Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwanza nataka Mheshimiwa Waziri anisaidie kupata majibu kuhusiana na barabara za Jimbo la Kawe ambazo ni barabara za kupunguza foleni ya Makongo, Chuo Cha Ardhi, Makongo Juu kwenda Goba. Nimesoma kitabu cha hotuba hapa kinaonesha kwamba, kilometa nne zimekamilika. Sasa kilometa nne zilizokamilika ni kutoka Goba na kilometa moja imeingia Makongo.

Mheshimiwa Spika, sasa nataka nifahamu, kwa sababu zoezi sasa hivi ni kama limesimama na haijulikani kama kuna fedha ya fidia kwa sababu hapa fidia sijaona; na corridor ya barabara ina changamoto kidogo. Sasa nataka nipate majibu kwa mustakabali wa barabara ya Makongo.

Mheshimiwa Spika, pili, nataka vile vile anisaidie majibu ya barabara ya Wazo-Tegeta Kibaoni-Wazo-Madale, kuungana na Goba; kuna ujenzi unaendelea sasa hivi, lakini nikiangalia hiki kitabu kinazungumzia kilometa tano zinazojengwa sasa hivi, hakizungumzii kilometa sita ambazo zitaunganisha Madale kwenda Wazo. Kwa hiyo, naomba anipe hayo majibu kwa sababu hii barabara ni very strategic.

Mheshimiwa Spika, la tatu lakini sio kwa umuhimu; tunafahamu kwamba kuna upanuzi wa barabara ambao unatakiwa ufanyike kati ya Tegeta kwenda Bagamoyo. Sasa pale ni kati ya maeneo ambayo yanakumbwa na mafuriko miaka yote. Tutakumbuka katika utawala wa Awamu ya Nne viongozi wote walikwenda pale, mpaka aliyekuwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Pinda na tukakubaliana kuna mfereji wa chini utakaojengwa, ili kuondoa yale mafuriko na kumwaga maji Mto Nyakasangu.

Mheshimiwa Spika, sasa mfereji ulichorwa na watu wa TANROADS Mkoa wa Dar-es-Salaam, lakini mpaka sasa hivi hakuna hatua zozote ambazo zinafanyika. Sasa nataka tu nifahamu kwa sababu wananchi wanaumia sana kipindi hiki cha mafuriko, kwamba ule mpango wa ujenzi wa mfereji upo? Ama kwa sababu kuna mpango wa kuipanua hii barabara kutoka Tegeta kwenda Bagamoyo basi ndio utajumuishwa katika huo mradi wa upanuzi wa barabara?

Mheshimiwa Spika, baada ya kumaliza hayo ya ufupi ya jimboni kwangu, naomba nije kwenye suala la kitaifa la ATCL. Nikiangalia randama ukurasa wa 11 tunaambiwa kwamba kwa mwaka huu wa fedha Serikali inatarajia kufanya ununuzi wa ndege mpya kwa ajili ya Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL), shilingi bilioni mia nne tisini na tano. Tunakumbuka vile vile mwaka jana Serikali kupitia Waziri wa Fedha ilitenga vile vile bilioni zisizopungua mia tano kwa ajili ya ununuzi wa ndege.

Mheshimiwa Spika, ni muhimu ieleweka hapa na Wabunge waelewe, kwamba hoja hapa si kupinga ununuzi wa ndege. Hoja hapa ni hizi fedha ambazo tunaziwekeza ambazo ni matrilioni ya shilingi zinaenda kuzalisha ama tunaenda kuzitupa chini na zinapotea kama fedha nyingine? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina taarifa ya Msajili wa Hazina hapa. Msajili wa Hazina ndiye amepewa dhamana ya kusimamia mashirika yote ya Tanzania, anasema hivi, ukurasa wa nne wa taarifa yake:-

“Imekuwa vigumu kwa ofisi yangu kuweza kufanya uchambuzi wa kina wa utendaji wa ATCL kutokana na kutokuwepo taarifa za kutosha za kampuni. Kwa mfano, mahesabu ya kampuni yaliyokamilika ni ya mwaka 2014/2015 tu yaliyofanywa na PWC. Hata hivyo mahesabu hayo hayajatizamwa wala kupitishwa na Bodi. Hali hii imesababisha Ofisi ya Msajili wa Hazina kutoweza kuchambua na kubainisha hali halisi ya uwekezaji ilivyo hadi sasa kuhusu madeni na mali za kampuni,”

Mheshimiwa Spika, vile vile wanasema wanashindwa kujua hali ya ukwasi wa kampuni kwa sababu ya kampuni kutokuwa na mahesabu kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukija kwenye taarifa yenyewe ya ATCL wanasena kwamba, shirika halikuwa na mpango wa biashara. Yaani tunawekeza bilioni mia tano 2016/2017, 2017/ 2018 tukawekeza bilioni mia tano, 2018/2019 tunataka tuwekeze bilioni mia nne tisini na tano halafu hatuna mpango wa biashara. Hivi unaenda kuanzaje kufanya biashara wakati huna mpango? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hakuna business plan, tunawekeza trillion shillings. Tunakuja hapa wanasema inabidi tuanze kuajiri management yenye uwezo kwa sababu sasa hivi shirika halina wataalam wenye uzoefu wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Bunge lako mwezi Januari, walitoa taarifa za Kamati, kwa niaba ya Bunge wameita wataalam wa Serikali wanaosimamia mashirika yetu. Wamesema kwamba shirika letu mpaka sasa lina hali dhoofu na lina madeni ya shilingi bilioni mia tano kumi na saba. Sasa shirika lina madeni, shirika halina mpango wa biashara, shirika halina wataalam, tunaweka trilioni mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niliombe hili Bunge tutekeleze wajibu wetu. Hivi inaingia akili timamu, kwamba kwenye kilimo ambacho mkinaajiri asilimia zaidi ya 75 ya Watanzania tumeweza kuweka bilioni 11 tu, kwenye ndege ambayo tuna uhakika kwamba hii pesa tunaenda kuimwaga chini, tuna uhakika, tumeweka trilioni moja.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri akija hapa atujibu. Ni muhimu akajua wasije wakafikiria watakuwa salama, hizi pesa wanakumbuka akina Mramba, mnakumbuka akina Yona, hizi pesa tukigundua wameziwekeza kinyume na utaratibu, kama ambavyo nyaraka zinaonesha, tutawachukulia hatua.

Mheshimiwa Spika, ni muhimu Mheshimiwa Rais akajua pia, hiyo kinga aliyonayo ya Kikatiba inaangalia kama kuna masuala yalifanywa kwa makusudi kwa kuona kwamba kuna hasara mbele tukajiingiza kichwa-kichwa, huo usalama ama hiyo kinga ya Katiba haipo, tutamshughulikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani. Naongea kwa dhamira ya dhati na najua Wabunge wengi wanajua, wengi wakiwa huko nje wanalialia, tukija huku ndani…

KUHUSU UTARATIBU . . .

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, Rais alichaguliwa na Watanzania. Hili Bunge ni la wawakilishi wa Watanzania. Rais lazima akosolewe na jina la Rais lazima litajwe kama anaenda kinyume na utaratibu. Lazima hii perception kwamba, Rais ni untouchable, lazima iishe. Bunge likiogopa kumtaja Rais wakati sisi tunapitisha bajeti, Rais ni sehemu ya Bunge, tutakuwa tunalifanyia makosa makubwa sana aifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi sijatumia jina la Rais kwa kebehi, nimesema hivi, tuna taarifa mbili hapa; tuna taarifa ya Msajili wa Hazina, tuna Taarifa ya ATCL. Taarifa ya Msajili wa Hazina inasema, nataka…

T A A R I F A . . .

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nimesema hivi, siwezi kumjibu Dokta Shika bidhaa ya Kichina, umenielewa; nikimjibu nitakuwa najidhalilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja yangu iko wazi kabisa. Nimesema hivi na naomba nirudie kwa sababu, najua kengele itagonga; nina nyaraka mbili za Serikali, nina nyaraka ya Msajili wa Hazina, nina nyaraka ya ATCL yenyewe; wanasema kwamba, mosi, tumewekeza bilioni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)