Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Kemirembe Rose Julius Lwota

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. KEMIREMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kukushukuru wewe kwa kuweza kunipa nafasi hii ya kuchangia, vilevile napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kunifikisha hapa siku hii ya leo na kuwashukuru wanawake wote wa Mwanza walionipigia kura kwa wingi kabisa nasema ahsanteni wote na ninawaahidi sitowaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kushukuru na kumpongeza Rais wetu John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kufanya na hotuba nzuri sana aliyotufungulia Bunge letu hili.
Vilevile napenda kuwapongeza Mawaziri wote walioteuliwa na Mheshimiwa Magufuli, amewaamini na sisi wote tunawaaamini na tunaona kazi mnazozifanya na tunawapongeza tunasema kazeni buti tuko nyuma yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kuunga mkono asilimia mia moja hotuba ya Mheshimiwa Rais. Mambo aliyeyasema kwenye hotuba yake ni mengi yamehusisha nyanja zote, kwa Mtanzania na kwa maendeleo ya Tanzania yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ameongelea suala la miundombinu, ameongelea suala la reli na suala barabara. Kwanza kabisa napenda kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri inayofanya kwenye barabara zetu, wote ni mashahidi, barabara zimeunganishwa, Mikoa tofauti mingi imeunganishwa kwa lami na wote tunafahamu. Mheshimiwa Rais alishawahi kutoa mfano humu Bungeni akasema barabara za lami zilizopo Tanzania zingekuwa Burundi wasingepata hata sehemu ya kulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo natoa pongezi sana kwa mambo yanayofanyika na Serikali yetu ya Cha cha Mapinduzi. Napenda nijikite kwenye suala la barabara baada ya mvua za elnino zilizoanza kunyesha hivi karibuni mwezi Novemba Mkoa wa Mwanza tulipata matatizo makubwa ya maafa, watu walipoteza maisha. Lakini vilevile barabara zetu zimeharibika sana kwa Majimbo yote mawili ya Mjini, nikiwa na maana ya Jimbo la Ilemela na Nyamagana.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya uharibifu huo, jitihada zilifanyika kwenye Halmashauri zetu, Halmashauri zikaandika barua TAMISEMI, TAMISEMI wakatuma wataalam wakaja Mkoa wa Mwanza, wakazunguka na ma-engineer wetu wa Wilaya zote mbili na wakaona uharibifu zaidi umefanyika kwenye Wilaya ya Ilemela.
Mheshimiwa Spika, utafiti huo ulifanyika mwezi Novemba na baada ya hapo mvua zimeendelea kunyesha sana, na mpaka hivi tunavyoongea mvua zinanyesha na barabara za Mwanza hususani Ilemela zimekatika kabisa. Baada ya wataalam hao kuja, walifanya emergence plan kana kwamba barabara za Mwanza hususani za Ilemela zitengewe fedha na zije zitnegenezwe, lakini mpaka sasa hivi ninavyoongea jambo hilo halijafanyika, barabara hizi ambazo zimekatika kabisa zinafanya wananchi wetu wanashindwa kufika mahali wanapotaka kwenda kwa wakati, gharama za usafiri kwa maeneo yanayopitika zimekua juu, akina Mama wajawazito wanashindwa kufika hospitali kwa wakati, wanajifungulia barabani, hali kwakweli ya barabara ni mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya barabara ambazo zimeharibika sana naweza kuzitaja. Mojawapo ni barabara ya Kirumba – Mwaloni ambayo inaenda kwenye soko letu la samaki la kimataifa. Barabara hii inaingiza fedha nyingi sana kwenye Halmashauri ya Ilemela na Serikali kwa ujumla wake, lakini barabara hii sasa hivi imekatika kabisa, maroli na magari makubwa yanashindwa kupita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna barabara ya Kiseke PPF; barabara ya Busweru - National na barabara ya Bwiru.Tunamuomba Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Miundombinu kama kuna uwezekano hili suala litatuliwe kwa sababu hali ni mbaya sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni Waziri alifika Mkoa wa Mwanza akatoa ahadi ya kujenga barabara ya lami inayotoka Sabasaba kwenda Busweru. Barabara hiyo hali ni mbaya na safari hii mpaka barabara imefungwa yaani haitumiki tena, kwa hiyo, tunaomba kwenye bajeti hii inayokuja tutengewe hizo fedha za huu mradi ambao Mheshimiwa Waziri ametupa ahadi na utekelezwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kuchangia kwenye masuala ya afya, wote ni mashahidi masuala ya afya wote ni mashahidi hotuba ya Mheshimiwa Rais, aliongolea suala la afya kwenye kurasa za mbele kabisa za hotuba yake na wote ni mashahidi tumemwona baada ya kuapishwa siku chache ya sehemu ambazo amezitembelea ni Muhimbili na amejionea changamoto zilizopo kwenye hospitali zetu za Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto zilizopo Muhimbili hazina tofauti sana na changamoto zilizopo Mkoani kwetu Mwanza. Tuna hospitali ya referral ya Sekou Toure. Hospitali hii inahudumia watu wengi sana na inatoa huduma nzuri sana na ndiyo maana nadhani watu wanakuwa wengi na wazee, akina mama na watoto wanahudumiwa bure. Napenda kupongeza Serikali kwa jitihada hizi wanazozifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini changamoto bado ni nyingi vilevile hapo tulipo. Moja ni ufinyu wa bajeti, bajeti inayotakiwa kwenda kwenye hospitali yetu ya Sekou Toure haiendi kwa wakati na ikienda haiendi bajeti kamili. Najua Waziri na Naibu Waziri sasa hivi tumepata ni wachapakazi na nina imani haya mambo tunayoongea hapa yatatekelezeka.
Mheshimiwa naibu Spika, kuna suala la vifaa tiba. Changamoto za vifaa tiba pia ni nyingi pale, hospitali inahudumia watu wengi x-ray iliyopo ni moja na ni x-ray ambayo imekuwepo tangu hiyo hospitali inaanzishwa. Kwa hiyo tunaomba Mheshimiwa Waziri utusaidie kwa hilo, ni hospitali ambayo inahudumia wakazi wengi sana wa Mwanza na mikoa ya jirani.
Mheshimiwa Spika, suala lingine nilitaka kuongelea ni kuhusu afya ni kuhusu hospitali ya Wilaya ya Ilemela. Hospitali hii tunashukuru sana Serikali kwa sababu inaendelea vizuri, imeshapewa hela almost 80 percent ya kazi zinazotakiwa kufanya, kwa hiyo iliyobaki ili hospitali ikamilike tuweze kupata hospitali ya Wilaya ya Ilemela ni fedha ndogo sana. Tunaomba Mheshimiwa Waziri tunapokuja kujadili bajeti utusaidie kutenga hela za hospitali ya Wilaya ya Ilemela. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna kituo cha afya cha Buzuruga. Kituo hiki cha afya kinahudumia wakazi wengi sana wa Mwanza kwa sababu kwa upande wa Ilemela hatuna hospitali ya Wilaya, kwa hiyo watu wengi sana wanajikuta wanaenda kwenye hicho kituo cha afya lakini kituo cha afya hiki pia kina changamoto na hatuna wodi ya wanaume. Kwa hiyo, wanaume wanapokuja kuhudumiwa pale hata kama wanaumwa kiasi gani cha kuwa admitted hawawezi kuwa admitted kwa sababu hatuna wodi, kwa hiyo tunaomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hili na kutupa kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la watoto njiti. Suala hili ni changamoto, watoto hawa kwenye hospitali zetu nyingi kwa Mkoa wa Mwanza hawana wodi za watoto njiti, wodi hazipo watoto hawa wakitokea wamepatikana na matatizo hayo wanachanganywa na wodi za kawaida, yaani katika wanawake waliojifungua kawaida watoto, suala hili ni nyeti sana naomba Mheshimiwa Waziri tuliangalie.
Vilevile vifaa vya kuhudumia watoto hawa kama incubators, suction machines, feeding tubes, ni vitu ambavyo gharama yake siyo kubwa sana lakini vinakosekana kwenye hospitali zetu.
Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri tunakuomba utuangalie kwenye hilo suala la watoto njiti na pia kama kuna uwezekano research ifanyike, tujue hawa watoto wapo kiasi gani na wanapatikana sana kwenye Wilaya gani ya Tanzania ili tuweze kufanya utafiti na kujua ni kitu gani kinapelekea watoto hao wanakuwa njiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja asilimia mia moja. (Makofi)