Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Lucy Simon Magereli

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa ya kuchangia ndani ya Bunge hili Tukufu katika hii hoja ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Ningetaka nianze na kuendelea hapo hapo alipoishia Mheshimiwa Kubenea kuhusu ATCL kwa sababu hili ni suala muhimu sana ambalo lazima tuendelee kukumbushana, lazima tuambiane ukweli, lazima tuwe wakweli juu ya nini tunataka kuhusu kuifufua ATCL.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiona ni kwamba nadhani wataalam wa Tanzania hawajapewa fursa kabisa na wala nadhani hawakushirikishwa wakati ulipokuja mjadala wa kutaka kuifufua ATCL. Naamini wangeshirikishwa maamuzi haya yaliyofanywa leo yasingefanywa. Hivi jamani ni nani aliyemshauri Mheshimiwa Rais kwamba anunue ndege? Kulikuwa kuna uwezekano mkubwa kabisa wa kuifufua ATCL kwa kutumia ndege za kukodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hatukuhitaji ndege kubwa Tanzania kwa wakati huu kwa sasa. Hivi tunatakaje kwenda kushindana na mashirika makubwa ya kimataifa ya ndege ambayo yameshajiimarisha kwa muda mrefu, ambayo pamoja na yenyewe yanafanya biashara ya hasara. Badala ya kufikiri ya kwamba tunahitaji kwanza kuimarisha mtandao wa ndani wa ndege kabla ya kuanza kushindana kimataifa.

T A A R I F A . . .

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee na mchango wangu kwa kusema suala siyo kuhitaji ndege. Ndege gani, kwa utaratibu upi, kwa malengo gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri na ningeomba nisikilizwe kwa sababu hivi tunavyozungumza yaani hata viwanja vya ndani ya nchi vya ndege havifai kwa matumizi yetu. Mtalii leo akitua pale JK Nyerere anataka kwenda Ruaha, anataka kwenda Rubondo, anataka kwenda kisiwani Lake Victoria anapata tabu ya kufika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunadhani ukweli halisi ni kwamba Tanzania inao uwezo wa kununua ndege kubwa wakati network ya ndani bado haijakuwa imara? Ambacho kingefanywa sahihi ni kwamba tulihitaji kuimarisha network yetu ya ndani kwanza halafu baadaye tutapiga hatua hiyo kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize, hivi ni nani aliyemshauri Mheshimiwa Rais kwamba tununue ndege kutoka makampuni tofauti tofauti? Tunaongelea habari ya Bombardier, tunaongelea habari ya Boeing, tunaongelea habari ya Air bus. Haya yote ni mzigo kwa nchi hii. Ndege za Bombardier zitahitaji kuwa na service centre yake yenyewe, ndege za Boeing tutahitaji kuwa na service centre, ndege ya Air bus itahitaji service centre. Unatengeneza service centre Tanzania kwa ndege moja ya Air bus? Unatengeneza service centre kwa ndege moja, mbili za Boeing!

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tukubaliane kwamba kesho na keshokutwa Bunge hili litakaa tena tupeane taarifa, tulaumiane kwamba tumechezea kiasi kikubwa sana cha pesa za walipa kodi katika kuifufua ATCL ambayo mwisho wa siku imegeuka kuwa msiba kwa Taifa. Nawaambieni huu ndiyo ukweli, ATCL miaka mitano ijayo tutakaa ndani ya Bunge hili tutajadili jinsi ambavyo imekuwa tatizo kwa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali kwamba hili suala la ATCL warudi kwenye mikono ya wataalam, watafute menejimenti nzuri, washauriane, waone namna ambavyo ATCL itafufuliwa. Hizo ndege mnazozisubiria huko kwa sababu hebu kwa mfano tumetumia bilioni 130 ku- sort ile kesi ya Mahakama ya Bombardier zile bilioni 130 ni ndege nne zingine za Bombardier. Jamani mnataka mseme hata hapo mlifanya rational decision? Hizo pesa bilioni 130 ziliidhinishwa na Bunge gani? Nani aliyeidhinisha pesa zika- sort hiyo tatizo la Mahakama Canada? Hasara ambayo ATCL itatutengenezea ni kubwa na itaenda ku-bust. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihamie kwenye suala la Daraja la Kigamboni. Naomba nishukuru na nipongeze mchango wa Mheshimiwa Zainabu Mndolwa. Daraja la Kigamboni ni mzigo kwa Watanzania wa Kigamboni. Sisi tulikuwa tunatumia vivuko vya Magogoni, MV Kigamboni na Alhamdullaah wametuongezea kivuko kingine cha MV Kazi. Vile vivuko vyote tunalipia, awali nyuma kabla ya daraja tukaambiwa daraja litakuja kuwa suluhisho na kutupunguzia gharama kama optional way ya kupita kama huhitaji kulipia au huna huo uwezo wa kulipia. Lile daraja limefanywa la kulipia, tena basi tulifikiri ni kwa muda fulani specific lakini it’s a life time business. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Mheshimiwa Waziri atusaidie, kwa hili kwa kweli wamewadanganya na wamewadhulumu wananchi wa Kigamboni. Walikuwa na sehemu yao ya kulipia kwenye ule mkataba na NSSF, Serikali wameingia mitini, wamegoma kulipia sehemu yao ya mkataba, badala yake wamewaangushia wananchi wa Kigamboni kulipia zile gharama na hata hawaja-specify kwamba ni kwa muda gani. Maana yake sasa sisi tumeshakuwa commodities of trade.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu wa Kigamboni ukitaka kuvuka kwenye daraja unalipa, kwenye kivuko unalipa na basi si gharama kidogo ni gharama kubwa sana. Gari ya daladala ambayo inatoka Mnazi Mmoja kuja Kigamboni kuvuka pale darajani inalipia Sh.7,500 kila inapopita.

Sasa fikiria kweli wananchi wa Kigamboni kama tulifikiri tukipata daraja basi tutapata na namna rahisi ambayo tutakuwa tunavuka kutoka Kigamboni kuja Dar es Salaam badala yake mpaka leo tuna…

T A A R I F A . . .

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili ningeweze kuafikiana nalo kama tungekuwa tuna mbadala mwingine, lakini sisi tunalipa kote kwenye kivuko unalipa na kwenye daraja unalipa. Kwa hiyo sikubaliani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye hoja nyingine ya barabara ya Kibada - Mwasonga – Tundwi – Kimbiji. Nashukuru Mheshimiwa Waziri kwenye kitabu chake ametaja barabara hii ambayo tangu bajeti ya mwaka wa 2016/2017, 2017/2018 imetajwa na imetengewa fedha. Ile barabara ni muhimu sana kwa eneo hilo la Kigamboni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile barabara inapita katika kata nne ambazo bahati nzuri tunashukuru ni katika kata ambazo zina maeneo mengi ya uwekezaji. Ile barabara hata leo hii ukipita hali yake ni mbaya mno na tumekuwa tunaitengea fedha inatajwa, inatengwa, inatajwa lakini haipewi fedha na wala haijawahi kufanyiwa kulingana ambavyo taarifa zimekuwa zimetolewa katika kitabu cha Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata taarifa zilizotolewa hapa kwenye kitabu ukurasa wa 34 sijaelewa kilichomaanishwa kwa sababu kwenye sehemu ya 21 inasema barabara ya Kibada – Mwasonga – Kimbiji kilometa 19 lakini sehemu ya 22 inasema barabara ya Kimbiji – Tundusongani kilometa 30.5 sijaelewa kwa sababu sidhani kama barabara hii inafika kilomita 49 point something nadhani kuna jambo hapa halikuwekwa sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ile barabara haipitiki hasa wakati wa mvua. Nimeona wanasema upembuzi yakinifu na usanifu wa kina unaendelea, tunaomba Mheshimiwa Waziri atusaidie hata itengenezwe kwa kiwango cha moram na ishindiliwe vizuri, iwekewe mitaro ya barabara kwa sababu yale malori ya cement yanapita kutoka Nyati Cement Kimbiji yanapata shida sana kupita kwenye ile njia na mara nyingi yanakwama na yakishakwama maisha yetu ya Watanzania wa eneo lile yanakuwa magumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie pia mtandao wa barabara katika Manispaa ya Dodoma. Naamini tunakubaliana wote tuliokaa ndani ya nyumba hii kwamba uamuzi wa kuhamia Dodoma nadhani kuna step ilirukwa ya kuandaa miundombinu. Barabara za Dodoma sasa hivi mji huu asubuhi unasimama msongamano ni mkubwa sana na barabara ya Dodoma ni nyembamba sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi barabara ya Dar es Salaam hii kwa maana ya kutokea maeneo ya Ilazo kuja Kisasa mpaka kufika eneo la Bunge asubuhi ni eneo lenye msongamano mkubwa sana. Nimeona orodha ya barabara zinatajwa hapa katika ukurasa wa 36 barabara ya Shabiby- Arusha-Dodoma road-round about, barabara ya Chimwaga- Chinyoya-Kikuyu, barabara ya Dar es Salaam-Nane nane na nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, hizi barabara waziangalie kwa jicho la wepesi tena kwa kipaumbele kabisa especially haya malori makubwa yanayoingia mjini ile barabara ambayo ilikuwa imeandaliwa inayotokea Ihumwa basi ile barabara ijengwe kwa uharaka ili tupunguze magari makubwa ambayo yanaingia ndani ya Mji wa Dodoma na kusababisha msongamano mkubwa sana na ikitokea kwa mfano hapa Dodoma barabara moja tu ikapata hitilafu mji wote unasimama. Kwa hiyo, wanaweza kuona namna ambavyo haiko networked sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimalizie hoja yangu kwa kusema naomba tuwe wakweli, naomba tunaposema tunaishauri Serikali tuseme ukweli, naomba tunapopewa ushauri na wataalam hasa katika maeneo haya ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Yako mambo mengi sana katika Wizara hii ambayo yamekuwa kama wimbo wa kawaida hivi upembuzi yakinifu, sijui uchambuzi wa kina yaani kuna ucheleweshwaji mwingi tunashindwa kusema ukweli kwamba bajeti yetu haikidhi haja.