadau wengine wa maendeleo mradi wa SAGCOT na kuna mradi mwingine Feed the Future. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii ili iwezeshe nchi hii ijitegemee kwa chakula ni kwamba lazima kuwe na kilimo cha biashara. Sifa ya kilimo cha biashara kuwe na mambo matatu; mosi, kuwa na miundombinu ya uhakika; pili, kuwa na nishati na nishati tayari tunayo na maji, maji tunayo Mkoa wa Morogoro. Tulichopungukiwa ni barabara za uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira yetu ya Mkoa wa Morogoro, hizi kilometa 1,497 zinapita katika maeneo ya bonde na mvua inanyesha karibu miezi saba. Hali yake ni kwamba itakapokarabatiwa tu baada ya miezi mitatu imeharibika. Sasa nauliza hizi bilioni 21 sijui kama zitatuwezesha na hiyo dhamira ambayo tunakwenda ndani ya Mkoa wa Morogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili nifafanue zaidi nirudi kwenye barabara ambayo tutaizungumzia muda mrefu, barabara ya Ifakara – Lupilo – Malinyi – Londo – Lumecha mpaka Songea. Barabara hii ina kilometa 396, barabara hii inapita katika ardhi kama nilivyosema ni bonde lakini ardhi yenyewe ni tifu tifu, kwa hiyo inahitaji hela ya kutosha. Nimekwenda kwa Mheshimiwa Profesa Mbarawa mara mbili, nimeandika na barua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Engineer Mfugale, wanamuumiza bure huyu dada TANROADS Manager wa Morogoro, Engineer Dorothy Ntenga, anajitahidi lakini kwa hicho wanachompelekea wanamuumiza. Nami nimpongeze yeye na kundi lake zima pale TANROADS Morogoro wanajitahidi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekwenda ofisi kwa Mhandisi Mfugale zaidi ya mara mbili…

T A A R I F A . . .

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea Taarifa yake na ndiyo maana nilikuwa nataka kuishinikiza huko huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ina mambo mawili ambayo inabidi Waziri ayaelewe. Tarehe 5 Septemba, 2015, wakati tunatafuta kutengeneza Serikali, tulimnadi Dkt. John Pombe Magufuli na tulimwambia moja ya shida ya wakazi wa Wilaya ya Malinyi ni miundombinu ya hii barabara. Pale pale alisema nimefanya kwenye hii Wizara, sasa nipeni nafasi kwa nchi nitaweza niikamilishe, maana yake ni kwamba hii ni ahadi ya Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni sera. Sera zinazungumza wazi kuunganisha barabara zinazounganisha mikoa ziwe za lami. Hii barabara ninayozungumzia hawa TANROADS wanaijua, inaitwa T16 na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umeshakamilika miaka miwili iliyopita. Sasa inabaki kuanza kujenga hiyo barabara. Habari njema tayari wadau wameshajitokeza, ADB Bank, wao wako tayari kufadhili hii barabara. Sasa niwaulize namna gani wataweza kusogeza speed maana hii barabara sasa hivi imebaki miaka miwili na Rais hapa ameshaahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mawasiliano. Wilaya ya Malinyi kuna Kata mbili ndani ya Tarafa moja ya Ngoilanga Kata ya Kilosa Mpepo na Kata ya Biro. Kata hizi hazina kabisa mawasiliano. Nimeomba sana, habari njema ni kwamba wameniletea kupitia UCSAF ule Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, tumepata minara miwili mmoja Ngoilanga na mwingine Kiswago pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Serikali wamewekeza kila mnara dola la Marekani 30,000, minara hii haifanyi kazi, hii minara ya Tigo, tumeeleza mara nyingi hebu tuone hii value for money, kwa nini hawa wanatuchezea kiasi hicho mbona minara yao ambayo haina ufadhili wa Serikali inafanya kazi? Kwa nini hii minara ambayo wanatengeneza sub-standard? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na minara hiyo lakini bado Kata yangu ya Ngoilanga iko kwenye giza, haina mawasiliano na vilevile Kata ya Biro bado hawana mawasiliano kabisa. Nimwomba Mheshimiwa Waziri, wakati anajumuisha awahakikishie maana ilikuwa ni mojawapo ya ahadi ambayo wameahidi. Mheshimiwa Profesa Mbarawa wewe ni rafiki yangu toka 2015 ulikuwa unasema mimi nitamaliza hii lakini mpaka leo hii hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Wizara wameelezea ujenzi wa vivuko, kuna kivuko pale cha Kikove kinaunganisha Jimbo la Mlimba na Jimbo la Malinyi. Kivuko kile wameweka milioni 400 kwa ajili ya kumalizia ujenzi. Niwaombe, hata wakimalizia ujenzi, kile kivuko bado kuna changamoto, hakuna barabara ya kufika pale kutoka Ngoilanga. Niwaombe, kwenye hii bajeti watafute na mifumo mingine au vyanzo vingine wakimaliza kile kivuko cha Kikove basi ili kitumie barabara ile sasa kutoka kwenye Kijiji cha Ngoilanga iweze kufika pale kwenye kivuko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.