Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Hon. John Wegesa Heche

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii ili nami niweze kuchangia kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu wananchi wa Tarime wanichague nimekuwa na miaka mitatu hapa Bungeni. Nimejifunza mambo mengi sana na wakati mwingine fikra nilizokuja nazo hapa na kitu ninachokiona kinafanywa hapa ni tofauti kabisa na inasikitisha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1994 Rwanda iliingia kwenye machafuko makubwa sana yaliyosababisha mauaji ya zaidi ya watu milioni moja. Ukiangalia na ukifuatilia mauaji yale, kulikuwa na visasi, kupuuzwa watu, watu kuonewa, double standard na watu wakafika sehemu wakachoka kweli kweli, yakatokea matatizo makubwa kama yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hapa Tanzania kule Musoma mwaka 2010 yaliwahi kutokea mauaji mabaya ya kulipiza kisasi. Watu zaidi ya 16 kwenye familia moja wakauawa, wengi mnajua. Mbuzi wakauawa, ng’ombe, mpaka kuku na mbwa wakauawa kwa sababu ya visasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nchi hii watu wanapigwa kwa sababu wengine wanafikiri wako salama na kwa sababu wanafikiri wako kwenye madaraka, wanaona ni sawa hawa kufanyiwa hivi. Katibu wetu wa Kata ameuawa, watu wanaona ni sawa. Tundu Lissu amepigwa risasi, watu wanaona ni sawa; watu wanaonewa, mnaona ni sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wengine tunajua tuko kwenye list ya kuumizwa. Sisi wengine tumeziambia familia zetu kwamba hata kama ni baada ya miaka 10 kwa watu watakaotufanyia ubaya, lazima familia zao ziwajibike. Hili liwe kwenye record kabisa. Hatuwezi kuwa kwenye nchi ambayo imejaa upendeleo, double standard. Tunazungumza kuhusu utawala bora hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza kuhusu utawala bora. Utawala bora tunaouzungumza Mzee Mkuchika ni utawala wa aina gani? Utawala ambao leo mnakamata mtu, Polisi wanazungumza kwamba huyu mtu amejiteka, lakini yeye mnamzuia kuwaambia Watanzania kwamba yeye hakujiteka au alijiteka. Utawala bora upi? Utawala bora leo tunajua, Serikali leo duniani ni chombo cha mabavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza Bunge ndiyo chombo cha wananchi, dunia nzima ndivyo ilivyo. Leo mtu anatoa opinion yake kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 18 anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake. Jambo tunalopaswa kufanya kama Bunge ni kumjibu kwamba hili Bunge haliko hivyo kwa kuandika makala kinzani. Au huyu mtu mnafikiri kwa nini anatuona hivyo? Kwa nini hakuliona hivyo Bunge la Mama Makinda? Kwa nini hakuliona hivyo Bunge la Mzee Sitta? Kwa nini hakuona hivyo katika Mabunge mengine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili likiwa sehemu ya kutoa hukumu kwa watu wanaotutazama nasi hatuwezi kulazimisha kila mtu atuone kama tunavyojiona. Watu wana haki ya kutuona tofauti. Kila mtu ana macho yake na wewe utaona umevaa suti umependeza, mwingine atakwambia hujapendeza umevaa suti mbaya. Kwa hiyo, huwezi kuanza kumchapa kwamba amekwambia umevaa suti mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri kama Taifa, nasi tunaongea hapa, watu wanafikiri sisi ni walalamikaji. Tumewaambia mambo mengi. Mwaka juzi mligusa hapa sukari, “oh, sukari, watu wanaingiza sukari, sijui sukari, sukari! Tutaishusha bei! Sukari imepanda kutoka Sh.1,800/= aliyoiacha Mheshimiwa Kikwete, leo ni Sh.2,800/=. Mnajifanya kama hamjui, yaani mmejisahaulisha. Eti mmejisahaulisha kwamba sukari haijapanda bei. Yaani mnafikiri Watanzania hawawaoni. Hakuna anayezungumza, yaani mmejisahaulisha tu, hamjui kwamba sukari hii mlitibua bei nyie. Tukiwaambia, ooh, hawa ni watu wabaya. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwenye kitabu, msije mkasema maneno ya Heche; kitabu chenu hiki hapa cha Mheshimiwa Waziri Jafo, cha sasa hivi; Vituo vya Afya tunavyo asilimia 15. Yaani kati ya vituo 4,220, tuna vituo 696. Hapo hatujazungumzia ubora wake, hatujazungumzia vifaa vyake, hatujazungumzia wahudumu, 696 na viongozi wa dini mliowatukana kati ya hivyo vituo 600, vya kwao 183.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtemi nakuamini, nakushukuru sana. Naomba niendelee. Mama nafikiri nikimsema itakuwa mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasema, Mwalimu Nyerere ambaye ni Muasisi wa Taifa hili kama hamumheshimu, aliwahi kusema maendeleo ya vitu siyo maendeleo ya watu. Maendeleo ya watu ni pamoja na watu kuwa na afya. Mimi nawaambia CCM nyie mnaopiga kelele, Vituo vya Afya tangu uhuru kati ya 4,420 mna Vituo vya Afya 696.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa hivyo Vituo vya Afya kwa mujibu wa kitabu hiki cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri, 183 ni vituo vya Makanisa na madhehebu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema, kama ni kujenga reli, Wakoloni walijenga hata kabla ya uhuru.

T A A R I F A . . .

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. You are always firm. Nasema hivi, miaka 59 vituo vya Serikali 513; ili tujenge vituo 4,422 tunahitaji miaka 600. Mnahitaji mtoke madarakani nyie. Ndicho ninachosema hapa, a simple logic. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunakuja hapa mtu anatuambia SGR. Wakoloni walijenga reli hii. Wakati ule ndiyo ilikuwa standard gauge ya sasa hivi, wakati wakoloni wanajenga ile (Wajerumani). Watanzania na Watanganyika walikataa kwa sababu walikuwa wanawa-oppress. Kitu ambacho mnafanya nyi, leo mnatu-oppress. Sisi tukizungumza kuhusu nyie mnatuweka Polisi, mnatupeleka Mahakamani. Mheshimiwa Rais akizungumza kuhusu sisi, mkitukashifu, nyie hakuna pa kupelekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo tunasema, hata watu wa Afrika Kusini walizungumza na Makaburu wakawaandikia barua, wakafanya nini, lakini ilifika sehemu wakaunda MK kukataa ushenzi uliokuwa unafanywa na Makaburu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunachozungumza hapa ni kwamba ni lazima tuheshimiane. Ni lazima tuelewe; leo unamshtaki Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbowe, Mheshimiwa Mchungaji Msigwa, mimi na Mheshimiwa Ester, eti sisi tulisababisha kifo cha mtu (Akwilina). Yule Mkurugenzi aliyetunyima viapo ambavyo vipo kwa mujibu wa sheria, alisababisha nini? Haya mambo ndiyo tunayozungumza.