Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naanza kwa kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano na Awamu zilizopita kwani tayari tumepata daraja la Kilombero. Wananchi wa Morogoro tunashukuru sana na hivi karibuni daraja letu la Kilombero litafunguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naomba kuongelea ni barabara ya Kidatu – Ifakara – Kitanda - Namtumbo. Hii barabara imetengewa fedha kidogo, lakini tunashukuru Serikali hata kwa kutengewa fedha hiyo. Fedha iliyotengwa ni ya kutoka Kidatu – Ifakara, tunaishukuru sana Serikali kwa sababu hivi karibuni itawekewa jiwe la msingi. Hata hivyo, kwa upande wa kutokea hapo Ifakara - Namtumbo bado haieleweki. Ni muda mrefu tumeisemea tunaomba sana iweze kutengewa hela kwa bajeti zinazokuja au hata sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naomba kuongelea ni usafiri wa anga hasa nikimaanisha viwanja vya ndege vya mkoa. Mkoa wa Morogoro ni mkoa unaokua, una mbuga za wanyama ambazo ni Mikumi pamoja na Selous ambapo unapata watalii wengi na pia kuna ajali zinatokea. Juzi ajali ya ndege ilitokea kwenye kiwanja cha tumbaku ilibidi isukumwe kwa sababu ya kutokuwa na kiwanja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri tufikirie kiwanja cha abiria ambacho kitajengwa Mvomero au Kisaki. Morogoro huwezi kujenga hovyo ovyo kwa sababu ya mambo mengine yanayoeleweka, lakini kwa upande wa Mvomero na Kisaki kinaweza kikajengwa kikatumiwa na watalii wanaokuja kwenye mbuga zetu na kwa abiria pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Bigwa – Mvuha - Kisaki. Barabara hii tunaiongelea mara kwa mara ambayo ikijengwa kwa lami itasaidia watalii pia na kusafirisha mazao mengi ambayo yanaweza kulisha viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa TARURA pamoja na TANROADS, naungana na wenzangu kusema kwamba TARURA iangaliwe kwa sababu bila kupata malighafi kutoka vijijini ambako barabara zake ni mbovu hatutaweza kwa kweli kufanikiwa vizuri sana. Naomba sana itengewe fedha zaidi ili kusudi tuweze kujengewa hizi barabara zetu kadri inavyowezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Ifakara – Mahenge - Mwaya - Ketaketa sijaisikia. Hii ndiyo barabara ya kwenda Selous ambako kuna watalii na malighafi. Kwa hiyo, naomba wakati wanatenga bajeti na yenyewe waifikirie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile barabara ya kutoka Ifakara - Mbingu - Chita na yenyewe sijaisikia. Naomba na yenyewe waiangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye mitandao ya simu, kuna sehemu mbalimbali ambazo Wabunge tumempatia Mheshimiwa Waziri ambazo hazina mitandao. Naomba sana waziangalie kusudi na zenyewe ziweze kupata minara ya simu tuweze kupata usikivu kwa upande wa Mkoa wetu wa Morogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee barabara ya Magole – Dumila - Kilosa – Mikumi – Mziha – Turiani, naishukuru Serikali imeanza kujengwa kwa lami, lakini kuna sehemu ambayo bado haijajengwa kwa lami. Naamini imetengewa fedha lakini fedha hiyo kidogo iliyotengewa ni kwa sababu ya fidia na hela za kuwalipa wakandarasi. Kwa hiyo, hiyo sehemu ya Ludewa - Kilosa - Mikumi - Mziha - Turiani naomba itengewe fedha kusudi iweze kupitika. Wakati wa mvua barabara ya Kilosa - Mikumi mawasiliano yanakatika kabisa ambapo huko ndiyo mahali ambapo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.