Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Juma Selemani Nkamia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru sana wewe bunafsi, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia leo kuwa na afya njema. Kwa namna ya kipekee tena niongeze kukushukuru sana Profesa Dkt. Mtemi Chenge kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya Bajeti ya Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru sana na nimpe pongezi za dhati kabisa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, mwalimu wangu, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri Mkuu, Mawaziri wote na Makatibu Wakuu wote

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee kabisa uniruhusu nimpongeze sana ndugu yangu Jafo, anafanya kazi nzuri sana. Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni; nami naamini kwa kazi hii anayoifanya Jafo huwezi kujua huko mbele ya safari, kikubwa endelea kumuomba Mwenyezi Mungu, Mungu ndiye anayepanga kila kitu. Nikupongeze sana kaka yangu Kakunda na Naibu Mawaziri wote wawili, Katibu Mkuu Mzee wangu Mzee Iyombe, dada yangu Chaula na Nzunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze na suala la maji. Serikali kupitia TAMISEMI na hata Wizara ya Maji wanafanya kazi kubwa sana kwenye miradi mikubwa na miradi midogo, lakini msema ukweli ni mpenzi wa Mungu. Kama Mheshimiwa Rais ameweza kufanikiwa kupunguza ufisadi bado eneo la maji kuna ufisadi mkubwa sana kwenye miradi ya maji vijijini. Miradi mingi haikamiliki kwa wakati, miradi mingi fedha zinafujwa, miradi mingi haiko kwenye kiwango matokeo yake Serikali inaingiza fedha nyingi lakini miradi hii baada ya muda mfupi inakufa. Niombe sana jambo hili mliangalie kwa umakini na ikiwezekana Serikali undeni tume maalum kuchunguza miradi mikubwa na midogo ya maji nchi nzima kwa sababu kuna crisis kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mdogo tu, kuna mradi mmoja wa maji uko kule kwenye kijiji kinachoitwa Lahoda, nilikwenda na Mheshimiwa Waziri Kakunda. Serikali imetoa shilingi milioni 551 lakini hata tone la maji hakuna, na Waziri kaenda pale aadanganywa kwamba baada ya mwezi mmoja tutarekebisha mradi huu, maji yataanza kutoka. Waziri Kakunda akaagiza apelekewe akiba ya fedha walimwambia kuna shilingi milioni 83, hakuna hata senti tano. Kesho wanamuona Mheshimiwa Rais hafai, kumbe ni kwa sababu ya watendaji wachache. Niiombe Serikali ichukue hatua juu ya jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kule Chemba tunavyozungumza hapa, Mondo, Daki, Hongai, Chandama; tumechimba maji muda mrefu lakini two years now hakuna kinachofanyika. Niiombe Serikali, inafanya kazi nzuri sana, lakini hebu hakiksheni huko chini tunakotoka sisi miradi mingi ni useless. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nilikuwa nataka nizungumzie kidogo elimu. Nadhani kuna mahali tume-mess up. Hivi mwalimu alikuwa anakwenda darasani anakwenda anasema good morning folks, how are you? Leo unampeleka akafundishe chei chei shangazi. Si kwamba walimu hawatoshi, kuna tatizo kwenye upangaji wa walimu. Shule za mijini, hapa Dodoma Mjini kuna access ya walimu 371, shule ya sekondari ya Mpendo ina walimu wanne. Sasa hivi tatizo ni kukosekana kwa walimu au tatizo ni mpango wa walimu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, hebu fanyeni tathmini kabla ya kufanya hilo zoezi. Mnatawanya walimu bila kujua; TAMISEMI, leo mzee Iyombe uko hapa baba yangu, kwanza shikamoo.

Nikuombe, leo TAMISEMI mnapanga Mwalimu Juma Nkamia anaenda shule ya msingi Msaada. Akifika pale halmashauri anamkabidhi barua nimepangiwa shule ya msingi msaada, wapelekeni walimu acheni Halmashauri ndizo zipange waende wapi, lakini ninyi mtapanga wataenda kujazana mahali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia hivi katika shule za mjini walimu wengi wamejaa wanatoka wapi? Wengi wasichana wazuri. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia, shule nyingi za mjini wasichana wengi, wazuri tu hivi, hivi hawa wanapangwa makusudi au wanakosea? Niwaombe tu, fanyeni utafiti muone. Hapa tuna vitu ambavyo hatuendi sawasawa na matokeo yake watu wanafikia hatua wanasema; “aah, unajua Serikali ya CCM haijafanya…” si kweli! Wapo watu ndani ya Serikali wanafanya makosa kinachotukanwa Chama cha Mapinduzi, chukueni hatua! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye elimu hiyo hiyo, ajira za walimu. Ajirini walimu wa kutosha, lakini mhakikishe wanapangwa kule kwenye matatizo kweli si unaajiriwa vimemo kibao, acheni hii kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye issue ya watumishi, mimi sielewi tu. Watumishi kwenye halmashauri wengi hawatoshi, lakini nchi hii hapa katikati hapa kuna kitu tumefanya makosa makubwa sana, tumeongeza maeneo mengi ya utawala wakati hatuna resources. Hivi unaweza kuniambia uliigawaje Wilaya ya Siha na Wilaya ya Hai zikawa Wilaya mbili? Population ya pale ipoje? Hapa ni watu walitafutiwa vyeo. Tufike mahali tuangaie, kuna baadhi ya wilaya hazistahili kuwa Wilaya, vunja; Wilaya ina watu 70,000 ya nini? Ukisoma kwa sisi tuliosoma mambo ya International Relations kuna kipengele kinasema mtu anatafutiwa nafasi kwa sababu hana eneo lingine, anatafutiwa nafasi ili awe kiongozi mahali aje atafutiwe nafasi kubwa, this is wrong.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, zipo baadhi ya Wilaya vunja, kama wapo Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, kazi ziko nyingi za kufanya, wapeni hata Wakuu wa Idara tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho TAMISEMI ninyi ndio mnashughulikia Mfuko wa Jimbo, unakuta baadhi ya maeneo Wabunge hawa ile fedha ya Mfuko wa Jimbo, fanyeni tathmini upya. Tangu sheria imetungwa mpaka leo kiasi kile kile, jimbo limeongezeka, Chemba sasa hivi tuna karibu watu laki tatu na ushee, ile ile, hatuwezi kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na niishukuru sana Serikali kwa kweli, leo mimi nikitoka hapa kwenda Chemba dakika 45. Nakushukuru sana Mheshimiwa Rais, ongezeni fedha kwenye TARURA barabara zetu zijengwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru Mheshimiwa Jafo nina vituo vya afya viwili, Hamai milioni 400, Kwa Mtoro milioni 500, naomba zile za Kwa Mtoro ziingie tutulie. Umenipa bilioni moja na milioni mia tano Hospitali ya Wilaya ya Chemba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)