Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Silafu Jumbe Maufi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, natoa pongezi kwa kazi nzuri ifanyikayo na uongozi wa Awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli. Pia Waziri na Naibu Waziri wa Afya na timu yao nzima nawapongeza kwa kujitoa na kujituma kwa dhati katika nafasi zao kiutendaji kazi, wameonesha uweledi na uzalendo kwa dhati ya huduma kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa tuna wananchi takribani milioni 55, Serikali inajitahidi sana kwa upatikanaji wa dawa kwa uponyaji wa maradhi kadhaa. Kufuatana na hotuba inadhihirisha mapungufu ya rasilimali watu yaani watumishi na maandalizi yao yanachukua muda mrefu. Tunaomba Serikali kujipanga kwa kuwasambaza wataalam waliopo ambao wamerundikana kwenye miji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya. Vijijini tumekuwa na upungufu mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili Serikali kuangalia stahiki za wataalam wa afya ili waendelee kutoa huduma kwenye zahanati za Serikali, kwani tunawasomesha kwa pesa nyingi lakini wanakosa ajira na stahiki bora wanakwenda kwa watu binafsi au hata nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzungumzia suala zima la mapungufu makubwa ya rasilimali watu yaani watumishi wa maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii. Mheshimiwa Waziri tunakuomba sana upigie jicho la pekee na kutatua mapugnufu ya maafisa maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii kwani watu hawa ni wa muhimu ndani ya maeneo yetu. Wananchi wetu wanahitaji kupatiwa uwelewa na ufahamu wa maendeleo yao, hasa kina mama ndio chachu wa kila kitu ndani ya Kaya, Kijiji, Wilaya, Mkoa hadi Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wa matumizi ya bima ya afya ni pamoja na kuinua uchumi na kuachana na umaskini. Katika Mkoa wa Rukwa, Maafisa Maendeleo ya Jamii tuna mahitaji ya 158 tulionao ni 50 tu; katika Halmashauri ya Sumbawanga mahitaji ni 39 waliopo 15 kwa pungufu ya 24; Nkasi mahitaji ni 34 waliopo 10 kwa pungufu 24; Manispaa mahitaji ni 33 waliopo 13 kwa pungufu ya 20 na Kalambo mahitaji ni 29 waliopo 13 kwa pungufu ya 16.

Mheshimiwa Naibu Spika, maafisa ustawi wa jamii ni wachache sana tena sana ukizingatia uhitaji kwao ndani ya jamii katika suala zima la kukinga. Unahitajika uelewa huu awali kwa wananchi wetu kuliko tiba ni gharama kubwa. Hali halisi kwa mkoa wetu kwa maafisa ustawi wa jamii ni mkoa mmoja, Kalambo mmoja, Sumbawanga wawili, Manispaa watatu, hospitali ya mkoa wanne. Ifahamike mkoa wa Rukwa una kata 97 na mitaa 172 tu na Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa. Tunahitaji kuiomba Serikali kuona umuhimu wa kutoa ajira kwa watumishi wa kada hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Wizara kuona namna ya kuwasaidia na kuwatatulia Idara ya Maendeleo ya Jamii changamoto zifuatazo; usafiri (magari, pikipiki), vifaa vya uandishi (stationary), uhaba wa fedha za mikopo za Mfuko wa WDF toka mapato ya ndani (Wizara kulitolea maombi kwenye Serikali na ufuatiliaji wa karibu kwa maslahi ya watumishi hawa).

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali kuona umuhimu wa kutoa taulo kwa watoto wetu mashuleni kwani tunazo pamba za kutosha kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa pamba hapa nchini, tuna kila namna ya kuzalisha taulo hizi na wanafunzi wa kike waweze kujistiri katika kipindi cha miaka nane kabla ya kwenda chuo angalau tuwawezeshe Watanzania hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.