Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda sana kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mola)aliyetuwezesha, ambapo ilikuwa siku ya kwanza, ilikuwa asubuhi, ilikuwa jioni, tukakamilisha siku ya kwanza. Tukaenda hivyo mpaka leo tumefika ilikuwa asubuhi na itakuwa jioni siku ya sita na tutakamilisha jukumu letu tulilopewa katika Wizara hii kuwasilisha hoja hii mezani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa dhati ya moyo wangu sana naomba nimshukuru sana Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, aliyenipa dhamana kubwa sana ya kusimamia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ambayo ina watumishi takribani 388,000 sawa na watumishi asilimia 74.02 ya watumishi wote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru Spika, nikushukuru wewe kwa kazi kubwa na Wenyeviti wa Kamati, pia niwashukuru sana viongozi wote wa Kamati ya Utawala na TAMISEMI, ikiongozwa na mkubwa wangu Mheshimiwa Jasson Rweikiza na Mheshimiwa Mama Mwanne Mchemba, lakini wapiganaji wote wa Kamati hii walikuwa wametoa maelekezo ya kutosha mpaka na sisi tukapata umahiri wa kuweza kuwasilisha hoja hii hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa dhati ya moyo wangu niwashukuru Wabunge wote. Michango ilikuwa mizuri sana yenye afya ambayo kwa namna moja au nyingine inatuwezesha kama Wizara tuone nini tunapaswa kufanya katika mwaka wa fedha 2018/2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishukuru familia yangu kwa msaada mkubwa. Mkiona ninapendeza maana yake nyuma kuna watu wanafanya shughuli hiyo, lakini niwashukuru watoto wangu wote, najua wengine saa hizi wako masomoni, Mungu awafanyie wepesi masomo yao yaende vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana, baba yangu amefariki, nimshukuru sana mama yangu mzazi kwa malezi mazuri. Siku zote amekuwa mama mlezi kwa kipindi chote, namshukuru sana mama yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Kisarawe. Mjadala huu unavyoendelea walikuwa wakiufuatilia japokuwa katika vipindi vya vipande vipande, wengine wakati mwingine wanakaa mpaka saa sita usiku, saa tano usiku, kuona mjadala jinsi gani unaendelea katika ofisi abayo nimepewa dhamana Mbunge wao kuweza kuisimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja hii ilikuwa ni hoja nzito, Wabunge waliochangia kwa kweli wamepatikana takribani
123. Kati ya hao Wabunge 71 walichangia kwa kuzungumza hapa Bungeni na Wabunge takribani 52, wengine walikuwa wanaongezeka saa hizi kwa maandishi, hawa wamechangia kwa maandishi. Najua kwa mujibu wa mwongozo wa kanuni zako na suala zima la muda, naomba Wabunge wote mliochangia mridhie kwamba kumbukumbu yenu itaonekana katika Hansard za Bunge za Taarifa yetu hii ya Wabunge waliochangia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kusema ukweli hoja zimekuwa nyingi, lakini hoja hizi zote nazichukulia kwamba ni hoja zilizolenga kujenga mwenendo na utendaji mkubwa wa Wizara yetu. Hoja ya kwanza ambayo Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Rweikiza, mkubwa wangu na ninaomba Wabunge wengine wote mridhie, sitaki kuwataja Wabunge hapa kwa majina inawezekana mtu mwingine nikamuacha ikaja kuwa nongwa, kwa nini nimesema, lakini sijatajwa. Naomba wote tuliozungumza tubebwe na Mwenyekiti wa Kamati ya Utawala na TAMISEMI. Akitajwa yeye basi, chukulia na mimi nimetajwa katika hoja hiyo kwa sababu nilichangia Bungeni. Maana naweza nikasema dada yangu Mheshimiwa Zainab Mndolwa hapo, wengine wakasema kwa nini umemtaja yule peke yake na mama Kauthar yupo hapa jukwaani ikawa nongwa hapa shughuli ikaanza kwa nini umemtaja yule peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hoja ambayo ilionekana Wabunge wengi wamechangia, Mwenyekiti wa Kamati alizungumzia ni suala zima la mapokezi ya fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Hoja hii ukiiangalia imetamalaki mahala mbalimbali, hata katika hoja za CAG katika vipindi tofauti ilikuwa ikielekeza jinsi gani fedha hazifiki katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Kamati yetu ya Utawala Mheshimiwa Rweikiza amezungumza hapa kwamba ndiyo hoja ambayo hata katika Kamati walizungumza sana. Naomba nikiri wazi kwamba hoja hii ni ya kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo ni-appreciate juhudi kubwa za Serikali kwa sababu kwa ujumla wake kutoka Hazina kwa kipindi hiki cha sasa hivi katika mwaka wa fedha 2017/2018 mpaka tunapofika mwezi Februari tumeweza tumepokea takribani shilingi bilioni 231.33 sawa na asilimia 50 ya fedha za mengineyo. Hata hivyo, katika suala zima la maendeleo tulipokea jumla ya shilingi bilioni
914.39 sawa na asilimia 50 ya bajeti iliyokuwa approved ya mwaka wa fedha 2017/2018. Hata hivyo, ruzuku ya maendeleo inatolewa kulingana na ukusanyaji wa mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika imani yangu kubwa kwamba kwa sababu bajeti iliyotolewa mpaka mwezi Februari mwaka huu tumefika asilimia 50, lakini hapa katikati tunatarajia kupokea pesa za ile miradi viporo ambayo ninyi Wabunge tuliwaita, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi na Maafisa Mipango. Hazina inafanya harakati nadhani kabla ya mwezi Juni tutapata baadhi ya fund ya fedha imani yangu kubwa mwaka huu wa fedha kiwango cha fedha kilichopokelewa kitazidi kuongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala hili naomba sana niwahimize wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninachoamini ni kwamba fedha zote zinatoka katika Mfuko Mkuu wa Serikali, tunapaswa katika ile ajenda ya pamoja kama Taifa, kuhamasishana suala zima la watu waweze kulipa kodi ambapo naamini kodi ikilipwa Mfuko Mkuu wa Serikali hautaona aibu kupeleka pesa katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, katika mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 tumetenga miradi mikakati. Ajenda yetu ni nini? Licha ya Halmashauri kutegemea fedha zile kutoka Serikali Kuu lakini miradi ya Halmashauri ibuni miradi ambayo itasaidia kuchagiza upatikanaji wa fedha katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Katika hili niwasihi Wabunge wote katika Kamati zetu za Fedha kule katika Halmashauri zetu tusiwaonee aibu Maafisa Mipango, badala ya kubuni mipango wao wanakaa tu Maafisa Mipango haiwezekani. Haiwezekani leo hii kuna Halmashauri zimepeleka miradi mikakati mpaka leo hii lakini kuna Maafisa Mipango wengine wamelala msikubali Waheshimiwa Wabunge katika Halmashauri zenu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha imetengwa kwa lengo kubwa kuhakikisha kwamba tunapata watu mahiri kwa ajili kuhakikisha wanafanya resource mobilization tupate fedha katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, jambo hili nina imani kwamba kama Taifa kwa pamoja tutaweza kufika mahala pazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine lilikuwa ni suala zima la TARURA bahati nzuri msaidizi wangu Mheshimiwa Kakunda amelizungumza hapa kwa kina, lakini kama tunavyofahamu ni kwamba hii ni taasisi mpya ambapo mtandao wa barabara kama nilivyosema awali tuna mtandao wa barabara takribani kilometa 145,000, lakini kilometa karibuni 108,000 zote zinasimamiwa na TARURA maana yake changamoto ni kubwa, lakini ukiangalia mgao wa bajeti ambayo tunaitegemea ni ile asilimia 30 kutoka Road Fund. Wabunge mlisema hapa kwamba ikiwezekana formula iweze kurekebishwa. Waziri Mkuu wakati anazindua TARURA mwezi Julai, 2017 alilizungumzia hili kwamba Serikali ikae na jambo hili tunalifanyia kazi kama Serikali kwa pamoja kuona namna gani bora vipi baadaye, TARURA kiwe chombo kinachoweza kusimama kipate fedha kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanaozalisha uchumi, kule maeneo ya vijijini ambao mazao na mifugo inakotoka waweze kusafirisha malighafi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo Serikali tunaenda kulifanyia mpango mpana zaidi tuangalie ikiwezekana vyanzo vingine vya mapato, maana yake hata tukiitegemea mgawanyo huu hatutoweza kujibu shida za mitandao ya barabara ya kilometa 108,000.9. Ni lazima kama Wabunge wote endapo Serikali itakuja na mpango mkakati wa kutafuta fedha, kuhakikisha fedha hizi zinakuwa ring fenced kuenda kujibu matatizo ya barabara vijijini, naomba Wabunge wote tuungane na Serikali katika ajenda hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo limezungumzwa sana na Waheshimiwa Wabunge wengine, nimesikia akina Mheshimiwa Lusinde walisema barabara zetu, madaraja yetu, kule Nzega kuna daraja kule la ndugu yangu Mheshimiwa Bashe maeneo yote ya nchi hii, ndugu yangu Mheshimiwa Lubeleje alizungumza barabara zake za Mtanana, tunayafahamu haya Wabunge wote naomba niwaambie. Ajenda yetu kubwa ni kuhakikisha tutabaini barabara zote, lakini tutaisimamia TARURA iweke legacy katika nchi hii ni taasisi inayofanya vizuri kuboresha miundombinu ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha ajenda ya TARURA, jambo lingine lililojitokeza ni suala zima la uwekezaji wa elimu msingi bila malipo. Kwanza tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kila mwezi kuanzia mwezi Disemba, 2015, Serikali ilikuwa ikitoa bajeti ya fedha takribani shilingi bilioni 23 kwa ajili ya ku-service suala zima la programu ya elimu bure. Hata hivyo mwaka jana tulikwama, Wabunge wengine ninyi mlisema humu ndani kwamba fedha zile hazitoshi. Tulimuomba Mheshimiwa Rais akasema tusubiri mwaka wa fedha umefika sasa, bahati nzuri mwaka huu tumepata additional fedha karibuni 3.6 bilioni ambayo inaongezeka katika suala zima la elimu msingi bila malipo. Jambo hili litatupa nguvu kuhakikisha programu hii inaenda vizuri, kwa sababu nikijua wazi kwamba kuna wanafunzi ama watoto walioongezeka wengi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili naomba nikiri kwamba jambo hili Watanzania naomba niwasihi Wabunge tuache kubeza mambo mengine ambayo yana maslahi mapana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya Wabunge wamesema mpango huu hauna maana yoyote, ndugu zangu naomba niseme kuna watoto wa maskini ambao walikuwa wanashindwa kabisa kupata elimu, tuone kwa nini mwaka 2016 Januari mara baada ya suala zima la elimu msingi bila malipo, kwa nini tuliweza kuwapokea mpaka watoto wenye umri wa miaka kumi wanataka kuja kuanza darasa la kwanza. (Makofi)

Kuna wakati mama mjane, baba amepotea, ana mtoto wake anataka kumpeleka shule lakini anaambiwa lete uniform, lete dawati, mchango wa shule wanashindwa, lakini baada ya elimu msingi bila malipo tumeona watu wengi wakiwatoa watoto waliowaficha, waliokuwa wakiwatwisha vikapu vya vitumbua na karanga, sasa wamepelekwa shule. Kwa hiyo, jambo hili ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nafahamu jambo lolote lenye mafanikio lina changamoto yake, changamoto ndio suala zima la ujenzi wa madarasa, madarasa yanakuwa pungufu, madawati na hali kadhalika walimu. Hata hivyo, naomba niwaambie Serikali haikulala, Serikali katika mwaka huu wa fedha tumeamua kuwekeza vya kutosha. Inawezekana kuna bajeti zingine msizione katika vitabu hivi lakini naamini mtaviona katika mpango wa Serikali katika maeneo mbalimbali hasa vilevile katika suala zima la Wizara ya Elimu, ndiyo maana mwaka huu mnaweza mkaona tutakuwa tunafanya arrangement ya ndani ya Wizara kati yetu na Wizara ya Elimu, inawezekana watu wengine wanahoji kwanini fedha nyingi za miundombinu hatuzioni TAMISEMI wakati ninyi ndiyo mnaojenga madarasa na vyoo vya shule za msingi Kamati ilisema, hili tunalifanyia kazi mtaona ujenzi wa madarasa, ujenzi wa vyoo, ujenzi wa nyumba za walimu jinsi gani Serikali imejipanga kwenda kujibu matatizo katika sekta ya elimu katika nchi yetu.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ambayo ndugu yangu Mheshimiwa Bashe alizungumza hapa kwanini TAMISEMI inaonekana bajeti zake zote zimeenda katika recurrent expenditure. Kama nilivyosema, TAMISEMI ukiiangalia bajeti ya mishahara recurrent expenditure yote ni ya nchi nzima mwaka huu ni trilioni 7.4; lakini bilioni 4.1 yote ni mishahara kwa watumishi waliopo chini ya ofisi ya Rais, TAMISEMI, hata katika bajeti process obvious utaona gharama hizi zinaongezeka kwa kiwango kikubwa kwa sababu bajeti peke yake katika ofisi hii inachukua asilimia 56 ya bajeti ya mishahara ya nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata leo Wabunge mkisema kwamba walimu waongezewe mishahara, wauguzi waongezewe mishahara maana yake unaongeza recurrent expenditure kwa ajili ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI ni jambo jema, kwa hiyo msishangae ndugu zangu kwamba bajeti peke yake ni trilioni 1.8 ya development budget out of trilioni 6.58 ni kwa sababu ni kwamba watumishi wengi na transaction nyingi za kiutumishi ziko katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa mambo ambayo yalitamalaki sana ni suala zima la ujenzi wa miundombinu ya afya. Tumetoka mbali na hapa nilisema siku nilipo-table hotuba bajeti yangu, Tanzania tumetoka mbali ukiangalia hospitali za wilaya, vituo vya afya, zahanati changamoto ni kubwa, nilisema wazi tutafika kipindi ambacho nchi hii imeweka historia, Mheshimiwa Dkt. John Pombe ameweka historia, ataweka historia kubwa ndani ya miaka hii mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii katika vituo vya afya, nenda Hospitali ya Amana, nenda Muhimbili, nenda kokote, nenda hata hospitali ya Tabora pale mtani wangu siku ile juzi alivyokuwa anachangia hapa Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, idadi ya watu wamejazana ni kwa sababu hatuna back up strategy kule katika ngazi zetu za kata, hatuna vituo vya afya vyenye kufanya upasuaji ndiyo maana mama kama hitaji la upasuaji ni lazima aende katika Referral Hospital.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli chini ya Serikali ya Awamu ya Tano ndiyo maana ajenda ya kwanza tumeanza kujenga vituo vya afya 208 kwa mara ya kwanza. Vituo hivi ni historia ambayo haijawahi kuwekwa kipindi chochote cha nchi hii kuweza kuweka miundombinu, tena niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge nilisema tutapeleka fedha hizi kwa kutumia force account na Wabunge kweli mmesimamia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika watu wanaostahili heshima kubwa ni Wabunge ninyi mmeweka historia kusimamia fedha zile kwa force account. Shilingi milioni 500 kwa mwanzo ukizipeleka katika Halmashauri wakatumia Wakandarasi tu hakuna kitu, lakini tulielezana, tulikubaliana, mkaenda kusimamia, sasa mafanikio makubwa yamepatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hiyo tu mwaka huu katika bajeti tumeamua kujielekeza katika suala zima la ujenzi wa hospitali za Wilaya. Hili lilikuwa ni tatizo kubwa sana Dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama siku moja amekuja ofisini kwangu ametoka “jicho nyanya” anaomba Hospitali ya Wilaya kwake, anasema mimi Waziri mzima sina Hospitali ya Wilaya, sasa kawape salamu wale watani zangu wa Songea kwamba kule unaenda kujenga Hospitali ya Wilaya ya kwako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa faida ya nchi hii naomba nizitaje Hospitali ya Wilaya hizo kila mtu aweze kujifahamu. Tutajenga Hospitali za Wilaya 67 mwaka huu kwa maelekezo maalum na ramani maalum, wataalam wangu nimewatuma kazi hiyo, wakishirikiana na watu wa Wizara
ya Afya, Mkoa wa Arusha tukianza tunajenga Hospitali ya Wilaya ya Longido na Ngorongoro, katika Mkoa wa Dodoma tunajenga Hospitali ya Wilaya ya Chamwino, Bahi na Chemba, katika Mkoa wa Dar es Salaam tunajenga Wilaya ya Kigamboni na Wilaya ya Ilala kwa rafiki yangu pale Mheshimiwa Mwita Waitara pale Kivule tutaenda kujenga, katika Mkoa wa Geita tutaenda kuweka Geita DC na Nyang’hwale; Katika Mkoa wa Iringa tutajenga Mufindi, Kilolo pamoja na Iringa; katika Mkoa wa Kagera tunaenda kujenga Kagera DC, Karagwe na Kyerwa, Mkoa wa Kigoma tutaenda kujenga Uvinza, Buhigwe na Kasulu; Mkoa wa Katavi tutaenda kujenga Mlele, Mpimbwe na Mpanda; Mkoa wa Kilimanjaro tutaenda kujenga Siha na Rombo. Siha tunaenda kumalizia pale na Rombo kwa Mheshimiwa Joseph Selasini tunaenda kujenga; Mkoa wa Lindi tunaenda kujenga Ruangwa na Lindi DC kwa rafiki zangu hawa akina Mheshimiwa Bobali na mwenzake Mheshimiwa Dismas Bwanausi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Manyara tunaenda kujenga katika Wilaya ya Mbulu DC na Wilaya ya Simanjiro; Mkoa wa Mara tunaenda kujenga Bunda DC, Musoma na Rorya; Mkoa wa Mbeya tunaenda kujenga Busokelo, Mbeya DC na Mbarali; Mkoa wa Morogoro tunaenda kujenga Gairo, Morogoro na Malinyi; Mkoa wa Mtwara tunaenda kujenga Mtwara DC, Nanyamba pamoja na Masasi; Mkoa wa Mwanza tunaenda kujenga Buchosa pamoja na Ilemela; Mkoa wa Njombe tunaenda kujenga Wanging’ombe, Njombe DC pamoja na Makambako; Mkoa wa Pwani tunaenda kujenga Kibiti, Kibaha DC pamoja na Kibaha TC; katika Mkoa wa Rukwa tunaenda kujenga Nkasi, Sumbawanga na Kalambo.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Ruvuma tunaenda kujenga Nyasa, Songea DC pamoja na Namtumbo, Shinyanga tunaenda kujenga Shinyanga DC, Ushetu pamoja na Bariadi; Mkoa wa Simiyu tunaenda kujenga Itilima pamoja na Busega; Mkoa wa Singida tunaenda kujenga Singida DC tena tunaipeleka kule Ilong’ero ambapo watu walikuwa wanalilia sana muda wote pamoja na Mkalama DC; Mkoa wa Songwe tunaenda kujenga Ileje DC pamoja na Songwe DC; Mkoa wa Tabora tunaenda kujenga Uyui pamoja na Sikonge. Mkoa wa Tanga tunaenda kujenga Korogwe, Tanga DC pamoja na Muheza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo tunaenda kutafuta fursa zingine katika baadhi ya maeneo kuhakikisha jinsi gani tutafanya tupate fedha zingine kama tulivyofanya katika vituo vya afya kuhakikisha tunaenda kuongeza Hospitali za Wilaya kwa kadri itakavyowezekana katika mwaka huu wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili najua ndugu zangu wa Tanga pale Korogwe walikuwa wamepanga hospitali ile ijengwe Korogwe TC, lakini katika suala zima la proper resource allocation Hospitali ya Korogwe iko pale Mjini Korogwe DC, ikaonekana siyo vema twende tena tukawapelekee Korogwe TC pale pale. Kwa hiyo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imefanya maamuzi hospitali tunaenda kujenga kwa Maji Marefu, wale wa Korogwe DC hospitali yao wataipeleka Korogwe TC kwa ajili ya wananchi waweze kupata huduma vizuri. Haya ndiyo mambo ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mambo mengine ni suala zima ni ajenda ya viwanda. Niwashukuru sana Wabunge kuna siku ambayo tumethubutu hapa. Mheshimiwa Rais ajenda yake ni kwamba jinsi gani tutafanya uwekezaji wa viwanda katika nchi yetu na ndiyo maana katika ofisi yetu tukaona kwamba tuna Wakuu wa Mikoa, tuna Wakuu wa Wilaya na Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa. Tutafanya vipi tuunge mkono ajenda hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliamua kutoa maelekezo kuwa Mikoa yote ijenge viwanda 100 katika kila Mkoa kwa mwaka mmoja. Bahati nzuri tarehe 20 Machi, Wakuu wa Mikoa tulikutana hapa Dodoma kufanya tathmini ya kwanza ndani ya miezi mitatu tumefanikiwa vipi katika jambo hili. Bahati nzuri ndani ya miezi mitatu tumejenga viwanda vidogo 1,285, ujenzi wa viwanda hivi ni sawa sawa na asilimia
49.4 ya utekelezaji wa lengo. Mimi naomba niwapongeze Wabunge wote katika maeneo yenu, lakini niwapongeze Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Mamlaka ya Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana Maafisa Maendeleo ya Jamii tuliwaita hapa kwa ajili ya kuwapa terms of reference, nini wanapaswa kufanya katika suala zima la ujenzi wa viwanda, tumeanza kupata mafanikio makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi viwanda vidogo ndugu zangu ndivyo vinavyoajiri watu wetu kati ya wanne, watano mpaka 10. Viwanda 1,285 hata kiwanda kimoja kikiwa na wastani wa kiwango cha chini watu watano, unazungumza takribani watu karibuni 6,000 wamepata ajira ndani ya miezi hii mitatu. Haya ni mafanikio makubwa ambayo naomba Waheshimiwa Wabunge tuungane kwa pamoja katika suala zima la ajenda hii tutafanya vipi zaidi kuongeza ajira kwa vijana wetu na mwisho wa siku tutaenda kujenga uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika ofisi hii mambo ni mengi na jambo lingine ambalo lilijitokeza ni suala zima ambalo Mheshimiwa Dunstan Kitandula alilizungumza hapa, kwamba ameona hotuba yote mwanzo mpaka mwisho haina habari ya mambo ya lishe. Tena anasema Mheshimiwa Selemani Jafo ulikuwa miongoni mwa wapiganaji wa lishe! Naomba niwaambie budget speech maana yake inatoa summary ya baadhi ya mambo mengi huwezi uka-capture yote, lakini kuna majedwali, kuna vitabu mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 katika bajeti ya mwaka huu tumetenga takribani shilingi bilioni 15 tumetoka shilingi bilioni 11 tumeenda shilingi bilioni 15 ambapo hii maana yake tunaenda kujibu, hata hivyo siyo kutenga fedha kwa mara ya kwanza kutokana na agizo la Makamu wa Rais tuliamua kuwasainisha mikataba Wakuu wa Mikoa wote nini wanapaswa kufanya katika suala zima la afya haswa suala la lishe, tunajua wazi leo hii hatuwezi kupata watoto ambao wanasoma vizuri kama lishe yao itakuwa ni tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema suala la udumavu, mtoto akipata udumavu katika siku 1,000 za kwanza, mtoto huyo hata akiwa mkubwa anakuwa poyoyo hawezi kuelewa hata mwalimu akimfundisha. Mwalimu akimwambia Juma sema ‘a’ na yeye anasema Juma sema ‘a’ haelewi lolote! Lazima tuwekeze katika suala zima la lishe. Hivyo, Mheshimiwa Kitandula na Wabunge wote naomba niwaeleze kwamba mwaka huu tumechanga sekta ya lishe shilingi bilioni 15 ili kuhakikisha kwamba tunatengeneza kizazi kilicho imara kwa ajili ya kuhakikisha kwamba watu wote wanaenda vizuri katika suala zima la lishe na kupambana na udumavu.

Jambo lingine lilikuwa suala zima la mifumo ya elektroniki, naomba nishukuru sana, mwanzo ukusanyaji wetu wa mapato ulikuwa na changamoto kubwa na ripoti ya CAG ilikuwa inazungumza wazi jinsi gani uvujifu wa mapato umekuwa ukiendelea kila siku, lakini hata hivyo tumejitahidi sana hivi sasa makusanyo ya mapato yote sasa tunatumia mifumo ya elektroniki, hata hivyo hatutegemei tena huko tunakokwenda baadaye watu kutumia vitabu vya risiti ya kawaida, lengo letu ni kuzisaidia hizi Halmashauri ziweze kukusanya mapato ya kutosha kwa lengo kubwa ni kwamba Halmashauri zetu zikiwa na nguvu kubwa ya kiuchumi zitaweza kufanya mambo sahihi mengi sana katika suala zima la kuendeleza maendeleo katika Wilaya zetu.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine lilikuwa suala zima la posho ya Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji. Jambo hili tumelichukua kama Serikali, ninafahamu wazi tulipokuwa katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere pale Dar es Salaam Madiwani wote kupitia kwa Wenyeviti wao wa Halmashauri na Mameya walileta hoja hii na Mheshimiwa Rais alisema tumeichukua hoja hii, tunaweka vizuri mfumo wa kiuchumi wetu pale utakapokuwa vizuri basi tutaangalia jinsi gani jambo hili tuweze kulitendea wema kwa kadri itakavyofaa.

Kwa hiyo, hoja hii ni hoja ya msingi tunawashukuru Waheshimiwa Wabunge, tumeipokea tutaendelea kuweka miundombinu vizuri ya ukusanyaji wa mapato na kuangalia pale tutakapokuwa na hali nzuri tutaliwekea utaratibu mzuri wa wananchi na hasa Madiwani wetu ambao wanafanya kazi kubwa sana. Naomba nikiri wanafanya kazi kubwa iliyopitiliza tuweze kuangalia ile posho yao iweze kuongezeka ili waweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ni suala zima la maeneo mapya ya utawala. Hoja hii imechangiwa na Wabunge wengi, tumesikia kwamba mtaa mmoja una watu karibu 20,000, kule Mondole na Msongola tumesikia hilo akina Mheshimiwa Malembeka wakilalamika, naomba tulichukue jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la uwezeshaji wa mamlaka mpya na hasa katika sehemu zile za wilaya; kwa mfano kaka yangu Mheshimiwa Malocha alizungumzia sana jimbo lake, maana Jimbo lake lipo kama mbalamwezi, ana changamoto kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuseme tumeyachukua haya, lakini tutaangalia utaratibu wa kufanya, kwa sababu lengo letu kubwa kama Serikali kwa sasa ni kujikita katika maeneo mapya tuliyoanzisha lazima kwanza tuyaboreshe, hili ndilo jambo la kwanza. Kama kuna zile special cases kiserikali tutaangalia nini cha kufanya ili kuweza kujibu matatizo ya wananchi. Lakini kipaumbele cha kwanza sasa tulichokiweka ni suala la kutatua matatizo ya zile Halmashauri na wilaya mpya kama kule Tanganyika, tulizozianzisha; lazima zisimame vizuri kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine lilikuwa linahusu utawala bora. Watu walizungumza kwamba kuna wakati mwingine watu wanatumia vibaya madaraka yao. Sheria ipo ndiyo , ya kumuweka mtu kizuizini, lakini viongozi wanatumia madaraka yao vibaya. Kama nilivyosema, ni kwamba sisi tumeendelea kutoa mafunzo awamu kwa awamu. Hivi sasa nilisema wazi kwamba yale ni mafunzo ya utawala tuliyoyamaliza kwa Wakurugenzi pamoja na Wakuu wa Wilaya; na hapa katikati tutatoa tena mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo ninyi Waheshimiwa Wabunge mnafahamu; hata humu ndani ya Bunge kwamba tabia hatufanani hata siku moja, ndio tabia ya binadamu. Kwa hiyo, kuna vitu vingine vinaweza vikarekebishika lakini vingine ni mambo ya kibinadamu. Hata hivyo jukumu kubwa la ofisi yetu ni kuhakikisha kwamba tunasimamia utaratibu. Tumesikia Waheshimiwa Wabunge, tutalisimimamia jambo hili na hasa maeneo mbalimbali yenye changamoto kubwa tutayaweka sawa ili yaweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengine hata wiki hii iliyopita nimeweza kuyatolea maelekezo, kwamba kuna baadhi ya mambo yalikuwa yamesimama, nimetoa maelekezo yale mambo ndani ya siku 14 yaanze kufanya kazi zake ili kwamba tuhakikishe utawala bora unafanya kazi yake. Nilitoa maelekezo kule Tunduma kwa Mkuu wetu wa Mkoa, na nina imani mambo yale yatakwenda vizuri na muda si mrefu ile migogoro yetu itakuwa imeisha na tutahakikisha tunawatumikia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kuna hoja nyingine ilikuwa inahusu miradi ya TSP, ULGSP, kwamba kwa nini miradi 18 peke yake, kwa nini miji minane peke yake, naona pale kaka yangu wa Kasulu, Mheshimiwa Nsanzugwanko juzi amenitumia ki-note anasema namuona Mheshimiwa Zitto mwenzangu barabara zake zinajengwa, mimi kwangu choka mbaya kwa nini na mimi ni halmashauri ya mji. Ni kwamba tulianza na miji 18 ile ambayo nimesema kuna Arusha, Tanga, Mbeya, Mwanza na miji mingineyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeamua, kama nilivyosema tumetengeneza barabara za kisasa na tunaendelea kutengeneza na mwaka 2020 tutamaliza miradi hii. Miradi ya halmashauri ya miji pamoja na Manispaa zipatazo 18 ujenzi ndio unaendelea hivi sasa. Hata hivyo hii kazi inafanyika kwa awamu. Kuna miji ambayo imesahaulika ambayo imeingizwa katika programu hii inayokuja kuna Mji wa Nzega, Mbulu TC na Kasulu, wataalam wetu wako mbioni wanaifanyia taratibu, itakapoiva tu jambo lile litakuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo letu ni kwamba halmashauri za miji zote ziwe katika ubora ule tunaoukusudia. Hata hivyo, kuna jambo lingine mahususi ambalo hata leo hii asubuhi watu wamelitolea mwongozo suala la eneo la Jangwani. Nimezungumza katika Mradi wa DMDP ajenda yake kubwa miongoni mwa yakufanya ni kwamba licha ya ujenzi wa barabara za kisasa, ujenzi wa masoko na sehemu za kupumzikia lakini ajenda yetu kubwa tumetenga takribani dola milioni 20 kwa ajili ya kuhakikisha tunalishughulikia Bonde la Msimbazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo ndugu zangu mambo haya ya majanga huwezi kuyazuia. Mheshimiwa Naibu Spika, hata nchi zilizoendelea, angalieni leo kule Marekani wakati mwingine California utakuta maji yamefurika mitaani, hali ni mbaya na wananchi wako katika hali mbaya. Hili jambo si Tanzania peke yake, inapoteokea matatizo haya ya majanga wakati mwingine hayajalishi ukubwa wala uchumi wa nchi, hayachagui. Jana tulikuwa tunaangalia kule Arusha hali ilikuwa mbaya kweli kweli katika baadhi ya maeneo, maeneo mengine yanasombwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuseme, kwamba kama Serikali kwa bahati nzuri tumeliweka kwenye mkakati, tumejipanga kutumia dola milioni 20. Pia kwa bahati nzuri hapa na Mheshimiwa Zungu kaka yangu vilevile ameniletea andiko la mpango mkakati ili kama ikiwezekana Serikali tuangalie option; nini tufanye katika Bonde la Msimbazi na eneo la Kariakoo. Jambo hili pia lote tunalichukua kwa pamoja. Nia yetu kama Serikali ni kuangalia ile njia sahihi na nzuri ili hatimaye tuweze kujibu matatizo ya Watanzania katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, naomba niseme kwamba kuna suala ambalo limezungumzwa na manaibu wangu wamelitolea ufafanuzi, suala la walimu wa kuhamishwa kutoka sekondari kwenda shule ya msingi; limeleta mkanganyiko mwingi sana. Nafahamu jambo lolote likiwa geni/jipya lina changamoto yake kubwa. Hata hivyo tufahamu kwamba lengo la Serikali ni kuwapa huduma wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, kuna baadhi ya wilaya leo hii zilikuwa na walimu wa sanaa na walimu wa arts, mwalimu wa arts tunatarajia kwamba mwalimu awe na vipindi visivyopungua 20 kwa wiki, lakini imefika wakati mwingine kuna mwalimu mwingine wa kiingereza au kiswahili wiki nzima ana kipindi kimoja tu. Akiingia saa nne asubuhi leo Jumatatu mpaka wiki ijayo saa nne asubuhi ndio anaingia darasani.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiangalia miongoni mwa maeneo ambayo tuna changamoto kubwa ni suala la masomo ya kiingereza. Leo hii nenda katika shule zetu mtafute mwalimu wa kiingereza mwambie akupigie ung’eng’e wake wa kiingereza, msikilize vizuri. Tuna walimu wengi lugha vilevile wako huku sekondari ambao hawakuwa na vipindi. Jambo la kuwachukua na kuwapeleka katika shule za msingi si baya. Hata hivyo Waheshimiwa Wabunge hoja yenu mliyozungumza, suala la induction course, hili ni jambo mahususi na zuri, tunaomba tulichukue kwa ajili ya kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nafahamu walimu hao kweli kwa sarakasi tulizokuwa tunapiga huko sekondari na huku unajua kuna elimu, kunaitwa “mlamwa luwaza” kuna mambo ya uchopekaji, kuna lugha nyingi zinatumika. Kwa hiyo huyu mwalimu wa sekondari lazima akajifunze kuchopeka huku shule ya msingi anachopeka vipi. Jamani kuchopeka inaita intergration katika lugha nyingine. Sasa kuna lugha inafundisha uchopekaji wa masomo, kwa hiyo, lazima hawa walimu, mlivyosema hoja yenu kwamba ikiwezekana wapate induction course, jambo hili kama Serikali tunalichukua kwa ajili ya uboreshaji kwa sababu tunajua ufanisi wao wa kazi utatokana na suala zima lilivyo.
(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la malipo, tumepeleka sasa hivi takribani bilioni arobaini. Katika bilioni 40; asilimia 20 ni kwa ajili ya kuwagawanya walimu; asilimia 20 maana yake tunazungumza wastani wa shilingi bilioni nane. Bilioni nane, imani yangu kubwa, Waheshimiwa Wabunge nimewasikia. Kuna wale walimu ambao tumewahamisha na wanastahili kulipwa. Ninaamini katika Halmashauri nyingine hakuna tatizo, ila kuna baadhi ya Halmashauri kweli ninakiri inawezekana matatizo yapo. Tutaweza kushughulikia case by case kutokana na halmashauri ambazo hazikufanya vizuri. Lakini nina amini Halmashauri zingine watu wamefanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo tutawaangalia wale wakurugenzi ambao tumepeleka fedha katika halmashauri yake kwa ajili ya walimu wale wanapohamishwa, kwa nini amezizuia, hazikuweza kufanya kazi hiyo; tutashughulika nao. Kwa sababu haiwezekani, tumetoa maelekezo watu wapo maofisini wanashindwa kutekeleza maeleo haya. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge jambo hili kama Serikali sisi tumelichukua kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaboresha katika maeneo mbalimbali ya utendaji wetu wa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo ya TAMISEMI yapo mengi na ndiyo maana nikiangalia hapa kila jambo ninalolitazama naona tamu, linataka ulitolee maelekezo, lakini hatuwezi kuyamaliza yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa zaidi naomba niseme wazi kwamba kuna miradi mingi sana imetengwa katika mamlaka ya Serikali za Mitaa na jukumu letu kubwa ni kuhakikisha kwamba bajeti hii ambayo mimi nitaomba Wabunge wote mridhie ipite na ipite kwa sababu ndiyo bajeti ya mishahara ya watu wetu wote. Walimu takribani 300,000 na watumishi wengine 388,000; asilimia 74.6 leo unashika shilingi unataka kuondoa shilingi, unataka kumnyima mwalimu mshahara wake? Kwa hiyo mimi nina amini wote tutakuwa katika agenda moja ya kuhakikisha hii bajeti inapita vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, naomba nikiri kwamba hoja zote za Waheshimiwa Wabunge sisi tumezipokea na zingine zitakuja kwa ufafanuzi mbalimbali wa kimaandishi na hoja hizi lengo letu kubwa si kuzisikia na kutoa maandishi, ni kwa ajili ya kwenda kujipanga kuyatekeleza. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kupitia timu yangu mahiri iliyopo hapa kuna Mheshimiwa Kakunda na Mheshimiwa Kandege tutahakikisha mwaka 2018/2019 tunakuja kuwatumikia katika majimbo na mikao yenu yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutaongeza kasi yetu ya utendaji wa kazi na tutakuja kubainisha changamoto mbalimbali zinazobainika katika maeneo yetu, lengo letu kubwa ni kwamba lazima tuwatumikie wananchi katika maeneo mbalimbali. Hata hivyo, mnajua kuna baadhi kuna mapungufu baadhi mengine yapo, hayo vilevile tutayasimamia kwa karibu zaidi. Ajenda kubwa ni kuhakikisha kwamba kila mtu katika eneo lake anaweza kutimiza wajibu wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi naomba niwasihi wahehsimiwa Wabunge, naomba tupendane sote kwa pamoja; tukipendana tukiwa na upendo bila kujalisha mipaka ya aina yoyote tutaweza kupata mafanikio makubwa kwa sababu bajeti tunayojadili leo ni bajeti inayohusu mustakabali wa nchi katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa zote. Kwa hiyo, nawasihi sana upendo kwetu ndio litakuwa jambo la msingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa ridhaa yako, kabla sijahitimisha hoja yangum naomba kutoa hoja maalum, kwamba katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Wilaya ya Handeni imetengewa shilingi bilioni
2.3 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Halmashauri. Kwa kuwa Halmashauri ya Handeni inapaswa kuhama na kujenga Ofisi katika Kata ya Kabuku, Ofisi ya Rais, TAMISEMI inaliomba Bunge lako tukufu liridhie mabadiliko ya bajeti yaliyotengwa kwa ajili ya kujenga Ofisi ya Halmashauri ya Mji wa Handeni ihamishwe kwa ajili ya kujengea Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni. Halmashauri ya Mji wa Handeni itachukua majengo ya Ofisi zitakazoachwa na Halmashauri ya Handeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo yote, naomba kutoa hoja.