Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kwa kweli kwa kuipongeza Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa kufanya kazi nzuri kwa maeneo mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri, naona kwa kweli anavyofanya kazi yake, yeye na timu yake, Manaibu wake wote wawili, kwa kweli niwapongeze sana, katika Awamu hii mnafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri anazofanya, nimesoma hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri hapa na nimeona kwa kweli barabara ambayo tumeiomba kwa muda mrefu, Barabara ya Mbulu ambayo imeelezwa hapa; Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti mpaka Lalago na huko Maswa na Bariadi. Barabara hii imeombwa kwa muda mrefu sana na ipo kwenye Ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi, ukurasa wa 18. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafarijika kwamba kwa kweli leo nimeiona angalau imetambulika, ila ninavyoona hapa kadri barabara hii ilivyo na usumbufu kwa sasa ningeiomba Wizara na Mheshimiwa Waziri aone, najua hajawahi kutembelea barabara hii, najua hajafika kabisa, lakini aone kwamba barabara hii sasa ni hitaji kubwa mno la wananchi wa maeneo mengi; wananchi wa Karatu, wananchi wa Mbulu Mjini, wananchi wa Mbulu Vijijini, wananchi wa Mkalama, wananchi wa Singida, maeneo yote yale yanayopita moja kwa moja mpaka ufike Lalago, Maswa, mpaka kwako kule barabara hii inafika yenye kilometa 389. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema ni hiki; barabara hii itakapojengwa itafungua eneo kubwa ambalo limesahaulika kwa wingi na uchumi wa watu hawa utapanda. Nimeona kwamba mmeandika hapa kwenye ukurasa huu wa 38 kwamba itafadhiliwa na KfW, hawa Benki ya Ujerumani, sina tatizo, lakini ninachohofu; mwaka jana walisema ipo kwenye upembuzi wa awali, sasa hofu yangu mwakani watasema pia ipo kwenye upembuzi wa kati lakini baadaye mtatuambia tena iko kwenye upembuzi yakinifu, miaka mitano imekwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu ambaye yuko sasa wa Awamu ya Tano wa Hapa Kazi Tu ameahidi barabara hii na ipo kwenye Ilani na nini maana ya ilani; ni mkataba kati ya mtawala na mtawaliwa. Tumeahidi hii, ndugu yangu, Mheshimiwa Profesa Mbarawa, aelewe, tumeahidi kwenye mikutano yetu, wananchi wa Mbulu na maeneo haya niliyoyataja wanaitegemea barabara hii na kule hatuna kitu kinaitwa lami kabisa, hatujawahi kuona tangu Mbulu imeanzishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikumbushe, Mbulu imeanzishwa 1905, haina barabara. Uchumi wa kule kwetu zaidi ya barabara hatuna lolote. Hatuna maziwa ambayo tungesema tungeweza kufanya usafirishaji wa maboti, meli na nini, hakuna huko na viwanja vya ndege kule hakuna. Kwa hiyo, tusipopata barabara hii ambayo naisemea sasa hatuna namna yoyote ya kufanya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa ndugu yangu Mheshimiwa Waziri aweke basi hela ambayo itaonesha namna nzuri ya kufanya upembuzi yakinifu mwakani. Najua ametenga milioni 50, milioni 50 sisi Wabunge saba tuliosema hapa tukichanga tunaweza kufika hizi hela, kwa nini nasema hivi? Sina nia ya kudharau alizoziweka hizi, lakini ni kidogo sana. Milioni 50 kwa barabara hii yenye kilometa 389, jamani sawasawa hakuna kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu barabara hii ni muhimu sana, muhimu mno, inaunganisha Mikoa ya Arusha na Manyara, Manyara na Singida na kutoka Singida inakwenda mpaka Meatu na Mheshimiwa Waziri anajua Simiyu iko kule. Kwa hiyo, niombe basi maana barabara hii ni muhimu na ni muhimu kwa sababu kuna Hospitali kubwa ya Haydom iko katikati ya mikoa hii ambayo watu wengi wanaitegemea kwenda katika hospitali hii. Basi nimwombe Mheshimiwa Profesa Mbarawa, anajua nampenda sana, lakini mapenzi haya yaende basi na kuweka hii barabara, awekea barabara ndugu yangu, aweke barabara narudia tena. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi, najua wazi kwamba Rais wetu ni msikivu, ili asionekane Rais ambaye ameahidi halafu baadaye haikufanyiwa kazi, Mheshimiwa Waziri asimuangushe, amemweka hapa ili akamsaidie kazi hii. Aweke Barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti – Maswa – Lalago, twende mpaka kwa Mheshimiwa Chenge kule. Kwa hiyo, naomba ndugu zangu wanielewe, Mawaziri wako watatu hapa wakumbushane katika ofisi yao basi, kwa kuwa barabara hii ni muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipenda nichangie mchango wangu wa dakika tano kwa kusemea barabara hii tu kwa sababu ndiyo kufa na kupona. Leo asipoiweka barabara hii akaiwekea fedha mwakani atakuwa hajatusaidia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, najua atatuwekea barabara.