Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Juma Othman Hija

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua fursa hii kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwa maandishi hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Pili, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri na wafanyakazi wake wote kwa utayarishaji na uwasilishaji mzuri wa hotuba hii katika Bunge hili. Katika kuchangia hotuba hii napenda kuchangia katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni uboreshwaji wa Hospitali za Rufaa za Mikoa. Takwimu zinaonesha kuwa ajali nyingi za magari zinatokea katika sehemu za mikoani kuliko mijini ambako ziko hospitali nzuri zenye vifaa lakini Hospitali za Rufaa za Mikoa inaonekana zina upungufu wa baadhi ya vifaa vya kukabili ajali hizo zinapotokea na kulazimika wagonjwa kusafirishwa kupelekwa Dar es Salaam. Mfano wa hivi juzi ambao Waheshimiwa Wabunge sita walipata ajali na kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro ilibidi wasafirishwe kupelekwa Dar es Salaam kwa matibabu zaidi baada ya kukosekana CT Scan ambayo ingeweza kuwachunguza na kuonekana matatizo yao pale Morogoro, hii inawatokezea Waheshimiwa Wabunge, lakini je, ajali hii kama ingekuwa ya wananchi wa kawaida ingekuwaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Wizara na Serikali kuendeleza juhudi za kuziimarisha hospitali hizi kwa kujipatia vitendea kazi vya kisasa ili kuweza kukabili matokeo haya na mengineo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu udhibiti wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza; napenda kuipongeza Wizara hii kwa kuendelea kusambaza elimu juu ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Wizara inajitahidi sana kueneza elimu katika mikoa yote ya Tanzania. Ushauri wangu katika suala hili ni kuomba Wizara iongeze ujuzi wa elimu hii katika maeneo ya vijijini ambako hawawezi kupata elimu hii kwa kutumia njia za vyombo vya habari kama vile tv na magazeti. Ni vyema Wizara ikawa na timu maalum ambayo itaweza kwenda moja kwa moja vijijini ambako itaweza kuwaelimisha wanavijiji

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante.