Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Risala Said Kabongo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia Wizara hii ya Afya. Kwanza kabisa natambua jitihada za Waziri wa Afya pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya ya kusimamia afya ya mama na mtoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita kwa akinamama ambao wana matatizo ya kupata ujauzito. Tatizo hili ni kubwa sana hapa nchini na linasababisha unyanyapaa pamoja na ndoa nyingi kuvunjika. Waathirika wakubwa wa tatizo hili ni wanaume na wanawake lakini inakuja kutokea kwamba wanawake ndiyo wanakuwa wanabeba tatizo hili. Kwa hiyo, namwomba Waziri aendelee kusimamia jambo hili ili wanawake wapunguziwe suala hili la unyanyapaa unaotokana na matatizo unaotokana na matatizo ya kupata ujauzito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie Dar IVF clinic ambayo ni clinic inayotoa matibabu kwa akinamama hawa wanaoshindwa kupata ujauzito; hospitali hii imekuwa ikisaidia sana wanawake wanaoshindwa kupata ujauzito na wanawake wawili mpaka watatu wanahudumiwa kwa siku. Tunaweza kusema kwamba wanawake zaidi ya 50 wanahudumiwa matatizo haya ya kupata ujauzito kwa maana ya kupandikizwa watoto au kusaidiwa njia mbalimbali za kupata uzazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za matibabu ni kubwa sana kwenye suala hili. Mwanamke au familia inaingia kwenye gharama ya dola 7,000 au 8,000 hadi dola 10,000 kwa mwanamke kupata matibabau haya. Familia nyingi zinauza rasilimali lakini pia zinaingia katika mikopo kuingia katika kusaidia wanawake hawa kupata ujauzito. Ushauri wangu kwa Serikali ili kupunguza gharama hizi kwa familia dawa zinazotoka nje ili kusaidia wanawake hawa kupata ujauzito zina gharama kubwa, lakini pia nataka kuishauri Serikali pamoja na Wizara hii kuondoa kodi kwenye dawa hizi ili ziweze kupatikana kwa urahisi, lakini pia kuondoa vizuizi vingi vinavyoambatana na uingizwaji wa dawa hizi ili tuweze kusaidia wanawake hawa na kuondoa urasimu pia ambao unapelekea dawa hizi kuchelewa kuingia nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ningependa kushauri Wizara ya Afya kusaidia dawa hizi kama zinaweza zipatikana kwenye MSD ili tuweze kuzipata kwa urahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kuishauri Wizara ni Madaktari Wataalam, kama ilivyofanywa kwenye Taasisi ya Moyo kupandikiza Figo tunaomba Wizara itafute hawa wataalam ambao wanaweza kusaidia zoezi hili kwenye hospitali zetu za rufaa ili tuweze kusaidia wanawake hawa kupata ujauzito kwa gharama nafuu. (Makofi)

Mhesimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la tatu, nataka pia Wizara ione namna gani tunaweza kutoa elimu kwa jamii ili kuona tatizo hili siyo la wanawake pake yao bali na wanaume pia wanahusika. Hii litasaidia sana kuondoa unyanyapaa kwa wanawake ambao wanashindwa kupata ujauzito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie pia kwa kumpongeza Waziri wa Afya na Naibu wake tena kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya, lakini niwaombe kwenye zile zahanati zetu kwenye maeneo ambayo tunatoka kwenye Majimbo yetu, kwenye Mikoa yetu ziboreshwe kuna tatizo kubwa sana la maji kwenye zahanati zetu. Tunaomba namna ambavyo tunakarabati zahanati zetu tuweke gata ili kuweza kuvuna maji ya mvua na itasaidia sana kuweza kupata maji katika zahanati zetu na watu waweze kujifungua kwa usalama zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.