Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Martha Jachi Umbulla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi. Kwanza mimi nimshukuru Mwenyezi Mungu anayetupa zawadi ya uhai kwa wote humu ndani na kuendelea na shughuli zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sitatenda haki bila kuishukuru Serikali yetu kwa kuweka kipaumbele katika Wizara ya Afya kuhakikisha kwamba inaboresha maisha ya Watanzania walio wengi. Kipekee pia na mimi nimpongeze sana Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, kwa kweli mdogo wangu na mwanangu umeweka alama katika nchi yetu, hongera sana. Pia nimpongeze Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara yako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mengi mazuri ambayo yamefanywa na Serikali yetu, ninaomba kushauri kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa tatizo la vifo vya akina mama wajawazito na watoto ni tatizo sugu katika nchi yetu, miaka nenda rudi tumekuwa tukipewa takwimu za kupanda na kushuka kuhusu tatizo hili ambalo limeshindikana kabisa kuisha. Namuomba Mheshimiwa Waziri kama ambavyo tunaona anaweka alama, tunamuomba ahakikishe kwamba suala hili la vifo ambavyo siyo vya lazima vya akina mama wajawazito naomba alitafutie ufumbuzi. Kwa kuwa sekta ya afya ni sekta mtambuka, naishauri Serikali itenge bajeti kwa kila wizara kuhakikisha kwamba suala hili la vifo vya wanawake wajawazito kila mwaka tunaloambiwa na kwa kuwa changamoto zake zinafahamika zinaweza kutatuliwa, ziweze kufutwa kama ambavyo nchi yetu imeondoa tatizo la ndui katika nchi hii na hili tatizo liwe historia. Naiomba kila Wizara itenge bajeti ili kutatua tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kuna tatizo sugu la malaria, malaria inaua Watanzania walio wengi kuliko ugonjwa wowote hapa nchini. Ninaiomba Serikali kwa kusaidiana na fedha na wafadhili wengi ambao wanatoa fedha katika eneo hili nalo hilo eneo liweze kuangaliwa kwa sababu changamoto zake zinajulikana, zinatatulika na lenyewe liweze kufutwa ili nchi yetu iwe salama kwa ugonjwa wa malaria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie haraka haraka usambazaji wa dawa kwa asilimia zaidi ya 80 katika maeneo ya vijijini. Naipongeza Serikali kwa hilo, lakini inasikitisha pia kuona juhudi ya Serikali kubwa kwa kiasi hicho maeneo ya pembezoni hususan Mkoa wa Manyara, Hospitali ya Mkoa ya Mrara, Hospitali za Wilaya na vituo vya afya havina dawa za kutosha wananchi bado wanaambiwa wakanunue madawa pembeni. Tunaoimba hili nalo ulivalie njuga uhakikishe kwamba kama kuna hujuma ya aina yoyote, wahusika wote waweze kuchukuliwa hatua hadharani ili iwe fundisho kwa sababu tatizo hili Serikali imekwishalimaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia huduma za Madaktari Bingwa kwa sababu nimeona kwenye kitabu cha Waziri ameizungumzia, kwanza nimshukuru kwa hilo. Huduma za Madaktari Bingwa inahitajika kwa sababu magonjwa sugu yapo vijijini, nitoe mfano wa ndugu yangu ambaye alipata mild stroke huko Kambi ya Simba - Karatu na badala ya kupewa huduma ya Udaktari Bingwa pale alipo akasafirishwa umbali wote huo zaidi ya kilometa 200 kwenda KCMC kumbe angeweza kushauriwa kwamba na hatujui kwamba aweze kupumzishwa, apewe huduma ya kwanza na baada ya hapo aweze kusafirishwa kwenda kupata huduma. Sasa hilo lilipoteza maisha na ninaomba kwamba Serikali iweze kuliona hili, imekwishaliona lakini iweze kuweka msisitizo kupeleka huduma bingwa katika maeneo ya vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuzungumzia pia suala zima la Wizara ya Afya kuweza kutenganishwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Michango mingi humu ndani ambayo tumeisikia, katika watu kumi pengine ni mtu mmoja amezungumzia masuala ya wanawake. Mimi nilikuwa natoa ushauri Wizara ya Afya ni Wizara kubwa sana na inameza kabisa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto. Ninaiomba Serikali ione ni namna gani inaweza kutenganisha Wizara hizi mbili ili huduma hizi za masuala ya wanawake yaweze kusambaa na ipate upana mrefu wa kuweza kushughulikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru na ninaomba kuunga mkono hoja hii kwa asilimia 100, nitachangia kwa maandishi.